You Can Win If You Want

Namna Ya Kuongeza Ubora Wa Maisha Kwa Kipato Kidogo14 Min Read

kuongeza ubora wa maisha kwa kipato kidogo

Utangulizi

Ubora wa maisha ni kilio cha kila mtu hapa Duniani ,kila mmoja anapambana kuishi maisha bora zaidi kila wakati,

Kuongeza ubora wa maisha ni tofauti kabisa na kuongeza ubora wa kitu unachofanya iwe biashara au kazi.

Hapa tunaangalia namna ya kufanya maisha kupata thamani zaidi na kuvutia kupitia matumizi ya kila siku

Matumizi ambayo hupatikana baada ya kuongeza ubora wa kazi au biashara zinazofanywa kwenye maisha ya kila siku,

Kujua zaidi namna ya kuongeza ubora wa kazi na biashara ili kupata kipato zaidi soma hapa kwa kubonyeza link hii.

Kuna tofauti kati ya ubora wa kazi na ubora wa maisha binafsi ,hivi vitu vinaendana ila haviingiliani kabisa

Japokuwa kimoja hupaswa kutangulia ili kubeba kingine ( ubora wa kazi kwanza kabla ya ubora wa maisha binafsi).

Ajabu huja pale wengi hasa vijana hutaka kuboresha maisha yao binafsi kwanza kabla ya kuboresha vipato vyao!

Na ili kuboresha kipato maana yake ni lazima kuboresha kazi au biashara (huduma au bidhaa) unayofanya kwanza,

Hivyo basi ubora wa maisha binafsi huhusisha zaidi matumizi kupitia kipato wakati ubora wa kazi ni kuongeza thamani ya kazi kabla ya kipato.

kuongeza ubora wa maisha
Photo by Scott Webb on Pexels.com

Udogo Wa Kipato Sio Sababu Ya Kuishi Kichovu

Kuna tofauti kubwa kati ya kuwa na kipato kidogo ( masikini) na kuishi kichovu au tuseme kujitupa (kujiacha nyuma)

Mfano Wa Kwanza

Niliwahi binafsi kutembelea nyumba fulani nikakuta chooni wanatumia kopo la maji ya uhai (lililokatwa nusu) kujisafishia!

Kilicho nishangaza zaidi sio kopo ila uchafu wa kopo lenyewe, yani kopo lote limeweka utandu wa kijani kiasi kwamba huwezi hata kulishika!

Sasa hio haikuwa shida kabisa tufanye ni sawa (maana kopo zuri kiasi huuzwa shilingi mia 500 au 1000 tu za Tanzania),

Wenyeji wa nyumba hio wanaishi maisha ya kawaida tu na ukikutana nao njiani walivyopendeza huwezi tegemea kabisa.

Au

Tuchukulie hawa watu hawana kabisa uwezo wa kununua kopo la mia 500 ,je kuokota kopo lingine pia ni kazi nzito?

Yani kuzunguka na kutafuta kopo la maji lingine pia ni umasikini? au uvivu wa kufikiri wa wahusika?

Basi tufanye hakuna kabisa makopo mengine ya maji yaliyotupwa, je kusafisha kopo hilo pia ni suala la umasikini?

Au ni uvivu wa kufikiri na kutenda?

Ukweli ni kuwa tunaupa sana umasikini lawama ambazo hazina msingi ikiwa makosa ya kuboresha maisha ni yetu wenyewe.

Ukweli wangu nilishindwa kabisa kutumia kopo lile na kulazimika kwenda duka la jirani kununua kopo jipya,

Sikutaka kabisa kujali watanionaje ila ninaamini nilifanya jambo sahihi zaidi.

Kuboresha maisha
Photo by Alper Tufan on Pexels.com

Maendeleo Binafsi ( Maisha Bora)Ni Mchezo Wa Akili Zaidi Ya Kipato

Wapo watu nimewahi shuhudia binafsi ,wana kipato cha kawaida tu ila wanaishi maisha ya ajabu sana !

Hawa hutumia pesa zao kwa mambo yasiyo na lazima sana halafu maisha yao binafsi huona hayana maana kwa kisingizio cha umasikini,

Kuna mtu kwa siku huweza kunywa bia kati ya mbili na kuendelea wala haoni shida kabisa ila chakula achokula sasa…

Nguo anazovaa….

Nyumba anayoishi….

Hata muonekano wake kwa ujumla….

ILA

Hakosi pesa ya bia (kuweka heshima bar ) na kuhonga wanawake.

