You Can Win If You Want

Mbinu za kupata furaha na amani katika maisha11 Min Read

Kupata Furaha na amani ni vitu viwili muhimu sana katika maisha ya kila mmoja wetu hapa duniani

Jambo kubwa zaidi ambalo tunalipigania ni kuwa na furaha ya kweli na amani ya kudumu katika maisha ya kila siku

Furaha na amani ipo katika kila ngazi kama:

Ngazi za furaha

  1. Ngazi ya Familia, watu huamini kuwa akiwa na mwenza atakuwa na furaha Ndio maana huamua kuoa au kuolewa
  2. Pia huamini katika watoto, kuwa akiwa na watoto atakuwa na furaha Ndio maana hutafuta watoto!
  3. katika ngazi ya uchumi, huamini akiwa na kazi, biashara, Mali na mafanikio fulani basi atakuwa na furaha hiyo hupelekea kila siku watu kupambana usiku na mchana kununua vitu kama magari, nyumba nk
  4. Ngazi ya siasa,wengi huamini kuwa na viongozi bora wenye sera thabiti katika kuleta mabadiliko ya nyanja zote na kufanya  wananchi kuwa na furaha hivyo chanzo cha  mapambano ya kisiasa kila mahala
  5. katika ngazi ya jamii, huamini kuwa jamii inapokuwa katika hali ya utulivu,  uchangamano Chanya hufanya watu wote kuwa na furaha Ndio sababu watu hufanya kila namna  kushirikina katika mambo mbalimbali ya kijamii ili kuleta amani na furaha
  6. Ngazi ya Imani
    Tunaona namna dini zinavyofundisha furaha, mahubiri yote lengo kubwa ni kuitafuta amani ya kila mmoja kupitia dini, Ndio maana watu kila mmoja kwa imani yake huamini katika furaha kupitia dini zao na kama chanzo cha kuondoa matatizo na changamoto za maisha
  7. Ngazi ya Elimu
    Elimu inaaminiwa kuwa njia kubwa inayoleta amani na furaha katika maisha ya watu kupitia kutoa ujinga na kuelewa mambo mbali mbali kupitia masomo mbali mbalimbali

Furaha ipo ndani yako

Hayo mambo yote yanapoenda tofauti, chanzo kikubwa cha ukosefu wa furaha huibuka!

Matarajio mbalimbali yanapoenda mrama  basi watu wengi hukosa amani!

Usikubali furaha yako uifuate siku zijazo au baada ya mafanikio fulani, bali furaha hupaswa kuwepo muda wote ndani yako bila kujali mazingira ya nje!

Kwanini watu hawana furaha?

Maisha yana kila sababu za kukufanya usiwe na furaha na amani hivo epuka huo mtego

Haya maisha yetu yamezungukwa na changamoto za kila siku ambazo zinafanya watu wakose amani na furaha

Changamoto zipo nyingi sana maishani ambazo ni chanzo kikubwa cha huzuni za mara kwa mara

Hata siku moja maisha hayawezi kukuweka katika mazingira ya kudumisha furaha yako!

Maana mzunguko wa maisha ya kila siku haujakaa katika kufanya mtu yoyote agande eneo moja la furaha, lazima mabadiliko ya mara kwa mara hutokea!

Lakini pia Jamii (watu) Ndio sababu kubwa zaidi ya kuleta furaha kwenye dunia ukiachilia mbali maeneo mengine yote kama Elimu, uchumi, siasa na Imani

Kama jamii ingekuwa katika uwiano Sawa, lengo moja, mshikamano, tabia zinazoendana na kuhurumiana nina amini,

Dunia ingekuwa sehemu salama zaidi yenye amani na furaha lakini jamii (watu) Ndio chanzo kikubwa zaidi cha huzuni na mvurugano

