You Can Win If You Want

Namna Sahihi Ya Kupanga Bajeti Ya Matumizi14 Min Read

Namna rahisi ya kupanga bajeti binafsi

Utangulizi

Kupanga bajeti binafsi ni jambo muhimu na lenye ulazima kwa mtu yoyote anaetaka kupiga hatua au kutunza mafanikio aliyo nayo

Watu wengi sana hupata changamoto kubwa kwenye suala zima la upangaji wa bajeti zao kwenye kipato wanachopata

Kuna wale waajiriwa ambao bila kujali ukubwa wa mishahara yao bado huwa na changamoto ya kuishiwa pesa kabla ya mwezi kuisha

Yaani suala la mishahara yao kukutana ni hadithi nzito sana na mara nyingi wiki ya mwisho wa mwezi huwa ngumu sana kwao

Licha ya waajiriwa ,pia kuna kundi la watu wengi sana hata waliojiajiri wanapata changamoto sana kwenye masuala ya bajeti zao

Bila kusahau wale wenye maisha ya kuunga unga na wasio na ajira yoyote kabisa ambao hutegemea misaada

Au hutegemea kipato kwa njia zao wao wenyewe kama madili ya hapa na pale na vibarua, pia wana changamoto za kupanga bajeti zao.

Wakazi Hawana Uhakika Wa kesho Yao

Kwa ufupi Tanzania ni moja kati ya nchi ambayo asilimia kubwa ya wakazi wake huishi maisha yasio na uhakika

Wengi wao wameshazoea kulia shida na matatizo ya kuishiwa fedha mara kwa mara kama sehemu ya maisha yao

Ajabu ni kuwa hata baadhi ya wanaolipwa pesa nyingi bado hukumbwa na changamoto za kuishiwa pesa kabla ya mwezi

Ni kama vile tatizo la pesa ni sehemu ya kanuni na misingi ya wakazi wa Tanzania pengine hata Africa kwa ujumla!

Sio kwa sababu ya hali ngumu ya maisha pekee bali pia tatizo la ukosefu wa Elimu ya fedha na kujitegemea

Elimu hii haikupaswa kufundishwa shuleni pekee bali hata kwa wazazi enzi na enzi kwa njia ya vitendo

Maana yake ni kuwa maisha ambayo tunaishi ni mazoea tuliyopata toka kwa wazee wetu na jamii inayo tuzunguka

Wakazi wengi wanaona kawaida kuishi chini ya kipato cha dola moja kwa siku.

kupanga bajeti
Photo by Photo By: Kaboompics.com on Pexels.com

Ugumu Wa Maisha Na Shida Ndio Kauli mbiu Ya Nchi

Neno ugumu wa maisha sio tu limebeba uhalisia wa maisha ya Watanzania bali ni kama neno lililozoeleka,

kila mmoja anahisi raha kulitamka! na ndio kama Kauli mbinu ya wananchi na wakazi wa Tanzania

Ni kosa kubwa kumwambia mtanzania mwenzako kuwa sasa umefanikiwa ,hapo unaweza hata kuchukiwa kabisa

Ndio maana mpaka leo mtu anaejitapa kafanikiwa na hana shida tena huonekana anajidai au ana dharau kwa wengine

Ila yule anae lia shida hupewa umakini wa kuonewa huruma za kinafki na kuonekana kama muhanga wa Serikali!

Hayo ndio mambo yanayo pelekea kukithiri kwa hali duni ya maisha na watu kuona kama vile ni haki yao ya msingi kuteseka

Ndio maana wengi hawafanyi jitihada za lazima kujikomboa wala kufikiria kupiga hatua kubwa za maisha

Mtu akipata kitanda cha tano kwa sita, redio kubwa, Tv na sofa la watu wawili hapo huna kitu cha kumwambia

Akijitahidi sana ataongeza makabati mawili la vyombo na nguo bila kusahau mtungi mdogo wa jiko la gesi

Kinachobaki ni starehe , kubadili wanawake na mavazi ya aina mbali mbali na huona kamaliza kila kitu na ana haki ya kutulia

Lakini pia ndio imefanya wengi kutumia pesa za ziada kwa fujo kwa sababu ya kutoogopa umasikini kabisa.