Mfano Wa Pili

Nimewahi kwenda kijiji kimoja wilaya ya kibondo kwa rafiki yangu alikuwa muajiriwa (Mwalimu)kwa lengo la kumtembelea,

Nilishangaa sana maisha wanayoishi Walimu wa eneo lile akiwemo rafiki yangu ! Na hata sikufumbia macho kabisa niliwaambia ukweli.

Walimu wanaishi maisha ya ajabu sana kwa kisingizio cha mshahara mdogo na Serikali haijafanya!

Nyumba haina taa! hakuna choo salama! hakuna vitasa vya milango, nyumba zimechoka matundu kila mahala na wala hawajali kabisa

Eti wanasema Serikali haifanyi kwahio na wao hawawezi kufanya kabisa kwa bajeti zao binafsi kutoka ndani ya mshahara.

Yani Mwalimu umesoma na kuelimika ila unaishi kwenye nyumba haina taa zaidi ya tochi ya simu yako! walio na familia wanatumia vibatari,

Mwalimu mzima unatumia choo hakina mlango ,kuna pazia la magunia tena yaliyotoboka toboka! hata kuweka gunia jipya pia ni kazi ya Serikali?

Chooni unapaswa kuingia kwa tahadhari maana ukicheza kidogo unaweza kudumbukia kwa sababu hakipo imara kabisa.

Aise eti Mwalimu anaishi nyumba haina vitasa vya milango na inavuja kila mahala hata kulala kazi siku mvua ikinyesha!

Mwalimu anakaa chumba hakina madirisha zaidi ya nguo chakavu anayotundika dirishani bila aibu wala uoga!

Niliishiwa nguvu kuona matundu kila kona ya nyumba ambayo yamegeuka kuwa makazi ya panya wakubwa hata kimuonekano

Kubwa kuliko ni kuwa hawa Walimu wanaona kawaida sana tena wanaishi kama vile hakuna tatizo lolote.

Hayo yote unahisi watoto wanao fundishwa na walimu hawa ,wana kipi cha kujifunza zaidi kwenye maisha binafsi?

Ajabu Zaidi Sasa

Walimu hawa wana simu toleo jipya ( smartphone za maana tu) na kila mmoja huenda kuchaji kwenye duka la kijiji kwa pesa,

Yaani walimu ( hususani rafiki yangu) kila mwezi lazima anunue nguo mpya na kila wiki lazima aende mjini kusuka!

Gharama ya kwenda mjini ni mpaka elfu 22 na wala haoni uchungu wowote ule ndio kwanza anawaza mitindo mipya ya nywele!

Hivi kuna ulazima gani wa kusuka nywele mpya kila wiki kwa maisha ya kijijini? (Unaweza kusuka sawa ila boresha na makazi yako pia)

Gharama za kusuka na matumizi ya siku nzima akiwa mjini ni zaidi ya pesa inayotakiwa kukarabati nyumba anayokaa (Mafundi ya vijijini hawana makuu)

Kubwa kuliko hakuwa anakunywa maji ya kijijini (ni maji safi na salama tu) ila ananunua maji ya chupa kwa bei ya jumla kutoka mjini!

Nilichoka kuona walimu hawa wanatumia majiko ya gas (kumbuka gas haiuzwi kijijini ni lazima kuifuata wilayani kibondo),

Hivyo hulazimika kulipia usafiri wa mtungi wa gas kati ya elfu 8000 kama wakimpa dereva au 22 kama wakienda wenyewe

Na hapo bado pesa ya kununulia gas husika, wakati huo huo gunia la mkaa lile kubwa sana kijijini wanauza elfu 7 tu!

Tena unaweza tumia zaidi ya miezi 5 kwa asiye na familia kubwa bila kumaliza mkaa na hapo bado msimu wa kiangazi mkaa hushuka bei zaidi.

Sasa Jiulize

Hii tunaweza kuiweka katika kundi gani? nani alaumiwe kati ya Walimu na Serikali?

Je, nikukosa Elimu ya maendeleo binafsi au uchoyo na roho mbaya kuona wakirekebisha watanufaisha wengine?

Au tuseme ni ujinga wao maana tusisingizie kabisa kipato wanachopata.

Shangaa Hapa Zaidi

Baada ya kukaa nao na kuona maisha wanayoishi, sikukubali kabisa niliamua kuwasanua kwanza

Hivyo nilianza na rafiki yangu maana ndio mtu ninaeweza kummudu zaidi na kumpa ukweli wa mambo yalivyo,

Tuliongea sana na hata yeye hakuwa na majibu ya kwanini anaishi maisha yale tena alibaki anasema eti huenda amerogwa!

