Utangulizi
Kujipa furaha mwenyewe ni kitu cha msingi sana kwenye kuitafuta ladha na furaha ya kweli maishani
Wengi huteseka sana ndani kwa ndani kwenye mioyo yao mpaka nje ya mioyo kwa kukosa furaha ya dhati
Kuna ambao husingizia ugumu wa maisha, changamoto za maisha na hata husingizia wengine kama chanzo cha wao kukosa furaha
Ila ukweli ambao mimi binafsi nina amini na kuuishi ndani yake ni kuwa furaha ni maamuzi ya mtu binafsi
Haijalishi sababu nyingine zozote, suala la kuwa na furaha haliingiliani na sababu yoyote ya nje ya moyo wa muhusika,
Binafsi niliteseka sana miaka ya nyuma kwa kukosa furaha ya dhati kwenye maisha yangu niliyoishi
Nilikuwa kati ya wale wanao amini maisha yapo kwaajili ya watu wachache ambao Mungu amewachagua
Nilimlamu sana Mungu mara kwa mara kwenye maisha yangu na kuona kama nimeletwa Duniani kuteseka
Ila mara baada ya kugundua baadhi ya vitu kuhusu maisha hakika hapa Duniani hakuna sababu yoyote inayoweza kunifanya nikose furaha
Haijalishi nitakuwa katika mazingira gani, nitaumizwa kiasi gani au nitapoteza vingapi hapa Duniani,
Kama havihusu kopoteza uhai basi kamwe siwezi kukosa furaha hata sekunde moja wala kuhuzunika kupindukia.
Furaha Haiuzwi Dukani
Hakuna duka lolote hapa Duniani ambalo unaweza kwenda kununua furaha yako unayotaka kuwa nayo
Wala hakuna kiasi chochote cha gharama kinacho tosha kununua furaha yako unayotaka kuwa nayo
Hivyo usipoteze muda wako kutafuta sana pesa ukiamini kuwa unaweza kununua furaha hapa Duniani
Kuna watu wana pesa na mali nyingi sana ila hawana furaha ya dhati japokuwa kwa nje huonekana wamekamilika
Wapo ambao hawana chochote kwenye maisha yao ila wana furaha ya dhati kutoka ndani ya mioyo yao
Unaweza kununua kitu chochote cha gharama yoyote Duniani ila kamwe huwezi kununua furaha yako
Kuwa na pesa au mali ni moja kati ya vitu vinavyosaidia kunogesha furaha ila sio chanzo cha kuwa na furaha.

Furaha Binafsi Hailetwi Na Watu Wengine
Kamwe usitarajie mtu mwingine yoyote nje yako binafsi akupe furaha unayohitaji kama wewe hujaamua kuwa na furaha
Wapo wanao amini furaha zao huletwa na wapenzi wao au wenza walionao kwenye mahusiano ya ndoa
Kuna wale ambao huamini kuwa furaha zao zipo kwa marafiki zao na bila kuzungukwa na marafiki basi hakuna raha
Kuna wengine huamini katika ndugu kuwa bila uwepo wa ndugu basi wao binafsi hawawezi kukamilika
Na kuna wale ambao bila watoto au wazazi kamwe hawawezi kuwa na furaha binafsi na hujiona kama hawajatimia.