Umasikini Ni Kama Nembo Ya Taifa

Kwa watu wengi uoga wa umasikini na kuishiwa pesa sio jambo kubwa wala halina mashiko kwao

Wao hata wakipata pesa za ziada huhisi kama watalaanika hivyo hutafuta namna ya kuzitumia kwa fujo

Roho huacha kwenda kasi pale anapobaki na kiwango kile kile alichozoea kukimiliki na hapo ndio akili hukaa sawa

Kwa maongezi unaweza kuhisi kila mtanzania anachukia sana umasikini wake lakini kwa vitendo ni kama wote wanafurahia.

Hivyo basi kuondoa umasikini nchini Tanzania sio tu suala la kufanya maendeleo ya miundo mbinu pekee

Bali mapinduzi ya fikra za enzi na enzi ikiwa pamoja na watu kupewa nembo mpya ndani ya akili zao kuhusu mafanikio

Leo hii mataifa yaliyo endelea zaidi kama Marekani hata wakija kuishi Tanzania na sisi kupewa Marekani,

Ndani ya mwaka tu tutatamani tena kuja Tanzania kwasababu tutaona mafanikio upya na Marekani tuliyopewa itachakaa!

Shida ipo ndani ya akili na mazoea ya enzi na enzi wala sio uhaba wa rasilimali zilizopo.

Ukitakaga kugombana na mtanzania mfundishe kuhusu mafanikio na Elimu ya pesa anaweza hata kukupiga

Ila kwenye umbea na masuala ya ushabiki usio na tija hapo atakupa hata ofa ya kinywaji umsimulie vema.

mbinu rahisi za kupanga bajeti
Photo by Tima Miroshnichenko on Pexels.com

Kupanga Bajeti Ni Zaidi Ya Kipato

Haijalishi ukubwa wa kipato anachopata mtu au udogo wa kipato chake suala la bajeti ni zaidi ya hayo

Kuna watu wana kipato kidogo sana lakini wana majukumu mengi makubwa mno na bado wanaweza kuyamudu

Na wapo wenye kipato kikubwa zaidi ila miaka nenda rudi hakuna walichofanya zaidi ya wingi wa nguo kabatini

Kwahio haijalishi mtu anapata kiasi gani, shida sio anachopata bali anachobakisha au anavyoweza kumudu maisha

Vile vile wengi huchanganya kati ya kuweka akiba na bajeti, wakidhani kuwa akiba ndio mafanikio ya bajeti

Kwamba akiwa na uwezo wa kutunza pesa basi mwendo ameumaliza!

Anasahau kuwa kuweka akiba haina tija yoyote kama pesa haizalishi kitu, ni bora ukose akiba ila uwe na mzunguko wa pesa.

Hivyo basi suala la kuweka akiba na kipato sio tija ya kupata mafanikio bali akili na matumizi sahihi ya pesa.

Sababu Kubwa Za Watu Kuteseka Kwenye Bajeti

Mazoea Ya Kuanza Ujenzi

Mazoea na imani mbovu , mfano suala la kujenga nyumba ya kuishi kwanza yaani mtanzania hato jiona amefanikiwa kama hana nyumba

Hata kama ni nyumba ya kuunga unga, Mtu anaogopa kulipa kodi kuliko anavyoogopa kulala na njaa!

Kuliko aanze uwekezaji wa mzunguko wa kipato kinachojizalisha baada ya kuajiriwa au kupata pesa za pamoja

Huona bora kuanza ujenzi wa nyumba ya kuishi hata kama kwa kuunga unga kisa kodi ya elfu 30000 kwa mwezi anayolipia

Haya ni mazoea na uoga ambao jamii imejiwekea miaka na miaka kwenye vichwa vya watu wengi

Yule anaeanza kufanya maisha nje ya ujenzi baada ya kupata pesa huonekana hana akili nzuri za maisha

Cha ajabu hata vibarua na wenye maisha ya shida nao wanapambana kuanza ujenzi kwanza badala ya kukuza kipato.

Hali hii ni janga kubwa sana la Taifa kwa ujumla , wengi wana uwezo wa kukuza vipato vyao ila imani na mazoea vimewaharibu

Hivyo kutoa watu katika imani kama hizi ni suala lingine na kuwapa maendeleo pia ni jambo lingine.

Kumbuka kama ujenzi wa nyumba sio kwa lengo la kuingiza pesa kupitia hiyo nyumba huko ni kuzika pesa!

Watu wengi huzika pesa zao bila wao kujua na kujipa hofu zisizo na msingi mkubwa sana kwenye maisha yao

Kisa ni uoga wa maisha.