Sikuwa na mzaha niliamua kuingilia kati na kumsimamia kama mama yake hatua kwa hatua maeneo yote yarekebishwe

Tulianza na choo ambacho marekebisho yote haikuchukua hata shilingi Elfu 25 za Tanzania!

Tukarekebisha vitasa, kuziba matundu ya panya na kuweka viraka vya mabati sehemu zinazovuja na madirisha( haikuzidi elfu 40)

Kisha akanunua mkaa gunia kubwa halafu gas nikamwambia atumie kwa vitu vyepesi tu ili angalau ikae mieiz 3 na kuweza kubana bajeti,

Kwenye maji ya kunywa ndio kabisa nilipiga marufuku maana hata maji wanayotumia wanakijiji ni salama sana na ,

Yamejengewa kisima imara kwa msaada wa wazungu (USAID) hivyo hayana shida yoyote na yanafaa kwa kunywa

Kwenye taa ilibidi achukue sola ndogo kwa mkopo na mengine yote tuliweka sawa kabisa ndani ya muda mfupi.

Walimu wengine walianza kuiga mmoja mmoja na walijikuta wanaishi maisha tofauti sana na awali hata wanafunzi na wanakijiji walishangaa sana.

kuboresha maisha kwa kipato kidogo
Photo by ezecutiveshot on Pexels.com
Mfano Wa Tatu

Wilaya ya Kigamboni kuna kambi ya jeshi ambayo sitoitaja kwa sababu za usalama zaidi na kuheshimu uhusika wa mtu,

Niliwahi kuwa na mahusiano na mwanajeshi kijana mmoja mdogo tu kwa umri na hana majukumu makubwa ya maisha,

Kijana huyu alikuwa na cheo kizuri tu kwa maana ya mshahara wake pia haukuwa mdogo kama tujuavyo kazi za jeshi.

Hakuwa mtumiaji wa kilevi aina yoyote ile wala mpenda starehe zinazo maliza pesa, kwa ufupi alikuwa mtulivu sana

Yule kaka alikuwa na tabia moja pengine tuite maozea mabaya au ulimbukeni ulio pindukia baada ya kupata vijisenti!

Hakuwa anakaa na chenji ( yaani akinunua kitu ,hutoa noti ya elfu 10 kisha chenji inayobaki haitaki kabisa) kama nipo nae hunipa zile chenji!

Ninapo ongelea chenji simaanishi pesa za sarafu pekee bali hata anapo nunua kitu cha elfu 1000 ikibaki elfu 9000 huwa haichukui,

Kiufupi hataki kukaa na pesa mfukoni zaidi ya noti nzima za elfu 10000 tu.

Mwanzo sikuwa naelewa na nilihisi anapenda kunipa pesa za chenji nitunze kwa matumzi madogo madogo yajayo,

Hivyo sikuwa namuuliza kitu, kila tunapotoka na afanyapo manunuzi basi hutoa noti ya elfu 10 kulipia kisha chenji inayobaki hunipa yote.

Niliamua Kuanza Uchunguzi

Baada ya tabia ile kuota mizizi nilianza kuhofia na kuona sio jambo la kawaida kabisa (najua ni ngumu kuelewa au hata kuamini)

Ila ni jambo la ukweli kabisa halina hata chembe ya uongo ndani yake (soma na jifunze).

Sababu kubwa ya kuchunguza ,nilihisi labda ni mambo ya ushirikina au kuna namna anafanya vile kama kutimiza maagano yake,

Kwasababu hakuwahi ishiwa pesa na hakuwa na biashara zaidi ya kazi yake tu sasa iweje anachezea pesa namna ile!

Nilifuatilia na baadae nikagundua kuwa ndivyo alivyo na hata marafiki zake wote wanajua tabia yake.

Kitu Cha Ajabu Zaidi

Kaka yule au tuseme mpenzi wangu (tuliachana baadae) alikuwa anavaa mavazi yale yale kila siku yaani shati moja na suruali moja tu,

Sijui alikuwa anafua muda gani maana sikuwa naishi nae pamoja ( nilidhani ana nguo za rangi moja labda)

Ila haikuwa hivo ,ni kweli kabisa alikuwa na nguo moja tu (suruali na shati) kila tunapo onana huwa amevaa hizo hizo,

Tukiondoa gwanda ( sare) za kazini za kijeshi, hakuwa na nguo nyingine yoyote ile ya kuvaa zaidi ya shati na suruali moja tu.