Mambo yanayosaidia kuleta furaha na amani maishani

Namna Ya kupata furaha na amani

  1.  Samehe na sahau
  2.  Usijilinganishe na wengine
  3.  Ishi ndani ya maana ya maisha yako
  4. Ondoa mahusiano mabaya
  5. Usiamini mtu kupitiliza /usiweke matarajio kwa watu na jifunze kuwa na mbadala
  6. Punguza matumizi ya mitandao ya kijamii
  7. Jifunze kushukuru
  8. Weka mipaka ya maisha yako, jiheshimu na heshimu mipaka ya wengine
  9. Epuka kusema Ndio kila wakati
  10. Jiamini na jikubali
  11.  Fanya maamuzi ya maisha yako wewe mwenyewe
  12. Panga malengo yako upya mara kwa mara na fanya tathmini ya maisha yako na jipongeze kwa mafanikio yako hata kama ni kidogo
  13. Saidia wengine pale unapoweza na usitarajie shukurani
  14.  Safari mara kwa mara
  15. Ishi ndani ya bajeti yako na maisha ya sasa tu (usiwaze sana yajayo)
  16.  Fata sheria zote za kazi na nchi yako
  17. Jipe mapumziko ya kutosha
  18.  Ishi maisha yenye afya
  19. Tafuta hobi na ujuzi mpya
  20. Jichanganye na watu wenye fikra chanya
  21. Kaa karibu/wasiliana na watu uwapendao mara kwa mara
  22. Beba msalaba wa makosa yanayotokea kwenye maisha yako
Samehe na sahau

Kila mmoja ana tabia zake ambazo huwa tofauti na mwingine, kila mara watu watafanya mambo yanayokukwaza na kukuondolea furaha,

Ukiwa mtu wa kuzingatia makosa madogo madogo kila mara lazima utaumia tu,

  • usichunguze sana mambo hasa kama hayakuhusu moja kwa moja
  • ikiwa mtu atafanya kitu kwa makusudi kukukera usioneshe kama umekwazika wala usijibu na usibadili hisia zako mbele yake baki katika hali ya kawaida na tawala hisia zako za ndani
  • Usilipize kisasi wala kuweka mambo moyoni, baki na funzo achilia na sahau
  • Kama mtu atakukera kwa bahati mbaya, usijibu haraka tafuta muda mwingine na mueleze taratibu ili asirudie
  • Epuka kujibizana na mtu yoyote kwa jambo lolote
  • Acha mambo madogo madogo yapite sio kila jambo baya unapaswa kulioesha au kulizingatia
  • Simamia Majukumu yako ipasavyo ikitokea umekosea rekebisha bila kusukumwa
  • Jifunze kukaa kimya
  • Usibebe kila jambo kama tatizo kubwa, mengine acha kuyapa umakini wako na baki na funzo

Jifunze kusahau haraka mambo yote yenye kumbukumbu za huzuni kama “Vifo ” “usaliti “na maudhi ya kila mara,

Ishi kama hakijatokea kitu na endelea na ratiba za kawaida bila kuona kama kuna shida ilitokea na tawala maisha na akili yako ya ndani

Kuwa na mtazamo Chanya kwenye kila changamoto itakusaidia kupata amani kubwa

Usijilinganishe na wengine

Ni kosa kubwa sana kulinganisha maisha yako na maisha ya watu wengine hata kama wamekuzidi kila kitu

Tambua kuwa maisha yana siri nyingi sana, inawezekana unaejilinganaisha nae na yeye anatamani kuwa kama wewe!