Mazoea Ya Chakula Cha Rejareja

Mazoea mengine ya ajabu ni watu kuona kama laana kununua chakula cha jumla na kuweka ndani

Hata wale wenye maisha yenye unafuu bado huona fahari kila siku kwenda dukani kwa mangi kununua kwa reja reja

Chakula ni kitu cha msingi na lazima kwa kila mtu na ndio hupaswa kupewa kipaombele cha kwanza

Ila mtanzania kuweka chakula ndani cha jumla kwake ni kama anasa au laana kubwa sana kwa nembo ya Taifa.

Vyakula vikinunuliwa kwa jumla huleta utulivu wa akili na uhakika wa kuishi kwa muda bila hofu ya kula

Nchi za watu walio endelea huwa na utaratibu wa kuweka chakula ndani kwanza kabla ya matumizi mengine

Ila tanzania hata wale wanao nunua vyakula kwa jumla huonekana kama wana leta ufahari sana au wana maisha mzuri sana

Na huo huwa mwanzo wa Ndugu kujaa ndani ya nyumba kisa kuna viloba vya unga na mchele ndani,

Kumbe chakukula cha jumla kina unafuu mkubwa sana hata wa bei ya ununuzi na pesa huweza kuwa na bajeti nzuri.

Njaa Haina Adabu ,Kipe Chakula Umuhimu Wa Kwanza

Njaa sio kitu cha kuchezea kabisa maana ndio chanzo cha mabaya na maovu mengi sana Duniani

Kila mtu hufanya kila jambo kujaza tumbo lake na matumbo ya wanao mzunguka kwanza

Hivyo chakula hupaswa kuwa kitu cha kwanza kabla ya mambo yote hata kama yana umuhimu mkubwa zaidi

Wengi hulazimika kufanya mambo ya ajabu hata kushusha utu wao kisa njaa hususani kina dada

Mapenzi yamekosa ladha na mvuto na kila mtu kuonekana yupo kimaslahi kisa kikubwa ni njaa inayotesa watu

Kama mtu akishiba huwa na utulivu mkubwa sana na hata uwezo mkubwa kufikiri huongezeka kwa wingi

Changamoto ni kuwa licha ya umuhimu wa kula bado wengi hukipa chakula nafasi ya mwisho kwenye bajeti zao

Kina dada wakipata pesa hukimbilia kununua mawigi na nguo nzuri huku wakaka wakihonga na kunywa bia

Wanakijiji wakivuna mazao huona anasa kukaa hata na debe kadhaa za mazao yao na huamua kuuza yote

Hili ni suala linalo sikitisha sana ,kama tukibadili mtazamo wa chakula asilimia kubwa ya maovu yatapungua sana.

Mendeleo yataibuka na hata kiwango cha ubunifu na fikra kitaongezeka.

Sababu Zingine Za Watu Kuteseka Kwenye Bajeti Zao

  • Anasa na starehe za muda mfupi hasa wanaopenda matumizi ya vilevi na ngono za hapa na pale
  • Ulimbukeni , hususani kwa wale waliopata pesa ukubwani na waliotoka familia za vipato vya chini zaidi
  • Makundi ya marafiki wanao waza maisha ya muda mfupi bila uwekezaji na malengo ya kudumu
  • Tamaa hasa kwa vitu vya kujionesha na visivyo na tija kwenye maisha kama kwenda na fasheni
  • Ndugu na wategemezi hapa zaidi ni wale ambao hufanikiwa wa kwanza kwenye familia zao na hupaswa kubeba majukumu ya wadogo na wazazi
  • Kujionesha na kutaka kufurahisha watu hapa ni wale ambao huishi kisa macho ya watu na kutaka sifa zisizo na msingi
  • Ukosefu wa malengo na dira ya muda mrefu ya maisha
  • Kuiga na kutaka kufanana na wengine
  • Kujikweza , kuna wale ambao huingia gharama kisa kutaka kuonekana amejipata na hakubali kujishusha NK

NB; Bajeti ya anaeanza kujitafuta na aliye kwisha kujipata haziwezi kufanana kamwe.

hatua za kupaga bajeti
Photo by RDNE Stock project on Pexels.com

Hatua Za Kupanga Bajeti Kwa Waajiriwa Na Wenye Kipato Cha Uhakika

Kundi hili ni rahisi sana kwa sababu wana uhakika wa kipato chao cha mwezi au wiki na hata kila siku

Hivyo ni rahisi sana kujua mapato na matumizi yao ya kila siku au mara kwa mara na hata kuweza kupanga bajeti zao

