You Can Win If You Want

Wazo La Biashara Ya Kulea Wazee Na Watu Wazima

wazo la biashara ya kulea wazee

Utangulizi

Kulea wazee ni moja kati ya kazi nzuri sana ambayo kwa nchi za wenzetu zilizoendelea ni kazi yenye Kuheshimika na malipo mazuri sana

Wazee ni watu wenye umri kuanzia miaka 65 na kuendelea ,wazee hawa wanaweza kuwa wanojiweza au wasio jiweza.

Nchini Tanzania bado soko la kutunza na kulea wazee lipo wazi sana na halina ushindani kabisa licha ya kuwa na vituo kadhaa vya kutunza wazee

Hivyo urahisi wa kupata wateja ni mkubwa sana kama utajua hasa namna ya kuteka soko na kuleta huduma bora na nzuri

Kuna wazee wengi wanapata changamoto za malezi kutokana na ndugu au familia zao kuwa bize na majukumu ya kiutafutaji

Lakini pia Familia nyingi zinapata shida ya kutunza wazee wao kwa sababu za mihangaiko na majukumu ya kimaisha

Sio kwamba hawapendi wazee au wazazi wao bali uhalisia unakinzana na ukweli wa kuwahudumia mara kwa mara.

Hivyo basi watu wengi hutamani kupata wasaidizi wa uhakika wa kuwatunza na kuhudumia wazee wao kwa asilimia zote

Hapa nazungumzia huduma sahihi na salama kama ambavyo wangewahudumia wao endapo wangepata nafasi.

Biashara hii inaweza isiwe tofauti sana na biashara ya wafanyakazi wa kazi za ndani japo kuwa haziingiliani sana

Hii imelenga zaidi kuhudumia wazee pekee kulingana na mahitaj yao ya mara kwa mara.

Biashara ya kutunza wazee
Photo by Kampus Production on Pexels.com

Aina Za Wazee

  1. Wazee wanao jiweza, yaani hawa angalau hujifanyia baadhi ya huduma wao wenyewe mfano kwenda msalani nk
  2. Wazee wasio jiweza hawa huhitaji msaada wa huduma zote za kibinaadamu na wengi huwa wamechoka kwa umri mkubwa au maradhi ya uzeeni.

Mahitaji Ya Wazee

  • Maandilizi ya chakula chenye mlo kamili na sahihi
  • Usafi wa mwili na nguo
  • Kufanyishwa mazoezi ya viungo
  • Kupewa dawa na maangalizi ya afya kwa vipimo vya mara kwa mara
  • Huduma za usafiri na kusindikizwa mahala wanapotaka kwenda
  • Kupata kampani ya maongezi na kuondolewa upweke
  • Kusaidiwa msaada wa kwenda msalani kila wanapohitaji kwa wale wasiojiweza
  • Ulinzi na usalama wao mara kwa mara NK.

Aina Za Huduma Za Biashara Ya Kulea Wazee

Kuna aina mbali mbali za huduma ambazo zimegawanywa kulingana na mahitaji ya huduma za wazee na wateja kama ifuatavyo:

  • Huduma ya Ndani ya nyumba ya mteja , hapa maana yake ni kwenda kuishi na kumuhudumia mzee ndani ya nyumba yake kulingana na makubaliano yenu au familia yake kwa usaidizi wa karibu zaidi
  • Huduma ya Kutwa, maana yake ni kuhudumia wazee kwa muda wa masaa kadhaa mtakayo kubaliana inaweza kuwa asubuhi mpaka jioni au masaa machache tu kwa kila siku au siku kadhaa
  • Huduma ya Nje au Kituoni, maana yake ni kutoa huduma kwa wazee nje ya nyumba zao yaani kumiliki kituo cha kutunza na kulea wazee.

Makundi Ya Huduma Za Kulea Wazee

  • Huduma za kitabibu ambazo huhitaji zaidi watu wenye maarifa na taaluma za uangalizi wa kiafya kama manesi
  • Huduma za kawaida hazihitaji taaluma wala ujuzi mkubwa wa afya zaidi ya uzoefu na upendo kwa wazee.
Kulea wazee na watu wazima
Photo by Kampus Production on Pexels.com

Sifa Za Wahudumu Wa Kulea Wazee

Kulea wazee sio tu kazi au biashara kwa lengo la kupata pesa ni lazima uwe na sifa mbali mbali ukiondoa sifa ya uuguzi:

  • Upendo wa hali ya juu na mapenzi ya dhati kwa wazee
  • Kuelewa namna ya kutoa huduma ya kwanza
  • Heshima ya kiwango cha juu sana
  • Huruma kubwa na moyo wa imani
  • Upole na utulivu
  • Uvumilivu na subra ya hali ya juu mno
  • Usafi
  • Mawazo na tabia chanya
  • Moyo wa kujali na kuthamini
  • Utatuzi wa matatizo kwa haraka
  • Nguvu na afya njema
  • Uaminifu
  • Uelewa wa mila, miiko na tamaduni NK

