You Can Win If You Want

Wazo La Biashara Ya Viazi Na Mihogo Ya Kukaanga

Biashara ya mihogo na viazi vya kukaanga

Utangulizi

Mihogo ya kukaanga sio chakula kigeni katika maisha yetu ya kila siku kuanzia sehemu za mjini mpaka vijijni

Lakini pia mihogo ni moja kati ya chakula asili sana na kinacho patikana kwa wingi nchini Tanzania

Bila kusahau mihogo ni chakula rahisi kupatikana na kinachopendwa sana na wakazi wa nchi ya Tanzania.

Mihogo imetofautiana katika aina za matumizi na upishi kwa maana kila mmoja hutumia kwa namna yake inayomfaa zaidi.

Vilevile viazi kama ilivyo mihogo ni miongoni mwa chakula kinachopendwa sana ,cha asili na kinaliwa sana nchini Tanzania

Viazi na mihogo vimetofautiana kidogo sana lakini matumizi yake na hata aina ya upishi vimeshabihiana kwa kiwango kikubwa.

Watu hupendelea kula mihogo au viazi vya kukaanga wakati wa asubuhi kama kifungua kinywa na jioni kama mlo wa usiku

Japokuwa wapo wanaupendelea kula wakati wowote hususani sehemu za mitaa iliyochangamka sana .

biashara ya mihogo ya kukaanga
Photo by micka randrianjafisolo on Pexels.com

Mahitaji Ya Msingi Ya Kuanzisha Biashara Ya Mihogo Na Viazi Vya Kukaanga

Hapa kuna orodha ya vitu muhimu lakini vinaweza kuongezeka au kupungua kulingana na aina ya uendeshaji unayotaka

Pia inaweza kutofautiana kulingana na uhitaji wa wateja bila kusahau hadhi ya eneo na kipato cha wateja husika

Bila kusahau gharama za manunuzi ya vifaa hivi zimetofautiana kati ya eneo moja na eneo jingine hivyo sitoweka gharama RASMI

  • Karai la kukaangia
  • kijiko kikubwa cha kukaangia na kuepulia mihogo
  • Sahani au mabakuli
  • Vifungashio kwa wateja wanaobeba
  • Beseni au ndoo
  • Kisu
  • Jiko
  • Kabati la kioo au ndoo inayo onesha ndani yenye mfuniko
  • Viti angalau vitatu au benchi
  • Meza japo sio lazima
  • Eneo la kuuzia mfano nje ya nyumba, kibanda na hata fremu
  • mihogo au viazi
  • Mafuta
  • Viungo vya kachumbali
  • Pilipili NK

Mahitaji Mengine Ya Ziada ( Sio lazima kwa anaeanza)

Unaweza kuongeza thamani ya biashara hii ya kuuza mihogo ya kukaanga kwa kuchanganya kuku, nyama,samaki au mishikaki

Inategemea na mazingira bila kusahau mahitaji ya wateja wako na uwezo wa kipato chao

  • Jiko la kuchomea kuku, mishikaki au samaki
  • Samaki
  • Kuku
  • Mishikaki
  • Mayai
  • Friji ( jokofu) NK

Pia unaweza kuuza mihogo na vinywaji laini kama juice au soda na hata chai au kitu kingine chohote wanachopenda wateja wako.

Biashara Ya Mihogo kwa Wenye Mitaji Kidogo

Kama huna mtaji au una mtaji kidogo sana usijali kwa sababu inawezekana kuanza bila mtaji au kuanza na ulichonacho

Baadhi ya vitu sio lazima kabisa kuanza navyo unaweza kununua kidogo kidogo baadae kulingana na uhitaji

Gharama za kununua vitu hutegemea eneo husika na uhitaji wa muanzaji lakini kima cha chini kwa vitu vya msingi angalau 30000

Kwa maana kuwa eneo sio lazima unaweza kuanza biashara hata nyumbani nje au mbele ya mlango hasa kwa maeneo ya uswahilini

Jiko na karai na hata vyombo pia unaweza kuanza na vile vya kila siku unavyotumia nyumbani unapoishi.

Hivyo basi mahitaji ya lazima ni mihogo au viazi, mafuta na viungo ambavyo kwa mwanzo hupaswi kuanza kuuza kiasi kikubwa

Bei huanza angalau shilingi mia moja kwa kipande cha muhogo au kiazi na huongezeka kulingana na aina ya wateja na eneo unaolouzia,

Lakini pia sio lazima kuanza kuuza mihogo na kuku wala samaki, unaweza kuuza mihogo peke yake na ukapata wateja wengi.

mihogo ya kukaaanga
Photo by Nano Erdozain on Pexels.com

Wateja Wa Biashara Ya Mihogo Na Viazi Vya Kukaanga

Mihogo na viazi vya kukaanga hutumika kama kitafunwa cha asubuhi kwa asilimia kubwa ya watu waishio sehemu za mjini

Na wale wa vijijini hupendelea zaidi mihogo na viazi vya kuchemsha, hivyo basi soko kubwa la biashara hii lipo maeneo ya mjini kama :

  • Mashuleni (Watoto na wanafunzi wa shule)
  • Wanafunzi wa vyuo
  • Mtaani hasa kina mama
  • Boda boda na madereva bajaji
  • Wafanyakazi wa ofisi mbali mbali
  • Kina dada wasio na familia
  • Vijana ambao hawajaoa NK

Mihogo au viazi huaminika kama chakula cha haraka zaidi, cha bei ndogo na chenye kushibisha.

Mambo Ya Kuzingatia Kwenye Biashara Ya Mihogo Ya Kukaanga

  • Mihogo laini na yenye unga kwa ndani
  • Kachumbali nzuri yenye ladha ya ndimu au limao
  • Pilipili ya kupika nyenye harufu nzuri
  • Usafi wa hali ya juu sana
  • Maji ya kunywa ya bure (huongeza thamani ya biashara kwa wateja)

Hitimisho

Biashara ya mihogo au viazi licha ya urahisi wake kupatikana kuna misimu ambayo hutoweka sokoni na misimu ambayo hupatikana zaidi

Mihogo ikiwa mingi hata wafanyabiashara wakaangaji mitaani huongezeka kwa wingi sana hivyo kupelekea ushindani mkubwa

Mihogo ikiisha msimu wake hata wauzaji na wakaangaji hupungua hivyo kufanya soko kuwa kubwa zaidi mitaani

Vile vile bei ya mafuta hupanda au kushuka na kupelekea changamoto kwa wakaangaji wa mitaani.

Hivyo basi unapaswa kujiandaa kwa vipindi vyote bila kusahau changamoto za kawaida za biashara yoyote.

Kupata mchanganuo kamili wa biashara hii kulingana na mtaji ulionao bila kusahau mazingira uliyopo bonyeza link hii.

Share this article
Shareable URL
Prev Post

Mbinu Za Kuongeza Mauzo Ya Biashara

Next Post

Wazo La Biashara Ya Juice Ya Matunda

Read next

Huruhusiwi ku copy. Asante.