Utangulizi
Biashara ya kukusanya takataka sio biashara ngeni katika maisha yetu ya kila siku , ni Biashara tunayo ishi nayo sehemu zote
Takataka ni vitu vyote ambavyo havihitajiki tena baada ya matumizi yake ya jumla, vinaweza kuwa mabaki au mahitaji yaliyoisha thamani yake.
Wengi tumezoea kuona wabeba takataka hasa wale wanaofanya kazi hii kama watu wasio sawa sana kiakili
Au hata wanachukuliwa kama watu wenye maisha magumu sana na dhalili mbele ya wengine,
Hii imesababishwa na ukweli kuwa asilimia kubwa ya wabeba takataka wanajihusisha na matumizi ya vilevi vya aina mbali mbali
Pia muonekano wao umefanya asilimia kubwa kuwadharau na hata kudharau kazi hii ya kukusanya takataka.
Na hatimae uchafu umekuwa sehemu ya maisha iliyozoeleka na wakazi wa maeneo mengi nchini Tanzania hususani jiji la Dar es salaam,
Baadhi ya mikoa kama Moshi na Iringa angalau kuna unafuu mkubwa sana wa hali ya uchafuzi wa mazingira kutokana na sheria zao.
KUNA UTAJIRI MKUBWA SANA KATIKA BIASHARA YA UKUSANYAJI WA TAKATAKA KWASABABU BADO SOKO LIPO NA HALINA USHINDANI KABISA.
Hata kampuni zinazofanya biashara hii hazifanyi kwa kiwango kinachopaswa hivyo kupelekea hali ya uchafu kubaki vilevile
Licha ya kutunza mazingira katika hali ya usafi , kuepusha miripuko ya maradhi kama kipindupindu na hata kuongeza mvuto ,
Biashara hii pia ina faida kubwa sana za kiuchumi kwa wenye mitaji mikubwa na wasio na mitaji kabisa.
Unaweza kufanya biashara hii peke yake au ukachanganya na zile za usafi wa nyumba na usafi wa ofisi

Aina Za Takataka
Kuna aina mbali mbali za takataka lakini zimegawanywa katika makundi makuu mawili
- Takataka ngumu kama vile machupa , mifuko nk na
- Takataka laini kama vile kinyesi ,matunda, mboga mboga nk
Katika makundi hayo pia zipo takataka ambazo
- Zinazoweza kutumika tena mfano machupa ya plastiki , kinyesi kwa kutengeza mbolea nk
- Zisizoweza kutumika mfano kemikali za hospitalini.
Takataka Zinatoka Wapi?
Takataka zina sababishwa na vyanzo vya aina nyingi sana kama vile
- Taka za majumbani
- Taka za viwandani
- Taka za hospitali
- Taka za mjini
- Taka za sokoni na sehemu za biashara
- taka za ujenzi
- Taka za shuleni NK
Udhibiti wa Takataka (Biashara Ya Kukusanya Takataka)
Maana yake ni kitendo cha kuweka mazingira safi na salama kwa kuondoa takataka katika maeneo yasiyo hitajika
Hii maana imejumuisha ukusanyaji wa taka, kurudia matumizi na thamani ya taka na kuharibu kabisa takataka.
Nchini Tanzania kuna namna mbili za udhibiti zimezoeleka zaidi kutokana na sababu za kiuchumi kama machupa na vyuma chakavu

Aina Za Udhibiti (utunzaji)Wa Takataka
Kuweza kufanya Biashara ya ukusanyaji wa taka lazima ujue aina ya takataka na udhibiti wake kabla ya kuchukua hatua
Zifuatazo ni aina za Udhibiti wa taka taka
- Kurudia matumizi , hii maana yake kufanya taka kuwa na thamani na kufaa kwa matumizi mengine tena mfano chupa za maji
- Kuweka dampo maana yake kukusanya takataka na kuweka sehemu moja maalumu ambapo hatua zingine za utunzaji hufuata
- Uchomaji moto maana yake taka taka huchomwa kwa lengo la kuondoa uchafu wa ndani yake
- Kutengeneza mboji maana yake taka taka hujivunja katika sehemu ndogo ndogo kupitia bakteria na kuingia ndani ya udongo kama mbolea mfano mboga mboga, majani,matunda nk.
HAPA TUTAZUNGUMZIA AINA MOJA AMBAYO NI KUPELEKA DAMPO.