Mwanzo nilipata sana shida kumuuliza pia sikutaka kabisa ajisikie vibaya ila wasiwasi ulianza kunitanda zaidi,

Kila nilipo linganisha mavazi yake na aina ya matumizi ya pesa zake havikuendana kabisa na niliona kabisa kuna kitu hakipo sawa .

Hii iliongeza sababu za kuhisi labda ana maagano ya ushirikina.

kuboresha maisha
Photo by Lukas on Pexels.com
Niliamua Kumuuliza

Kutokana na mapenzi ya dhati niliyokuwa nayo kwake, sikutaka kuona anaharibikiwa au mimi kuvumilia maisha yale anayoishi,

Nilitamani abadilike na pia nimshauri aweze kuwekeza au kufanya mambo ya maana zaidi kwa ajili ya maisha yake.

Hivyo siku moja nilijikaza na kuongea nae taratibu nijue shida ni nini? kwanini anavaa nguo moja na kwanini anatumia pesa ovyo!

Ukweli hata yeye hakuwa na jibu la moja kwa moja zaidi ya kuinama chini kwa muda mrefu sana kwa aibu,

Upande wangu pia nilikuwa na hofu ya kuharibu mahusiano yetu kwa maana sikujua atachukulia kwa uzito gani.

Ila baada ya muda kupita wa ukimya (hakunijibu kabisa) aliniaga kuwa anaenda mahala na atakuja baada ya masaa mawili

Kweli alirudi akiwa na mfuko uliojaa nguo nyingi mpya za kiume (kumbe alienda dukani kununua nguo).

Nilifurahia sana kuona kumbe sijaharibu mahusiano na hata yeye alisema “umenifungua macho sijui na sina jibu la kukupa kwanini sikuwa na nguo”.

Kuboresha Maisha Sio Lazima Uwe Na Kipato Kikubwa

Kuna watu huamini ili maisha yao yawe mazuri basi lazima wawe na nyumba kubwa ,gari kali na hata vitu vya kifahari,

Kumbe unaweza kuwa na maisha bora hata ukiwa unakaa chumba kimoja tu ,bila kujali unaingiza kiasi gani.

Hakuna uhusiano mkubwa kati ya pesa nyingi na kuboresha maisha binafsi kwani hili ni suala la akili ya mtu,

Watu wengi sana vijijini wana maisha mabaya na mabovu huku wanalalia pesa ndani! kama huamini kaishi vijijini uone.

Watu hawa hawana Elimu ya maendeleo binafsi na wamechagua kuishi maisha duni wakiamini hawana uwezo wa kuishi vizuri

Hulalia vitanda vya miti na nyasi au kulalia mikeka kabisa au hata chini kwenye udongo ,sio kama hawana pesa hata kidogo!

Bali hawajui haswa pesa zao zitumike vipi ili kuongeza ubora angalau kidogo kwenye maisha wanayoishi.

Vijijini hulima na kuuza mazao yao kila mwaka, hupata pesa kiasi lakini maisha yao hubaki vile vile miaka yote,

Kuna wanaume na vijana shupavu sana bila kusahau uwepo wa miti kila aina ila hata kuboresha vyoo wanavyotumia,

Au nyumba wanazokaa pia huona kazi sana kwa imani kuwa wao ni masikini!

Kumbuka

Kuboresha maisha sio kutumia vitu vya bei kubwa sana bali uwezo wa kujua kipi kinafaa na kitumike vipi basi.

Mifano ni mingi sana inayogusa suala la ubora wa maisha ila tuishie hapo kwanza.

man pouring water from dipper on blue and grey house
Photo by hitesh choudhary on Pexels.com

Hivi Suala La Uchafu Pia Linagusa Umasikini?

Sijui hii ikoje! wala sielewi kabisa uhusiano wa uchafu na umasikini? yaani hawa ni kama mapacha wawili wanao fanana sana

Masikini wameshajiona pia uchafu ni sehemu ya tamaduni zao na wakisafisha mazingira ni kama wanavunja miiko yao,

Tembelea mitaa ya watu wenye maisha mazuri na kisha tembelea mitaa ya masikini utajifunza kitu kikubwa!

Si hivyo tu pia tembelea nyumba za wenye pesa ( hata wale wa maisha ya kati)kisha tembelea nyumba za masikini utaona utofauti.

Asilimi 99 ya masikini wamezingirwa na uchafu uliokithiri kuanzia sehemu wanazolala mpaka mitaa ya nje,

Nyumba za masikini zimejaa makorokoro utadhani dampo ,vitu havina maana vya miaka 77 bado vipo kuanzia darini mpaka kwenye uvungu wa vitanda.