Siku zote kuwa ambae unajilinganisha mwenyewe kupitia jana na leo, mwaka ulioisha na mwaka uliopo na kuhakikisha unajirekebisha na kujiboresha wewe mwenyewe bila kutaza watu wengine

Angalia wapi unatakiwa kujiweka Sawa na wapi kupaongezea juhudi kwa kuangalia matokeo yako ya sasa na yale ya zamani

Usilinganishe kitu chako chochote iwe muonekano,  biashara,  Mali, au familia yako na watu wengine,

Tambua kuwa kila mmoja ana njia zake na  siri zake ambazo huwezi kuzijua kwa macho ya nje

Ishi ndani ya maana ya maisha yako

Maisha hayana maana yoyote! Lazima wewe Ndio uchague maana unayotaka na uyape maisha yako hio maana

Ishi katika maana yako na kila siku zingatia kile unachokiamini wewe, kila mmoja ana maana yake na anaishi maisha yake aliyoyachagua

Ondoa mahusiano mabaya yote

Usikubali kuishi ndani ya maisha ya mtu mwingine kwa kuteseka, tambua kuwa maisha ni mafupi sana hivo unapaswa kufurahia maisha yako wewe mwenyewe!

Iwe mwenza, marafiki, ndugu au mtu yoyote, ikiwa haoneshi kuwa sehemu ya kukupa amani Jitenge nae haraka

Kataa kuwa mtumwa wa mateso ikiwa wenzako wanafurahia unavyoteseka!

Ishi maisha yako na chagua watu wanaokuchagua!

Mfano umeamua kuwa na mahusiano na mtu asiye kupenda, wewe unalazimisha kwasababu unampenda, anakufanyia visa na vituko kila siku unateseka na kuvumilia halafu unakosa furaha na kuona dunia ni mbaya!

Hakuna kitu kinaitwa ndugu wa damu, ikiwa ni ndugu yako au hata mzazi au mtoto wako kama haoneshi na hataki uwe sehemu ya maisha yake basi Acha mara moja na angalia wale wanafurahia kuwa na wewe

Usiamini mtu kupitiliza /usiweke matarajio makubwa kwa mtu na jifunze kuwa na mbadala

Hapa duniani hatua ya kwanza ya kuwa na huzuni ni kuamini watu!

Akili za watu zinabadilika muda wowote, watu hupanga na kupanga malengo na ratiba zao!

“moyo wa mtu ni kichaka” na mioyo ya watu ina siri nyingi sana,

Sasa kama utaamua kuamini mtu kisa amekuaminisha jua umechagua kukosa furaha

Wakati mwingine watu huamua kukutumia kwa sababu zao kupitia uongo wa Ahadi unazopewa!

Hivyo jifunze kutoweka matumaini wala matarajio makubwa kwa mtu yoyote yule hata kama huko nyuma aliwahi kufanya kweli alichokuahidi

Weka mbadala wa Mara kwa mara ili mambo yakienda kombo uwe tayari na kitu kingine cha kukusaidia na kuepuka kukwama

Punguza matumizi yasiyo ya lazima na ishi ndani ya bajeti zako na maisha ya sasa (usiwaze sana maisha yajayo) 

Mara nyingi watu huumizwa kwa kutaka kuishi nje ya uwezo wao na bajeti zao,

Usipende kuwa na tamaa za muda mfupi kisa unataka kwenda na wakati au unataka kufurahisha wengine!

Ishi na bajeti za ndani ya uwezo wako tu, nunua kile unachoweza kukimudu na chenye ulazima katika wakati huo

Jipange kwa ajili ya baadae maana vitu vyote unavyotamani kuwa navyo leo baada ya miaka kadhaa vitakuja bora zaidi ya sasa na hutoona thamani ya vilivyopita

Punguza matumizi ya mitandao ya kijamii, ishi katika mazingira halisi

Watu wengi mitandaoni huishi maisha feki! Na maisha yasiyo ya kweli,

Hao unaowatamani kwa kuwaangalia mitandaoni hata wao wanatamani maisha hayo hayo wanayoyaigiza

Ukweli wao ni mchungu pengine kuliko wewe, hivo kamwe usikubali kuingia mtegoni,

Mtu mwenye furaha ya kweli katika ndoa hana muda wa kuaminisha watu mitandaoni kuwa Ana pendwa sana!