Biashara Ya Ukusanyaji Takataka Kwa Wasio Na Mitaji
kama huna mtaji wala sapoti ya kukupa mtaji ila una nia na shida ya pesa unaweza kuanza katika mazingira ya kawaida
Anza na aina ya kupeleka dampo kwa sababu haitaki mtaji mkubwa kuanza zaidi ya nguvu na jitihada
Unaweza kufanya mwenyewe au ukafanya na baadhi ya rafiki zako.
Jambo la kuzingatia ni kuweka nia ya dhati bila kusahau malengo makubwa sana ya baadae na usiifanye kazi kimazoea,
Anza na Toroli ambalo unaweza kukodi kwa bei ya wastani wa elfu 1000 mpaka elfu 3000 inategemea na mazingira ulipo
Pita nyumba za jirani ukianza nyumba unayoishi , vyumba vya wapangaji kisha jitangaze hapa lazima uepuke aibu
Hakuna aibu mbele ya njaa, wala malengo na kiu ya mafanikio ikiwa una nia na dhamira ya dhati.
Mara nyingi bei za kuchukua takataka watu hulipa kuanzia elfu moja na kuendelea inategemea wingi wa takataka
Kwa mazingira kama Dar es salaam hasa maeneo ya uswahilini kama Temeke, Tandika Mbagala nk uhakika wa soko ni mkubwa sana
Kwahio kumbuka mwanzo ni mgumu sana na changamoto hazikosekani lakini ukiamua kutoka moyoni unaweza.
Endelea taratibu na kila ukipata pesa nunua vifaa vyako kidogo kidogo huku ukijiboresha siku baada ya siku
Kisha baada ya muda jitoe kama mfanyakazi na anza kusimamia vijana chini yako na ukizidi kupata mafanikio sajili kampuni.
Biashara Ya Ukusanyaji Takataka Kwa Wenye Mitaji
Pia hapa unaweza kuchagua aina ya utunzaji wa taka kulingana na mawazo uliyonayo na mbinu zako za kupata pesa
Mfano kama utataka kukusanya taka kwa gari unapaswa kuwa na vifaa vifuatavyo:
- Gari kubwa la kubebea taka
- Toroli kwa wateja waliopo sehemu ambazo gari haliwezi kufika
- Gloves
- Kipaza sauti
- Sare za wafanyakazi
- Makoleo ya kuchotea takataka NK
Hatua za Kuazisha Biashara Ya Ukusanyaji Takataka
- Sajili kampuni
Lazima usajili uanzie Brela , TRA na kisha leseni ya biashara kwanza ambapo pia utapata mashine za risiti kila unapolipwa pesa na wateja
- Tafuta vibali
Ili kufanya biashara hii kwa usalama lazima kupata kibali kutoka NEMC Yaani Baraza la Taifa ya utunzaji na usimamizi wa mazingira
- Kodi Ofisi
Hapa sasa utachagua ofisi karibu na eneo rahisi kufika ndani ya halmashari husika na kuweka thamani zote unazotaka
- Sajili wafanyakazi
Ili kupata wafanyakazi wazuri zingatia uimara wa afya zao na uzoefu wa kazi hii kutoka kampuni zingine
- Nunua vifaa
Zingatia ubora wa vifaa kuanzia gari na vitu vingine vyote kupunguza hasara za awali
- Jitangaze
Hapa hakikisha kwanza wanachi wanapata taarifa za kampuni yako kupitia ushirikano wa ofisi za kata na serikali za mitaa ili kurahisha uaminifu na malipo
Changamoto Za Biashara Ya Ukusanyaji Takataka Na Suluhisho
- Ugumu na usumbufu wa malipo hasa kutoka kwa wananchi , kuweza kuweka sawa hili shirikiana na ofisi za kata na halmashauri
- Uelewa mdogo wa wananchi juu ya athari za takataka na madhara yake , kwahio lazima mara kwa mara Elimu itolewe kwa watu ili kuwahamasisha katika suala la usafi wa mazingira yao
- Ubovu wa miundo mbinu hasa barabara na nyumba zilizo katika mpangalio usio sahihi unapelekea baadhi ya maeneo kuwa na ugumu wa kufikika.

Hitimisho Na Wito Kwa Serikali Juu ya Utunzaji Wa Mazingira
Tumeona athari nyingi sana mara kwa mara juu ya mlipuko wa maradhi yanayotokana na Uchafu wa mazingira kupindukia
Athari ni nyingi sana na wanao teseka ni wananchi hasa wenye vipato vya chini sana,
Serikali na uongozi wote kwa ujumla lazima uchukue jitihada za lazima kunusuru maisha ya wananchi kupitia uchafu uliokithiri
BILA KUSAHAU TANZANIA NI NCHI INAYOFANYA VIZURI SANA KATIKA SEKTA YA UTALII
LAKINI UCHAFU WA MAZINGIRA HASA NDANI YA MKOA WA DAR ES SALAAM NI KERO KUBWA SANA KWA WATALII
HII INALETA SIFA MBAYA NA KUPUNGUZA LADHA YA TANZANIA KAMA KIVUTIO KIKUBWA KWA WAGENI NA WATALII
Hivyo basi kuweka mazingira katika hali ya usafi SERIKALI LAZIMA IINGILIE KATI kwa kufanya mambo yafutayao:
- Kuboresha miundo mbinu kuanzia mifereji ya maji machafu mpaka barabara za ndani ya mitaa
- Kusimamia kwa umakini sekta ya ujenzi na kuzuia ujenzi holela
- Kuweka sera sahihi ya kuhimiza kwa lazima wanachi kulipa pesa za ushuru wa utunzaji wa mazingira
- Kutoa sapoti na urahisi kwa wafanya biashara wa sekta binafsi katika ukusanyaji taka
- Kutoa elimu ya mara kwa mara kwa wananchi juu ya madhara ya uchafu na namna ya kuweka mazingira safi
- Kuweka sheria kali sana kwa kila atakae onekana anachafua mazingiraa kwa makusudi
- Kugawa vifaa vya kutunzia takataka kila mtaa ( Ndoo kubwa za takataka) na kuhimiza wananchi kutotupa taka ovyo
- Kutenga maeneo mengi ya kutupia taka ( dampo) mbali na makazi ya wananchi
- Kuangalia namna ya kuleta fursa jinsi ya kubadili takataka kuwa pesa kupitia Teknolojia mbali mbali.