Wafanyakazi wa majumbani ni biashara yenye uhitaji mkubwa sana kwa nchi kama Tanzania,
Wafanyakazi wa majumbani wanahitajika sana katika kusaidia shughuli mbalimbali ndani ya nyumba
Kama usafi wa mazingira, usafi wa nguo, kuandaa chakula, kulea watoto nk
Watu wengi wamekwama katika kufanya shughuli za maendeleo ya kiuchumi na kijamii
kutokana na kukosekana kwa wafanyakazi waaminifu wa kusaidia shughuli za nyumbani na watoto
Familia nyingi zinatamani kupata wafanyakazi waaminifu wenye kujua majukumu yao bila msukumo wowote
Wafanyakazi wengi wa majumbani hawajui majukumu yao na,
Wengi hufanya kazi hii kama chaguo la mwisho wanapokosa kitu cha kufanya na ugumu wa maisha Ila sio kwa kupenda
Tanzania haina kampuni kubwa yenye kuendesha biashara hii ya wafanyakazi wa majumbani kwa uyakinifu mzuri
Faida za wafanyakazi ni nyingi katika kuleta na kukuza uchumi wa nchi
Kwani kina mama wengi wamekwama kufanya shughuli za maendeleo kwa kukosa watu wa kuwaangalizia familia zao,
Pia faida kama kuleta amani za ndoa kwa kusaidia kina mama shughuli nyingi na kuwapa ahueni kutekeleza mambo mengine ya kifamilia.
Changamoto zilizopo katika sekta ya wafanyakazi wa kazi za ndani
- wafanyakazi kutojua majukumu yao
- wafanyakazi kutopenda kazi zao
- Mtazamo hasi kutoka kwa jamii (dharau)
- Maslahi duni kwa wafanyakazi
- Tabia na historia za wafanyakazi na wateja (mabosi)
- Imani za kishikirikina
- wizi, Utapeli na ujambazi
- Kusahaulika kwa sekta ya wafanyakazi wa majumbani katika serikali na mamlaka husika.
Wafanyakazi kutojua majukumu yao
Wafanyakazi wengi sana hawajui hata nini hupaswa kufanya wanapokuwa eneo la kazi,
hii hufanya mfanyakazi kufanya kazi kwa kusukumwa na kulazimishwa au hata
Kufanya kazi kama vile anaonewa na kuteseka wakati ni majukumu yake na analipwa mshahara
Wengi wao wanataka kuishi kama vile wapo nyumbani kwao,
Wakati pale ni eneo la kazi na jukumu lao kubwa ni kufuata sheria, kanuni na taratibu za kazi husika /familia husika
Wafanyakazi kutopenda kazi zao
Asilimia kubwa ya wafanyakazi wa majumbani hawapendi kabisa kazi hio,
Hufanya sababu za ugumu wa maisha na kwakuwa hawana mbadala wa kazi nyingine,
Huichukulia kazi ya ndani kama sehemu ya kukimbilia wanapokosa kabisa njia ya kuishi,
Ndio maana imefanya kazi zao kuwa kama adhabu na kutofurahia kabisa wanachofanya na kufanya kwa kujivuta vuta
Mtazamo hasi kutoka kwa jamiii
Asilimia kubwa ya watu huidharau sana kazi ya ndani na kudharau mtu anaefanya kazi ya ndani
Kwa kumuona kama mtu asiye na akili timamu, masikini sana, hana maisha mengine, mtumwa, na hata mtu asiye kabisa na maana katika jamii
Hali hio imepelekea hata wafanyakazi wenyewe kujidharau na kujiona viumbe ambao hawana thamani yoyote kwa mabosi zao
Hivo kujenga chuki kwenye mioyo hata kama hawajatendewa ubaya
Maslahi duni ya wafanyakazi
Mishahara midogo wanayolipwa wafanyakazi huku wakifanya kazi nyingi sana kupita uwezo wao