Mwenye mafanikio makubwa ya maisha, hana muda wa kuonesha watu Mali zake mitandaoni

Aliye fanikiwa kuwa na familia bora na maisha yaliyokamilika hana muda wa kuonesha watu hayo yote

Ukiona mtu anaonesha sana mafanikio yake mitandaoni jua  kuna mambo mawili:

1. Ni njia yake ya kuingiza kipato
2. Ana shida na mapungufu ya akili.

Kama hutumii mitandao kibiashara au kujifunza kitu basi Acha matumzi au punguza kabisa maana mitandao ni chanzo kikubwa cha kukosa amani na furaha

Jifunze kuishi katika mazingira halisi ya nje ya mitandao na utaona amani kubwa utakayopata

Jifunze kushukuru

Mara kwa mara shukuru hata kwa uzima wako tu ikiwa huoni mambo mengine mengi ya kukufanya ushukuru

Kumbuka kuna wengine wamelazwa wanapigania uhai wao muda ambao wewe unalia kisa Huna nyumba!

Kuna wengine wanatamani wangepata nafasi ya kusoma hata darasa la saba tu wakati wewe unaona degree yako haina Msaada

Kuna ambao wanatamani kuacha ndoa zao za mateso wakati wewe unalia hujaolewa

Pia kuna wale ambao hata mlo mmoja kwao ni mtihani wakati wewe Huna kazi Ila una mahala pa kula na kulala

Jiamini na jikubali

Ondoa uoga na aibu siku zote jua kuwa una kitu cha ziada ambacho wengine hawana Ndio maana hufanani na yoyote,

Jiamini kwenye kila unachofanya na weka matumaini ya ushindi

Usiogope waliokuzidi na fanya kila unachoweza kufikia malengo yako na hapo utafurahia maisha yako

Fanya maamuzi ya maisha yako wewe mwenyewe

Sio kila mara unapaswa kupangiwa chakufanya

Ukitaka furaha ya kweli basi jisimamie mwenyewe maana maisha ni yako

Simamia mipango yako na fanya maamuzi yako binafsi kwa kuangalia kipi kilichobora kwako

Maamuzi ya kupangiwa huzaa maisha ya huzuni baadae hasa yakitokea makosa au hitilafu

Panga malengo yako upya mara kwa mara na fanya tathmini ya maisha yako na jipongeze kwa mafanikio yako hata kama ni kidogo 

Kila mmoja ana malengo yake katika maisha anayotamani kutimiza

Kuna wakati kama hujatimiza malengo fulani huondoa amani yako na furaha yako hivo kukufanya uwe na huzuni kubwa

Lakini tambua kuwa malengo kutimia au kutotimia hutokana na sababu mbali mbali

Unapaswa kupanga malengo yenye kuendana na uhalisia kisha fanyia kazi kwa juhudi, ikiwa utafanikiwa basi furahia na jipongeze

Ikiwa hujafikia lengo na kabla ya kuhuzunika tafuta sababu na panga upya malengo yako mara kwa mara

Kuna mengine unapaswa kuyaondoa na kuwa hayawezekani au yameisha muda wake, na yapo yakuongezea muda zaidi ili yatimie, na yale yale yanataka juhudi na rasilimali

Saidia wengine pale unapoweza na usitegemee shukurani wala malipo yoyote

Usitoe ziaidi ya ulichonacho na pia usiwe mchoyo kupitiliza! Wala usitoe ambacho huwezi kukisahau

Furaha huja kwa kuona tabasamu la watu wengine, lakini sio kila utakae msaidia atakukumbuka au kukushukuru

Ila kuna ambao watafurahia na  wakifurahi kupitia wewe basi na wewe hujikuta unapata furaha pia

Kusaidia watu sio lazima pesa au Mali bali hata Ushauri mzuri na mawazo mbalimbali