  1. Elewa kipato chako kamili

    Hapa weka kile kipato cha uhakika sio pesa za madili ambazo hazina uhakika wa kupatikana

  2. Orodhesha matumizi yako yote

    Yawe makubwa au madogo ,yanapaswa kujulikana kwa uwazi hata yale ya lazima na yale ya mara moja moja

  3. Anza na mahitaji ya msingi

    Hapa zaidi ni chakula ,kodi (kwa waliopanga), ada za watoto ,usafiri na bili za maisha ya kila siku zipigie hesabu yake kamili

  4. Ingia matumizi ya ziada

    Kama mavazi (sio kitu cha kila mwezi au cha lazima zaidi) misaada ,sadaka starehe nk

  5. Andaa mpangilio wa mwezi na mwaka mzima

    Ili kuweza kuweka sawa bajeti ni vema ikae kwenye mfumo wa mwaka na mwezi kwa maana kuwa matumizi mengine hayawezi kuwa ndani ya kila mwezi

  6. Hesabu jumla ya kipato chako kwa mwezi na mwaka mzima

    Kwasababu ya uhakika wa kipato, huwa rahisi kujua ndani ya mwaka unapata kiasi gani jumla na mwezi kiasi gani

  7. Toa matumizi yote ya mwaka na mwezi

    Usiache kitu chochote kile iwe kidogo au kikubwa katika hatua hii ili kupata hesabu kamili za mwezi na mwaka

  8. Angalia kiasi kinachobaki

    Na hiko kielekeze kwenye dharura na uwekezaji wa pembeni hasa ule wa kuzalisha kipato zaidi kwa maana kuwa kama pesa haibaki au inabaki ndogo RUDIA NA RAHISISHA ZAIDI MATUMIZI YAKO

    Usianze Kuweka Akiba Kabla Ya Matumizi Ili Kupanga Bajeti Nzuri

    Haifai kabisa kuanza kuweka akiba kabla ya kutoa matumizi kwa sababu matumizi ni muhimu na lazima kwenye kuishi

    Akiba huja baadae na huwa pesa ambayo haiombewi baya litokee ila kuishi na kula ni lazima kwa namna yoyote

    Wengi huchemka kutaka kutunza pesa ndani na kusahau maisha yao ya kila siku kwanza au furaha zao

    Ndio maana unakuta mtu anafanya kazi nzuri ila kafubaa hata muoneano wakati huohuo benki kajaza pesa kibao

    Haifai kutumia pesa vibaya lakini pia sio sahihi kabisa kutunza pesa huku unateseka kila siku kisa kesho yako ambayo huna uhakika nayo

    Ishi vizuri kwa misingi sahihi lakini kamwe usiteseke kisha kufa na kuacha wengine kutumia jasho lako .

    KUMBUKA: Matumizi ya uwekezaji na pesa za akiba ni chaguo lako mwenyewe kuweka kila mwezi au baada ya miezi kadhaa

    Jambo la kuzingatia ni kutotoka nje ya bajeti yako uliyo andaa hata kama mchakato utakuwa tofauti.

    Pia kumbuka ukitafuta maisha usisahau kuishi

    kupanga bajeti
    Photo by maitree rimthong on Pexels.com

    Hatua Za Kupanga Bajeti Kwa Wasio Na Kipato Rasmi

    Hapa ni kundi la wahitimu wasio na ajira na wale wasio na kazi rasmi zaidi ya kuunga unga kwenye kipato chao

    Hakuna utofauti mkubwa sana kati ya kundi la wenye kipato rasmi na kundi hili zaidi ya mambo machache

    Lakini pia hapa ni wale wasio na majukumu ya kutegemewa kabisa au wana wategemezi wachache sana.

    Kwenye kundi hili hupaswa kuzingatia mambo makuu matatu tu kabla ya mengine

    • Tumbo (chakula)
    • Kodi ( makazi) kwa waliopanga
    • Pesa za mizunguko , ada za watoto kwa wenye watoto na dharura zingine

    Hivyo utaratibu ni ule ule wa kufuata kama hapo juu isipokuwa baadhi ya vitu havifai kuzingatiwa

    Mambo kama misaada ya ndugu ,hesabu za mwaka na mwezi sio kitu cha kufanya kabisa kwakua kipato hakipo

    Kila pesa inayopatikana inapaswa kwanza kuzingatia vitu vya hapo juu kabla ya matumizi mengine yoyote

    Yaani hata kama hudaiwi kwa wakati huo ni vyema kujazia ili kuwa na uhakika zaidi wa baadae hata ikitokea kukwama

    Hii itasaidia kuweka akili kwenye utulivu na kuzingatia mambo ya msingi na yenye ulazima pekee kwanza

    Ukipata kibarua, dili au msaada wowote kimbia kujaza chakula ndani, ongeza kodi hata kama hudaiwi na lipa ada za watoto haraka

    Kisha weka pesa za nauli ya mizunguko mingine , vocha na dharura kama maradhi kwanza mahala salama

    Kamwe usitake kusaidia watu ikiwa na wewe huna kitu , utajiumiza pasi na sababu za msingi, watu hawana shukurani.