Mitaa sasa ndio mtihani mwingine ,wao hata kutupa takataka kwa ustaarabu ni mtihani mzito sana wanaona sawa taka kujaa mpaka milangoni,

Ukija kwenye maji taka sasa ndio usiseme yaani hawaogopi hata maradhi ya mripuko.

Ustarabu Ndio Kama Mjomba Wao

Kelele na ugomvi usio na tija hupatikana mitaa ya wanaojiita masikini (uswahilini huko)

Kuwasha redio mpaka usiku bila kujali wenzao walio pumzika hilo ndio kama halisumbui kabisa.

Kiufupi ustarabu ,kelee,uchafu huwezi kukosa kwa watu wanaojiita masikini( kimsingi umasikini ni akili ya mtu).

Njia Za Kuboresha Maisha Kwa Kipato Kidogo

Kwa wewe ambae unasema huna kipato wala pesa za kuweka muonekano wa maisha yako vizuri sasa basi kwa ujumla fanya hivi:

  • Anzia chumba unachokaa (toa makorokoro yote kwanza yasiyo na muhimu)
  • Safisha vyema chumba (nyumba unayokaa)
  • Chunguza kitu kimoja baada ya kingine na acha vitu muhimu tu ( vilivyobaki gawa au choma moto)
  • Angalia sehemu zote zinazotaka maboresho hapo unapokaa ( yale unayoweza kufanya mwenyewe kwanza)
  • Chukua kalamu na daftari kisha andika vitu vyote, ambayo unahisi unataka kununua ili kuboresha maisha ya nyumbani kwako (kwa namna unavyoona inafaa)
  • Angalia mavazi yako pia yote (toa nguo zisizo na maana haijalishi utabaki na nguo ngapi)
  • Panga upya bajeti yako ili uone kitu gani ambacho sio cha msingi humaliza pesa zako na elekeza hio pesa kwenye maboresho ya maisha kwanza.

Siri Za Kuboresha Maisha (Kuishi maisha bora)

  • Wekeza vitu unavyotaka taratibu ( tafuta duka linalouza kitu unachotamani kisha peleka pesa kidogo kidogo ili ukimaliza malipo ukichukue)
  • Kuwa na vitu vichache sana ila vizuri (usinunue mavitu mengi badala yake weka nguvu ya pesa kwenye vitu vichache ila vyenye muonekano mzuri) mfano :Unaweza kuwa na godoro moja kubwa zuri la nchi 10 mpaka 12 badala ya kuwa na godoro pamoja na kitanda kisicho na mvuto
  • Zingatia usafi (mazingira unayokaa na mwili wako hususani mavazi)
  • Nunua nguo nzuri (hata kwenye mitumba kuna nguo kali za bei ndogo sana )hakikisha una muonekano nadhifu hata kwa nguo za mitumba na usiache kupiga pasi hata kama ni pasi ya mkaa
  • Ondoa matumizi yasiyo ya lazima kwanza kisha weka nguvu ya pesa yote kwenye maisha yako binafsi ( jipende wewe kwanza)
  • Kula vizuri mlo kamili (zingatia chakula chenye afya) ukiweza pika mwenyewe
  • Fanya mazoezi ya viungo ili uwe na muonekano wa kuvutia (unaweza kufanya mazoezi hata ndani kwako)
  • Ishi mitaa isiyo na makelele sana (kuna nyumba nzuri sana mpya za bei ndogo nje kidogo ya mji)kama hulazimiki kukaa katikati ya mji
  • Tafuta nyumba ya kupanga mpya ambayo imekamilika maboresho (achana na nyumba za zamani) wala usipange nyumba wenye wapangaji wengi.

Mambo ni mengi sana hatuwezi kuandika yote ila zingatia hayo machache kwanza.

Hitimisho

Ukweli ni kuwa hakuna haja ya kusubiri uwe na pesa nyingi sana ndio uishi maisha bora kwasababu huwezi kujua lini utapata hizo pesa,

Siku zote unapaswa kuishi vizuri wakati huo huo ambao unatafuta maisha mazuri bila kujali sana yajayo.

Lakini pia epuka kuharibu bajeti kwenye maisha binafsi kabla ya kuboresha kipato chako rasmi na biashara unayofanya,

Ina maana kuwa hupaswi kujiacha nyuma sana wakati unasaka maisha na hupaswi kuharibu pesa wakati unajiweka mbele.

Share this article
Shareable URL
Prev Post

Namna Ya Kuwa Bora Zaidi (Kuongeza Ubora Wa Kitu Unachofanya)10 Min Read

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Read next

Huruhusiwi ku copy. Asante.