Safari mara kwa mara maeneo ambayo hujawahi kufika

Safari hufanya mtu kupata furaha na kuona fursa zaidi ya mazingira aliyozoea

Ukiwa na tabia ya kwenda sehemu mpya mara kwa mara hata kama ni ndani ya wilaya yako itakufanya kuona maisha mengine ambayo hukuwa umeyajua kabla

Dunia ina mambo mengi sana ya kila aina, ukitembea utajua mengi na kujifunza mengi

Utakutana na watu na tamaduni mpya ambazo zitakupa mtazamo mpya wa maisha na furaha kila mara

Weka mipaka ya maisha yako na heshimu mipaka ya wengine

Mara zote simama na mipaka yako na usikubali watu wavuke mstari uliyojiwekea, fanya wengine waheshimu mipaka yako na wewe pia heshimu mipaka yao

Jifunze kusema hapana

Usikubali mara zote kukubali kitu hata kama Huna uwezo nacho

Angalia bajeti na ratiba zako kabla hujamkubalia mtu

Usiogope kuonekana mbaya, wala Usiogope kusemwa vibaya

Fanya kitu ambacho kimetoka moyoni Ili kuepuka huzuni na majuto

Fata sheria za kazi,na nchi na sehemu zote

Epuka makosa ya lazima, usijifanye mbabe kuwa kuamini msemo huu:

“sheria zimewekwa ili zivunjwe”

Epuka kuingia katika matatizo ya kujitakia

Ishi vizuri fanya kazi zako kwa uadilifu na heshimu sheria za nchi yako au nyingine bila shuruti utapata maisha ya amani sana.

Ishi maisha kwa kuzingatia afya
  • Fanya mazoezi ya kutoa jasho
  • Pumzika mara kwa mara
  • Kula vizuri kwa kufuta mlo kamili
  • Kunywa maji megi
  • Fanya Meditation

Hii itakupa maisha ya amani na furaha sana

Tafuta hobi na ujuzi mpya

Kama huna hobi tafuta na fanya kile unachokipenda mara kwa mara, jifunze mambo mapya kama kuogelea, jifunze lugha mpya kupitia Dualingo nk

Utajisikia unapata ladha mpya ya maisha kila mara maana ukizoea maisha yale yale kuna muda hua yanaboa

Jichanganye na watu wenye mawazo Chanya

Epuka watu wasio shukuru, watu wanaopenda kulalamika kila mara, watu wagomvi, watu wasio jali maumivu ya wengine hawa watakuambukiza nguvu hasi kwenye maisha yako ,

Tafuta watu wenye kufikiria vitu Chanya maishani na weka ukaribu nao watakufanya uone kila jambo linawezekana na utapata furaha sana

Kaa karibu/wasiliana na watu uwapendao mara kwa mara

Kwa njia mbalimbali hata simu au barua pepe

Watembelee walipo na zungumza nao

Inaweza kuwa marafiki zako , mwenza wako, watoto, wazazi au ndugu

Beba msalaba wa makosa yanayotokea kwenye maisha yako 

Usiwe mtu ambae unatafuta makosa na kulaumu watu wengine kwa kilichotokea hata kama kweli wamehusika,

Kila kosa chukulia kuwa wewe Ndio sababu ili ikufanye kutafuta suluhu na kuwa makini mfano,

Imetokea umemkopesha mtu pesa kisha hakurudisha, badala ya kumlaumu yule mtu na kujiumiza, jilaumu wewe na sema kuwa ulitakiwa kuwa makini kumkopesha mtu bila kuchunguza tabia yake

Hitimisho

Maisha ya amani yanawezekana, sio lazima utafute mafanikio kwa kuumiza akili na mwili wako, wala kuumiza wengine,

Badili mtazamo wako sasa! Pia soma mbinu za kusahau Mambo ya nyuma.

Share this article
Shareable URL
Prev Post

Biashara ya wafanyakazi wa majumbani10 Min Read

Next Post

Changamoto za biashara na jinsi ya kukabiliana nazo11 Min Read

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Read next

Huruhusiwi ku copy. Asante.