Kila mmoja ana tafsiri yake ya furaha, ila linapokuja suala la furaha ya dhati kutoka moyoni halihusiani na kitu chochote
Kuwa na wengine kama sababu ya furaha ni sahihi kabisa ila kuwategemea wengine kama chanzo cha furaha ni kosa
Binaadanu anahitaji watu ili aweze kujihisi mwenye furaha ila watu sio sababu ya binaadamu kukosa furaha
Ndio maana watu huja na kuondoka kwenye maisha kwa sababu mbali mbali na hata ile sababu kubwa zaidi ya KIFO,

Mungu Hakuweka Kifo Ili Kunyima Watu Wake Furaha
Kifo kimewekwa na Mungu sio kwa maana kuwa hataki watu wake wawe na furaha bali anathibitisha kuwa unapaswa kutimia hata bila wengine
Kama Mungu angeweka wengine kama chanzo cha furaha ya mtu basi Kifo ingekuwa adhabu kubwa ziadi
Ila kifo pekee ni ishara kuwa yoyote anapaswa kuishi bila mwingine na kufurahia maisha yake na kugandana sio furaha ya maisha
Ndio maana kifo hakichagui yupi wa kuondoka na yupi wa kubaki bila kuangalia uhusiano wala umri wa mtu huyo
Na maisha hupaswa kuendelea bila kujali wangapi wameondoka au kubaki kwenye maisha ya mtu.
Kwa hio suala la kujipa furaha binafsi ni lazima sana kwenye maisha ili kuishi ndani ya kusudi la Mungu.
Kumbuka ulizaliwa peke yako na pia utakufa peke yako.
Kujipa Furaha Binafsi Sio Jambo La Maigizo
Kuna watu hutia huruma sana hapa Duniani, wao hufanya kila wanachoweza kuaminisha wengine kuwa wana furaha
Wengi huigiza furaha zao kwa nje ila kwa ndani ya mioyo yao wanateketea vibaya sana kila sekunde!
Kujipa furaha binafi sio suala kubwa wala halitaki maigizo kama wafanyavyo wengine kwenye macho ya jamii
Bali furaha ni suala binafsi na linaanza ndani ya mtu mwenyewe hata bila ulazima wa kuonesha wengine kwa vitendo.
Kama Huwezi Kujipa Furaha Binafsi Basi Kamwe Hutoweza Kuwapa Furaha Wengine
Ni sawa na upendo ,kama huwezi kujipenda wewe binafsi utawezaje kupenda wengine? upendo unaanza na wewe kwanza
Ni lazima na sio suala la hiari ,kuanza kujipa furaha wewe mwenyewe kabla hujaanza kufikria kuwapa wengine
Siku zote ukiwa na furaha wewe mwenyewe binafsi kwanza huvutia na wengine kuwa karibu na wewe
Kwasababu moja tu kuwa hata wao wataamini unaweza kuwafurahisha kama umeweza kujifurahisha wewe binafsi.
Unaweza kushangaa unajitoa sana kuonesha watu kuwa umekamilika ila bado wakakuacha na kukukimbia
Jibu huwa rahisi sana kuna uwezekano mkubwa wewe mwenyewe huna furaha ile ya dhati kutoka moyoni.
Watu Hugawa Kinachozidi
Kwenye maisha mara nyingi watu hugawa kile kilichozidi, ni mara chache sana mtu kutoa kile anachohitaji
Japokuwa sio jambo zuri kumpa kitu mtu baada ya kuvimbiwa ila ndio uhalisia ulivyo na haupingwi kamwe .
Hivyo ukiwa na furaha binafsi huwa rahisi kugawia wengine furaha inayozidi na kamwe huwezi kuwapa ikiwa bado unaihitaji
Yani wewe mwenyewe huna furaha na unahitaji furaha sasa utawezaje kugawia wengine furaha?
Vile vile ukiweza kujipenda wewe binafsi kwanza basi pia utaweza kupenda wengine au mtu mwingine
Na watu hufurahia zaidi wale wanao jipenda wao binafsi kwakuwa huamini hata wao watapendwa pia
Huwezi kumuaminisha mtu unampenda na utamlinda ikiwa wewe binafsi unaonesha hujipendi!
Hivyo anza kujipa furaha mwenyewe kabla ya kuwapa wengine au kungoja wengine kukupa furaha.

