You Can Win If You Want

Namna Ya Kuwa Bora Zaidi (Kuongeza Ubora Wa Kitu Unachofanya)10 Min Read

namna ya kuwa bora zaidi

Utangulizi

Kuwa bora zaidi (kuongeza ubora) maana yake ni kuwa na uwezo mkubwa wa kufanya kitu katika kiwango cha juu zaidi,

Kitu kinapofanyika katika kiwango cha juu zaidi maana yake huvutia watu wengi zaidi kwa ukubwa na hisia nzuri

Na kadiri kitu kinapo vutia watu wengi zaidi maana yake mafanikio ya kitu hiko pia huongezeka na kupanda juu zaidi.

Kuwa bora kwenye kitu unachofanya hupaswa kuwa jambo la kwanza kufikiriwa kabla ya mafanikio ya kipesa!

Pesa haikimbizwi, inategwa!

Ili kuweza kutega pesa katika mtego sahihi basi suala la ubora wa jambo haliepukiki na hupaswa kuzingatiwa

Watu wengi sana hususani vijana nchini Tanzania hukimbizana kutaka kuona mafanikio ya pesa kabla ya ubora wa kazi zao,

Mwisho wa siku hujikuta wakichoka sana na kuwa watumwa wa pesa pasi na kuona mafanikio ya kudumu kwenye mambo wanayofanya.

Wengi hufanya vitu kwa kubabaisha lengo kubwa ni kuingiza pesa mfukoni bila kujali pesa hio imeingiaje,

Mbaya zaidi hujiona wajanja wanapoingiza pesa bila kujali pesa ile itaendelea kuingia kwa urahisi au itahitaji nguvu kubwa kupata pesa nyingine wakati mwingine!

Maana yake ni kuwa pesa hupaswa kuingia kwa mtiririko wa kuvutana yenyewe kwa yenyewe na kadiri unapokuwa bora kwenye eneo lako,

Ndivyo pesa huvuta pesa (wateja huvuta wateja) na hata fursa huvuta fursa bila kutumia nguvu kubwa sana.

Yote hayo huja baada ya kujitoa muhanga wa kutafuta ubora wa kitu unachofanya kabla ya kukimbizana na pesa.

Mfano

Kabla hujataka mteja mwingine jiulize je ,mteja aliyepita umempa thamani itakayomfanya arudi kununua kwako?

Au umemuhudumia kwa namna ambayo atakimbia na kutafuta wauzaji wengine? (usijidanganye vaa viatu vya mteja wako)

namna ya kuongeza ubora
Photo by Anna Shvets on Pexels.com

Watu Hupaswa Kufuata Ndoto Zao Kabla Ya Pesa

Siku zote pesa hupaswa kufuata watu na hio ndio siri ya mafanikio ya kweli kwenye maisha ya mtu yoyote,

Watu ili wapate mafanikio ya kufuatwa na pesa basi hupaswa kufuata ndoto zao kwa ubora wa hali ya juu sana.

Haijalishi unafanya nini au una ndoto na malengo gani, inawezekana ni:

  • Taaluma fulani labda Daktari, mwalimu, muhasibu NK
  • Pengine ni ujuzi fulani labda kushona,kujenga NK
  • Au hata kipaji mfano unaimba,unaigiza NK
  • Na labda kwa ujumla ni biashara( kubwa au ndogo),

Ili kufurahia mafanikio basi lazima kupambana sana kufanya kwa ubora unachofanya au utakachotaka kufanya baadae.

Kuwa bora ni pamoja na kuleta thamani ya juu zaidi kwenye jambo unalofanya ili kuvutia thamani zaidi na zaidi

Kiwango cha thamani unacholeta ndio kiwango cha malipo na mafanikio utakayopata kwenye kitu unachofanya!

Thamani ikiwa kubwa basi na mafanikio (malipo) huwa makubwa na thamani ikiwa ndogo basi pia mafanikio huwa madogo

Hivyo basi kuleta thamani kubwa ya kitu na jambo ni lazima ufanye kwa ubora wa hali ya juu sana .

Hakuna Aliye Zaliwa Akiwa Bora

Najua kuna mtu unamuangalia kwa sasa na unatamani kuwa kama yeye ,pengine hata unadhani amepewa zawadi na Mungu

Elewa kuwa hata aliye juu au bora kiasi gani , Amejifunza kuwa bora!