Namna Ya Kuanza Biashara Ya Kulea Wazee Kwa Wasio Na Mitaji

  • Weka nia na dhamira ya dhati kwa kujiuliza nje ya kutaka pesa una mapenzi ya kazi ya kulea wazee?
  • Fanya uchunguzi wa watu wenye shida na huduma hii ukianzia mtaani kwako lakini zingatia wenye vipato na uwezo wa kulipia
  • Andaa mpango wa biashara ,ili uwe na dira ya biashara na ujue gharama utakazohitaji baadae
  • Buni jina la biashara yako unalotaka, kama una simu janja fungua akaunti za mitandao ya kijamii na tengeneza ukurasa wa biashara
  • Pia kama una ujuzi wa graphic tengeneza na logo kabisa bila kusahau baadhi ya matangazo na kama huna sio lazima
  • Tafuta wateja kwa kuanza na watu wa karibu wenye uwezo wa kulipia lakini fanya aina ya kwenda kutolea huduma kwenye nyumba ya mteja hasa ya kwenda kwa masaa machache
  • Ukipata mteja kubaliana nae bei rafiki kwakua ndio kwanza unaanza na huna vifaa, ujuzi wala uzoefu ,mnaweza kulipana kwa siku,wiki hata mwezi
  • Anza kazi kwa mapenzi na jitume kwa moyo wako wote mpaka wafurahie huduma yako kwa dhati kabisa
  • Endelea kujitangaza, ukipata mteja mwingine tafuta rafiki mshirikishe kisha aende kwa mteja mpya na wewe endelea na mteja wa zamani
  • Wakati unatafuta wateja pia tafuta wafanyakazi,namna ya kunufaika ni kuomba pesa za gharama ya awali ya huduma kutoka kwa wateja na makato kidogo kwenye mishahara ya wafanyakazi
  • Endelea hivo hivo kwa muda huku unaanza taratibu usajili wa biashara na ununuzi wa vitu ambavyo unataka kwa kuanza na vile vya umuhimu kwanza kama usajili, sare NK
  • Ukiona unataka kujitoa kama mfanyakazi na kubaki kiongozi jitoe huku unasimamia walio chini yako mpaka pale utakapoona unaweza kuifikisha biashara katika kiwango kingine
  • Zingatia sio lazima uanze kuwa mfanyakazi hata kama huna mtaji ,unaweza kuanza kwa kutafuta wafanyakazi na kuwaweka wafanye kazi chiniyako.

Biashara hii pia haina tofauti sana na ile ya wafanyakazi wa kazi za nyumbani japo pia haiingiliani sana.

Biashara Ya Kulea Wazee Kwa Wenye Mitaji

  1. Fanya uchunguzi wa soko

    Angalia wateja ,ushindani na hata udadisi wa uwezo wa kifedha na utayari wa wateja kupata huduma yako

  2. Andaa mpango wa biashara

    Zingatia aina ya muundo unaotaka, mtaji ulionao, gharama za uendeshaji makadirio ya mapato na mambo mengine

  3. Sajili biashara yako

    Isajili biashara kama kampuni anza Brela ,TRAna kisha tafuta leseni na vibali vyote vinavyo husika

  4. Andaa eneo na ofisi

    Kama utataka uwe na kituo cha kulea wazee au uwe na ofisi pekee kisha uanze kutoa huduma kwa kumfuata mteja alipo

  5. Nunua vifaa

    Fanya maandilizi ya ununuzi wa vifaa unavyotaka kuanzia vifaa vya ofisi,kituoni na hata vifaa vya kazi

  6. Sajili wafanyakazi

    Zingatia sifa sahihi kuanzia kiwango cha elimu, udhamini na historia zao za nyuma

  7. Andaa matangazo

    Zingatia chapa kuanzia mwanzo na tumia mbinu za ushawishi hasa kulenga watu wenye uwezo mkubwa wa kulipia huduma usisahau website au application kwa ajili ya wateja wa mbali japo sio lazima

  8. Jiboreshe kila siku

    Kila mara boresha huduma ya biashara yako kwa kuzingatia matakwa ya wateja na simamia kwa moyo wote.

Hitimisho

Mbali na faida ya biashara hii pia ina changamoto nyingi sana ukizingatia kufanya kazi na wazee au watu wazima ni jambo kubwa,

Inahitaji moyo na subra kubwa mno kwasababu wengi wao wanapata shida ya msongo wa mawazo, hasira ,kupoteza kumbukumbu na mengine mengi

Kuna ndugu ambao hutelekeza wazee wao hasa katika vituo vya kulelea au hata kutotembelea wazee wao kwa muda mrefu

Kwahio licha ya ugumu na uzito wa kazi lazima uwe na moyo wa upendo na staha za hali ya juu sana

Kuanzia ngazi ya uongozi mpaka wafanyakazi wote.

Share this article
Shareable URL
Prev Post

Jinsi Ya kukuza Mtaji Wa Biashara

Next Post

Wazo La Biashara Ya Udobi ( Dry cleaning and laundry)

Acha Comment Yako

Read next

Huruhusiwi ku copy. Asante.