Dalili Za Mtu Asiye Na Furaha
Kucheka Sana Sio Ishara Kuwa Una Furaha
Kuna dalili nyingi sana zinazoonesha kuwa mtu hana furaha ya dhati kutoka moyoni bila kujali mafanikio yake ya nje
- Hasira za mara kwa mara
- Kupaniki hovyo hasa kwa mambo madogo madogo
- Kufatilia sana maisha ya watu wengine
- Kulala sana au hata kukosa usingizi mara kwa mara
- Kuongea maneno ya kukata tamaa hata kutamani kufa
- Kuchoka kila wakati bila sababu za msingi
- Kuhisi hali ya upweke kupitiliza
- Kuchukia maisha yake binafsi licha ya baraka alizonazo
- Kujitenga sana na watu hata pasipo na sababu maalumu
- Kutumia nguvu kubwa kuonesha wengine kwa vitendo kuwa ana furaha
- Kushindana na wengine hasa kwenye mambo yasiyotaka ushindani
- Msongo wa mawazo kupindukia
- Kusema wengine vibaya mara kwa mara na kuwakosoa hata wanapofanya vizuri
- Kauli za kujinadi na kujidai mara kwa mara. NK
Mara nyingi mtu mwenye furaha ya dhati kwa ndani hahitaji wengine kujua au kuhakiki furaha yake kamwe.
Kufurahia Maisha Haimaanishi Kufanya Sana Starehe
Kuna wengi sana huamini furaha ni starehe hasa pombe na ngono! watu hawa hufanya kufuru sana kwenye maisha yao
Wao kubadili wapenzi kama nguo ni jambo la kawaida sana wakiamini kuwa ndio wanajipa furaha
Au kuharibu pesa nyingi kwenye vilevi ndio huona kama wanafurahia maisha na kujipa furaha.
Japokuwa ni sawa kutafsiri maana ya kufaha kwa aina hio ya maisha ikiwa kama ni kweli inampa muhusika amani
Ila hakuna uhusiano wowote ule kati ya furaha,ngono na pombe.
Usisahau kuwa unaweza kufanya starehe kulingana na bajeti na starehe ambazo hazina madhara kiafya.
Udogo Wa Mafanikio Sio Sababu Ya Kukosa Furaha
Haijalishi kwa sasa uko wapi na unafanya nini ,kamwe hupaswi kusubiri kitu chochote ili uwe na furaha
Kujipa furaha binafsi sio suala la kungoja ukubwa wa mafanikio fulani kwa sababu Dunia ni Njia tu kuna siku utaondoka
Vipi sasa ukiondoka bado hujapata mafanikio uliyotaka , je utaishi maisha ya huzuni na kuondoka ukiwa na huzuni?
Yaani unakubali kuja Duniani kuhuzunika kisha kufa ukiwa na huzuni bila kufurahia maisha kabisa?
Tunaishi mara moja tu na uhai hauna mbadala wowote , ni lazima kufurahia maisha kwa namna yoyote ile .
Kama kuna kitu cha kupigania duniani kabla ya vingine basi ni furaha na inapaswa kutangulia mbele kabla ya chochote
Fanya ujuavyo vyovyote vile kwa namna yoyote ila siku isipite ukiwa hujafurahia siku yako uliyoishi.
Ni Kweli Changamoto Zipo
Kuna siku mbaya na siku nzuri, mwezi mbaya na mwezi mzuri na hata mwaka mbaya na mwaka mzuri
Hata uwe jasiri vipi zipo siku mambo huwa magumu zaidi na unapaswa kukubali ukweli, kulia na hata kuumia,
Ila baada ya yote simama imara na rejesha tabasamu lako kama mwanzo kwani maisha lazima yaendelee.