Hakuna muujiza wa kuwa aina fulani ya mtu kama hutaamua kufanyia kazi na kuleta mabadiliko wewe binafsi.

Ukiamua unaweza sana na hata kumzidi huyo unae mtamani kwa sasa kwakua nyie wote ni Binaadamu sawa .

Kuna Watu Wana Elimu Kubwa Za Darasani Ila weupe Kichwani

Unaweza kuhisi kama utani hivi ila huu ni ukweli mchungu sana nchini Tanzania!

Elimu ya Tanzania ( Elimu ya mkoloni)mbali na kuandaa watu kuwa watumwa na tegemezi bado pia inaandaa watu watafuta vyeti.

Wengi husoma ili wapate vyeti na sio kuelimika au kuleta mabadiliko ya dhati nchini na jamii kwa ujumla kupitia taaluma zao,

Utakuta mtu ana Elimu kubwa sana au hata kaajiriwa sehemu kubwa ila kichwani mweupe sana na hata hajui kitu kabisa.

Mtu huyo anazingatia mshahara wake tu hata mambo yanayohusu sekta yake huwa kama mgeni mualikwa!

Unaweza kutaka huduma ofisi fulani unakuta muhudumu (mtumishi) wa hapo hana taarifa za kina hata za sekta yake!

Hawa ndio waliosoma kwa lengo la kupata vyeti ili waajiriwe tu na wengine ndio hupachikwa kazini kwa connetion za ndugu zao,

Asilimia ya watu wanaojua kwa kina kitu wanachofanya nchini Tanzania ni wachahe sana tena ni bahati sana kuwaona!

Na hayo ndio madhara ya Elimu yetu ambayo tunapaswa sana kupigania kuleta mabadiliko (No Reforms No Election 2025).

Kanuni 3 Za Kuongeza Ubora Zaidi

  • Elimika zaidi (soma na jifunze zaidi)
  • Fanyia kazi zaidi
  • Zoea zaidi

Elimika zaidi

Elimu haijawahi kuwa nyuma kwenye kuleta mabadiliko, unaweza kukimbia vyote vikakuacha ila ukikimbia Elimu basi nayo haitakuacha salama!

Unapotaka kuwa bora kwenye kitu chochote kile basi hatua ya kwanza na muhimu ni kukijua hiko kitu kwa undani zaidi,

Kadiri unavyokijua kitu ndio una Elimika na kukimudu zaidi haijalishi kina ukubwa kiasi gani bado Elimu ndio silaha kuu.

Hivyo anza kujielimisha kila wakati kuhusu jambo unalotaka kuwa bora zaidi na hakikisha una Elimika kwa undani sana

Zipo njia nyingi sana za kupata Elimu zaidi ,hapa haijalishi kwa kiwango gani tayari una Elimu kubwa juu ya jambo hilo.

Maisha Yanabadilika Kila Siku

Kila siku mambo mapya huzalishwa na kuingia kwenye maisha ya watu hivyo huwezi kubaki na Elimu ya jana kwenye maisha ya leo,

Kuna watu hawalali kila siku kuhakikisha wanaleta mabadiliko zaidi kwenye maeneo mbali mbali hapa Duniani

Hii maana yake ni kuwa bila kujali kiwango cha Elimu yako bado unapaswa kujifunza zaidi na zaidi kila mara ili kwenda sawa na mabadiliko.

Kuna njia nyingi sana za kujifunza ,Elimu hii haimaanishi kusoma Elimu rasmi ya darasani bali Elimu inayohusu jambo fulani moja kwa moja:

  • Ingia you tube jifunze jambo unalofanya zaidi
  • Soma vitabu vipya vinavyohusu jambo unalofanya
  • Uliza kwa wenzako wanaofanya jambo kama lako kwa ubora na kubali kusahihishwa
  • Fatilia taarifa mpya mitandaoni zinazohusu jambo au kitu unachofanya kila siku
  • Tafuta majarida na magazeti kuhusu jambo unalofanya mara kwa mara NK

Kwa ufupi ni kuwa hakikisha siku haipiti bila kujua au kujifunza kitu chochote kipya kuhusu jambo unalofanya

Tenga angalau nusu saa tu kwenye masaa 24 ya siku ili kujifunza vitu vipya vinavyohusu jambo unalofanya.

Kumbuka: Kadiri unavyo jifunza zaidi ndio unavyoingiza (utakavyoingiza) faida zaidi.