    Funga Kwa Lengo La Kubana Bajeti

    Dini zote zina utaratibu wa waumini wake kujizuia kula au kufunga katika baadhi ya siku nje ya miezi ya mfungo rasmi

    Mfano waislamu hufunga siku za alhamisi na jumatatu kama sunna ya Mtume wao Muhammadi (sw)

    Pia Dini nyingine ni vyema kufunga baadhi ya siku na kutokula kabisa ili kupunguza baadhi ya matumizi hasa kwa wasio na watoto

    Licha ya kufunga kuwa ( sunna) kusaidia kuleta mapenzi na kuongeza imani ,inaweza pia kusaidia kubana bajeti

    Na wakati huo huo kumfanya Mungu kufungua njia zaidi na baraka kwa mfungaji.

    Mambo Ya Msingi Ya Kuzingatia Ili Kuishi Ndani Ya Bajeti

    • Kubadili mtazamo kuhusu pesa na kuondoa mazoea yote ya awali yasiyo faa juu ya pesa
    • Kununua chakula cha jumla na kupika nyumbani na kwa wanao lazimika kula nje iwe angalau sehemu zenye gharama sawa na kipato
    • Kuishi nyumba ya bei nafuu zaidi
    • Kuishi karibu na eneo la kazi
    • Kuoa na kuacha idadi kubwa ya michepuko au kutulia na mpenzi mmoja aliye ndani wa uwezo wako
    • Kuandaa bima za afya na bima za makazi au usafiri kwa wenye uwezo
    • Kununua vitu vya bei nafuu vilivyo ndani ya uwezo na vinavyo dumu muda mrefu
    • Kupunguza starehe na makundi yasiyo na faida
    • Kurahisha mahitaji mara kwa mara kwa lengo la kudhitibi matumizi
    • Kuweka malengo ya muda mrefu na muda mfupi mara kwa mara
    • Kuwekeza kwenye vitu vinavyo zalisha kipato zaidi kwanza kabla ya vile vinavyo maliza pesa
    • Kusomesha watoto shule za gharama nafuu zaidi
    • Kutozidisha misaada kwa ndugu na rafiki iliyo pitiliza
    • Kutotembea na kiasi kikubwa cha pesa mfukoni
    • Kutonunua vitu vya anasa mara kwa mara
    • Kuepuka mikopo kwa namna yoyote ile isipokuwa kweye dharura kubwa zaidi.

    Hitimisho

    Pesa nyingi sana za watu hupotea bila wao kujua zimepoteaje kutokana na kukosa ufatiliaji sahihi

    Vile vile kuna tabia ambazo zinaweza kuwa ndogo ndogo ila ndio zinazo maliza pesa mara kwa mara

    Ni vyema kufanya tathmini ya mara kwa mara kwenye kipato hata kama ni kidogo ili kujua namna ya kupanga bajeti

    Bajeti sio lazima iwe ngumu sana bali ile inayo mpa mtu amani na uhakika wa kuishi ndani ya uwezo wake

    Hakuna pesa nyingi wala pesa ndogo bali matumizi sahihi ya bajeti ndio hupaswa kuzingatiwa zaidi

    Kuna ambao hutumia pesa kwasababu wana uhakika wa kupata nyingine hivyo hujisahau na kuja kushtuka wameishiwa

    Pia soma namna nzuri ya kupata mtaji kwa wenye kipato kidogo

    Pesa yapaswa kuheshimiwa ili nayo iweze kumuheshimu mmiliki wake.

    #YOU CAN WIN IF YOU WANT

    Share this article
    Shareable URL
    Prev Post

    Mbinu Za Kuondoa Uoga Na Hofu11 Min Read

    Next Post

    Jinsi Ya Kupanga Bajeti Ya Biashara6 Min Read

    Leave a Reply

    Your email address will not be published. Required fields are marked *

    Read next

    Huruhusiwi ku copy. Asante.