Naelewa sana kuwa kuna changamoto za maisha hufanya watu kuwa na huzuni kubwa sana hapa Duniani
Najua kabisa kuwa maisha yametofautiana sana kati ya mtu na mtu au familia na familia pia nchi na nchi
Pia kuwa na mali , pesa au mahusiano na familia bora ni kitu kikubwa sana kwenye kujenga furaha kwa mtu,
Ila mbali na yote hayo maisha hayarudi nyuma , pia huwezi kulazimisha kupata vitu kabla ya muda wake sahihi
Ila furaha ni maamuzi binafsi ya mtu wakati wowote na sio chaguo la Mungu kwamba anagawa yupi afurahi,
Mungu inawezekana kweli anagawa mali ,mwenza au pesa ila kamwe hagawi furaha kwa mtu mmoja mmoja
Ndio maana kuna watu vijijini huko ndani ndani hawana chochote ila ukikutana nao unaweza kutamani maisha yao
Na wapo wegine mjini wanamiliki vitu vingi sana ila wamechagua kukosa furaha!
Kwahio inawezekana huna mafanikio yoyote yale kwa sasa ila kamwe isiwe chanzo cha huzuni kwenye maisha
Na hata ukipata mafanikio na ikatokea umeyapoteza basi isiwe tena chanzo cha huzuni yako kwa baadae.
Furaha Hupaswa Kuwepo Muda Wote Kwa Mtu Bila Kujali Mazingira Ya Nje
Yoyote awezaye kutunza furaha yake bila kujali mazingira ya nje au changamoto anazopitia kwenye maisha yake,
Basi pia anaweza kutunza chochote kile kingine iwe chake au cha mwenzake kwa uaminifu mkubwa sana
Kuweza kutunza furaha binafsi ni ishara tosha ya mwingine kuamini kuwa yupo na mtu sahihi na anaefaa.
Changamoto za maisha haziepukiki haijalishi zimesababishwa na nini, kitu cha msingi ni kuwa kamwe haziishi
Ni vile zimetofautiana ukubwa au namna zinavyo muandama mtu husika na mwingine tu .
Haijalishi unapitia mangapi, furaha hupaswa kubaki vile vile kama ilivyo ndani yako wewe binafsi
Hata kama nje ya mwili kuna kila sababu za wewe kuhuzunika bado unapaswa kulinda furaha yako ya ndani.
Chukulia Mfano Wa Samaki Na Bahari
Unapaswa kuwa kama samaki baharini, licha ya kuishi ndani ya maji yenye chumvi bado samaki hazina ladha ya chumi.

Furaha Ni Ufunguo Na Sumaku Ya Kunasa Vingi
Ukiondoa IMANI kama funguo ya kwanza ya mafanikio kwenye kitu chochote maishani,Furaha ni funguo mwingine
Ukiwa na furaha ya dhati sio ile ya kuigiza maana yake pia akili yako ni chanya sana kwenye changamoto unazopitia
Ukiwa na akili chanya maana yake ni rahisi sana kuishi na kila mtu, kuvumilia changamoto na hata kutatua changamoto
Na hio ni moja kati ya vitu ambavyo huchochea sana mafanikio kwenye maeneo yote muhimu ya maisha ya mtu.
Ukiwa na furaha ya dhati ,utanasa wateja ,utanasa wawekezaji, utanasa marafiki wa kweli, utanasa fursa NK
Furaha ya kweli husaidia sana kwenye kujituma kwa dhati na kuipa akili uwezo mkubwa wa kufikiri na hata kufanya maamuzi sahihi.
Pia soma namna ya kupata furaha na amani kwenye maisha.