Fanyia Kazi Zaidi

Ili kuipa uhai Elimu unayojifunza basi lazima kuifanya kwa vitendo ndio utapata nafasi ya kuwa bora zaidi,

Fanya zaidi na zaidi haijalishi utalipwa au utafanya bure ( zingatia kufanya mara kwa mara) bila kujali unachoingiza.

Endelea kufanya mara kwa mara ili ujenge hali ya kukizoea na kukijua kwa undani kitu chako kupitia vitendo

Usilale na Elimu ndani ( ni sawa na kutwanga maji kwenye kinu)ingia nayo kwenye uhalisia na ifanyie kazi.

Haijalishi unapata matokeo mazuri au mabaya wewe endelea kufanya tu zaidi na zaidi kila mara na kila siku,

Fanya kwa namna tofauti tofauti na njia mbali mbali ili kupata ujuzi wa mbinu zote na mitindo yote inayohusu jambo lako,

Kiufupi usiridhike na mtokeo yoyote yale iwe mabaya au mazuri kitu cha kuzingatia ni kufanya zaidi tena na tena.

Kadiri Unavyo Fanyia Kazi Zaidi Ndivyo Utaongeza Ubora Zaidi

Asikudanganye mtu ,siku zote mtu mwenye uzoefu wa kitu ( jambo) maana yake amelifanyia sana kazi,

Huwezi kuwa mzoefu au tuseme ( pro) wa jambo fulani kama hujalifanya mara nyingi kwa njia mbali mbali na kulizoea zaidi.

Kwa maana hio fanya jambo lako kwa vitendo na lifanye sana zaidi na zaidi kama kichaa au kama umetumwa na kijiji.

Usiogope Kukosea

Kukosea ni hali ya kawaida sana kwa yoyote anaejifunza na siku zote tunajifunza kupitia makosa tunayofanya,

Hakuna ambae hakosei au hajawahi kukosea kamwe bali hupaswa kurekebisha makosa mara kwa mara.

Hivyo fanya masahihisho ya makosa yako kila wakati kabla ya kusonga mbele ili ujihakikishie wakati ujao hurudii kosa

Na kila unapokosea na kurekebisha makosa maana yake ndio huongeza nafasi ya kuwa bora zaidi kwa wakati ujao.

Zoea Zaidi

Baada ya kufanyia kazi zaidi na zaidi bado hupaswi kuacha na kupumzika bali unapaswa kuendelea kuzoea mara nyingi zaidi

Kadiri unavyo zoea ndivyo unakuwa bora zaidi na zaidi hivyo uzoefu hupatikana kwa kufanya sana jambo lil lile mara nyingi

Uzoefu pia ndio hufanya jambo kufanyika kwa ubora na kwa muda mfupi zaidi kulingana na kiwango cha uzoefu wa mtu

Hivyo basi kwa ujumla muda ndio silaha nyingine ya ubora ( subra na uvumilivu) hakuna uzoefu wa siku moja.

kuwa bora zaidi
Photo by JESHOOTS.com on Pexels.com

Hatua Za Kuwa Bora Zaidi

  1. Jua eneo au jambo unalotaka kuwa bora zaidi

    Lazima ujue nini unataka kwanza kabla ya kukurupuka kuchukua hatua na pia elewa sababu za kwanini unataka kuwa bora

  2. Changanua unachokiweza zaidi

    Hakuna aliye bora kwenye kila kitu, hivyo chagua eneo au kitu unachokiweza zaidi na kukifurahia sana

  3. Jiulize unataka kuona matokeo gani

    Kupitia hicho ulichokichagua ,je unataka baadae uone nini haswa kitakacho kufurahisha zaidi

  4. Weka mikakati

    Unahisi ukifanya nini sasa kinaweza kuleta mabadiliko na kukupa matokeo unayotaka?

  5. Zingatia kanuni 3 za ubora

    Kupitia mikakati yako unapaswa kujielimisha, kufanyia kazi na kisha kuzoea zaidi

  6. Fanya kwa hatua ndogo ndogo

    Usiwe na pupa utachoka haraka, ila kama unaweza kwenda mbio pia sio jambo baya kikubwa zingatia ubora

  7. Rekebisha makosa

    Kila wakati fanya thathmini ili uweze kugundua makosa yako kisha yarekebishe na endelea mbele

  8. Pima matokeo

    Unapaswa kupima matokeo unayopata kila baada ya muda fulani ili kujua kama unapata matokeo chanya au hasi

  9. Rudia mchakato tena na tena

    Haijalishi matokeo unayopata usiridhike wala kuacha bali endelea kuboresha kila wakati na kila siku ili kulinda au kuongeza matokeo yako.