Namna Ya Kujipa Furaha Binafsi
- Badili namna unavyo fikiri na kuchukulia mambo
Ili kujenga furaha ni lazima uwe na fikra chanya kwenye mambo yote yanayotokea au kukuzunguka na yaone kawaida katika jicho chanya
- Jipende na jipe kipaombele
Zingatia mapenzi yako binafsi kabla hujapendwa au kupenda wengine,jijali na jifanyie mambo mazuri wewe mwenyewe kwanza
- Jinunulie zawadi mbali mbali
Usingoje kupewa au kukumbukwa , kama una uwezo jikumbuke mwenyewe na kanunue unachotaka chako binafsi
- Usijilinganishe na wengine
Epuka kujilinganisha na kuona wengine wamekuzidi hata kama ni kweli,wewe jiamini unachofanya na jinsi ulivyo
- Punguza matumizi ya mitandao
Hasa kama huitumii kuingiza kipato kwani wengi huishi maisha yasiyo halisi mitandaoni na yanaweza kuharibu furaha yako
- Tafuta muda wa peke yako
Mara kwa mara kaa mwenyewe na zoea kuwa mwenyewe bila uwepo wa mtu yoyote yule ili ujijue kwa undani zaidi na ongea na nafsi yako
- Jifunze kusema hapana na weka mipaka yako
Sema hapana bila uoga kwa jambo lolote lile ambalo hulitaki kamwe usifanye kitu kisha kujutia
- Acha mambo yapite kama yalivyo
Usifatilie kabisa maneno ya watu wala vitendo ambavyo havikuhusu zingatia maisha yako tu
- Weka malengo na yafatilie
Weka akili yako kwenye malengo unayotaka kutimiza
- Fanya mazoezi na jali afya yako
Afya ni msingi wa furaha na unapaswa kuwekeza kwenye afya yako
- Usilazimishe wengine kukupenda
Kamwe usitake wengine wakuthamini na jifunze kuwaacha waende
- Kubali uhalisia wa mambo
Yale ambayo huwezi kuyabadili yaache kama yalivyo wala usipambane na yaliyo shindikana
- Jiamini na jikubali
Haijalishi upoje na unaishi vipi ,unapaswa kujiona wa thamani kubwa sana kwenye maisha yako.
Mambo Mengine Yanayo Saidia Kujipa Furaha Mwenyewe
- Kusafiri mara kwa mara sehemu ambazo hujawahi kwenda kulingana na kipato chako
- Kunywa na kula chakula unachofurahia zaidi kwenye moyo wako
- Kukaa karibu na mazingira yanayovutia kwenye macho yako
- Kufanya ibada kulingana na Imai yako
- Kuwa msiri na kutoweka maisha yako binafsi wazi kwa kila mtu
- Kuwa na mibadala na machaguo mengi na kutotegemea jambo kutoka kwa mtu au kitu kimoja
- Kufanya tahajudi mara kwa mara
- Kusikiliza wimbo kwa sauti ya juu na kucheza mziki unao upenda ukiwa peke yako
- Kuimba na kucheza wakati wa kuoga bafuni
- Kuishi ndani ya bajeti na kipato chako
- Kupanga ratiba binafsi kuendana na majukumu ya kila siku
- Usafi binafsi na mazingira unayokaa hasa chumbani na kutandika kitanda kila asubuhi
- Kujitegemea kwenye kipato na maisha bila kuhitaji msaada au kuomba omba
- Kuangalia tamthilia nzuri au kusoma vitu vinavyokuvutia
- Kutazama kioo mara kwa mara na kujinenea maneno mazuri NK
Hitimisho
Watu wengi sana hawaamini kama inawezekana kujipa furaha binafsi bila uhitaji wa watu wengine kwenye maisha
Mwisho wa siku wanaishia kuumizwa na kuishi chini ya nyayo za wengine kisa furaha zao binafsi
Kosa kubwa zaidi ni kuweka furaha yako rehani kwa mtu mwingine kabla yako wewe mwenyewe
Watu hubadilika muda wowote na kuwategemea wao kama chanzo cha furaha yako binafsi ni kosa kubwa sana.
Ukweli ni kuwa ni jambo rahisi sana kama utaamua kuishi na kumiliki furaha yako mwenyewe binafsi
Hakika unaweza kwenda popote na kufanya jambo lolote lile bila kuhitaji mtu mwingine wa kuongozana nae
Ishi maisha yako na furahia uumbwaji wako bila kutaka wengine waishi na wewe.
Woooow penda sana hii kitu nzuri
Ahsante sana na barikiwa sana