  10. Jipe muda

    Muda ndio hutoa matokeo mazuri zaidi kwahio usijali endelea kufanya na acha muda uamue.

Kuongeza Ubora Zaidi Kwenye Kazi Unayofanya

Inawezekana kwa sasa umeajiriwa mahala haijalishi upo kitengo gani au unalipwa kiwango gani cha pesa

Ili kuongeza thamani zaidi na hata kulipwa zaidi basi lazima uwe bora zaidi ya hivyo ulivyo sasa ,

Ongeza thamani ya kazi unayofanya kila siku kwa kufuata maelekezo ya hapo juu bila kuangalia wengine.

Usiogope na kujiona umechelewa, anza sasa kuitafuta thamani yako na thamani ya kazi yako bila kuchoka na ,

Pindi ukikosa matokeo unayotaka, basi ongeza na fanya zaidi na ukipata matokeo unayotaka bado endelea kufanya!

  • Ukipanda cheo basi zingatia kuongeza ubora ili ulinde cheo chako
  • Ukishuka cheo ,fanya kwa ubora ili upande cheo tena
  • Ukichukiwa na bosi ,fanya kwa ubora zaidi kazi zako
  • Ukipendwa na bosi pia endelea kufanya kwa ubora ili akupende zaidi

Kwa ufupi ubora haupaswi kusimama bali kuzidishwa.

kuwa bora zaidi
Photo by The Lazy Artist Gallery on Pexels.com

Kuongeza Ubora Zaidi Kwenye Biashara

Haijalishi unafanya biashara ya aina gani wala haijalishi ni biashara ndogo au kubwa sana kwa sasa,

Kitu muhimu ni kuuza bidhaa au huduma yako kwa kuongeza ubora wa hali ya juu sana ili kulinda au kukuza baishara yako:

  • Ukipata wateja wengi basi ongeza ubora ili wateja waendelee kuja
  • Ukikosa wateja pia endelea kufanya kwa ubora ili wateja waje

Elewa kuna wafanya biashara wenzako hawalali wanawaza namna ya kupata wateja wako zaidi na zaidi

Wanabuni mbinu za kutawala na kuteka soko hivyo ukilegeza kidogo tu thamani ya biashara yako ikishuka,

Tayari ni mwanya kwao kupata wateja wako na kukushusha kabisa.

Zingatia

  • Usile pesa ya mteja kama huwezi kumfanya mteja huyo abaki kuwa mteja wako daima kupitia thamani unayompa
  • Usitangulize tamaa ya pesa mbele kabla ya ubora wa biashara yako ( kadiri unavyoonesha ubora ndio wateja huvutana)

Kujua zaidi namna ya kuongeza ubora kwenye kazi na biashara yako basi wasiliana nasi sasa kwa ushauri wa kina zaidi.

Hitimisho

Maisha yana machaguo mengi sana hivyo kwa kadiri unavyoleta uchovu basi hutafutwa mbadala wako,

Kumbuka Dunia haitosimama ukigoma kwenda nayo (watu wanaofanya kitu kama chako ni wengi sana).

Usiwe mtu unaependa kulalamika pale unapoona mambo hayaendi bali zingatia kuongeza ubora na thamani kwanza,

Hakuna mteja au mtu asiyetaka vitu vizuri anapotoa pesa yake ,hivyo weka sumaku ya kunasa wateja au watu zaidi kwako,

Na sumaku yenyewe ni ubora kwanza ( hata ukichelewa kuonekana kama unafanya kitu kizuri basi muda utafika tu)

Ni bora uchelewe kupata faida ila uwe unafanya kwa ubora mkubwa kuliko kuwahi kisha kuanguka chini.

Share this article
Shareable URL
Prev Post

Wazo La Biashara Ya Chips7 Min Read

Next Post

Namna Ya Kuongeza Ubora Wa Maisha Kwa Kipato Kidogo14 Min Read

Comments 3
  1. credited his charitable spirit to his education [url=www.en.wikipedia.org/wiki/Chuck_Feeney]www.en.wikipedia.org/wiki/Chuck_Feeney[/url] .

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Read next

Huruhusiwi ku copy. Asante.