kukosa ruhusa za kutembelea familia zao na mapumziko,
Kufanya kazi kwa masaa mengi zaidi, kukosa malipo ya NSFF na bima za afya
Imefanya sekta ya hii kuwa sekta chungu zaidi kwa wafanyakazi husika
Tabia na historia za wafanyakazi na wateja
Kila mmoja ana tabia yake, kuna wengine wana roho mbaya, chuki, husda, uasherati na tabia zingine
Hivo kuishi ndani ya familia ambayo pia ina tabia zake zingine ni changamoto kubwa zaidi,
Maana kubadilisha tabia aliyozoea mtu ni kazi kubwa sana matokeo yake tunapata Matukio kama “Vifo vya watoto” wanaouliwa na wafanyakazi wa ndani,
Mabosi wa kiume kuwa taka wafanyakazi wao na changamoto za ndoa kuibua nk
Imani za kishirikina na mila potofu
Kuna wafanyakazi wengi ambao hutokea vijijini, huja wakiwa na vifaa vyao vya kishirikina kwa lengo la kujibu mashambuliza watakayopitia
wengi huamini katika uchawi na kujaribu kufanya mambo kutimiza maagano yao au hata kujaribu kuwafanya mabosi kuwa chini yao.
Sasa hapa Ndio hutokea mabosi na familia kulishwa vitu vingi vya ajabu,
Kutumikishwa kichawi nyakati za usiku, ugomvi wa familia husika, Vifo visivyo vya kawaida nk
Wizi, Utapeli na ujambazi
Wateja wengi wametapeliwa na watu wanao waahidi kuwatafutia wafanyakazi na kisha kuchukua pesa na kutokomea
Au kuleta mfanyakazi na kumuondoa baada ya siku chache kwa siri kisha kumpeleka sehemu nyingine na kutapeli wateja wengine
Lakini pia wafanyakazi wengi huwaibia wateja na hata hutumika na majambazi kurahisisha wizi mkubwa ndani ya nyumba
Kusahaulika kwa sekta ya kazi za ndani kutoka kwa mamlaka husika na serikali
Moja kati ya sekta ambayo ina umuhimu mkubwa sana lakini haifatiliwi kabisa ni sekta hii
Hakuna chombo maalumu cha kutetea haki na sheria za wafanyakazi na waajiri
katika mifumo sahihi kama kupatiwa haki na stahiki zao, kupewa mikataba ya kazi, kutetewa na kusimamiwa haki zao nk
Changamoto za biashara ya wafanyakazi wa ndani na jinsi ya kuzikabili
wafanyakazi kutotulia kazini
Wengi sana hutoroka, hukatisha mikataba na hata kuacha kazi wanapojisikia, hii huleta usumbufu kwa wateja,
Sasa hapo lazima uweke mkataba mkali sana kuhakikisha kuwa mfanyakazi anakaa kazini mpaka muda wake wa mkataba kuisha
Wafanyakazi kuiba
Hapa ni changamoto nyingine wengi huiba Mali za wateja na kukimbia na
Usipokuwa makini mteja huja kukukamata wewe maana wewe Ndio una dhamana ya mfanyakazi
Hakikisha kuwa una utambulisho husika wa wafanyakazi wote, mahala wanapotokea na udhamini kutoka kwa watu wake wa karibu
Wafanyakazi kuua na kupiga watoto
Hapa kuna kesi nyingi sana tunazishuhudia kwa wafanyakazi kuua watoto au mabosi zao kutokana na sababu mbalimbali
Unapaswa kuwa na uhakika wa kila mfanyakazi, anapotoka na fatilia historia yake vizuri ili uwe na,
Dhamana na uhakika wa mfanyakazi, kamwe usichukue au kuamini mfanyakazi yoyote na kumpeleka kwa mteja bila kujiridhisha
Wafanyakazi kutolipwa kwa wakati na changamoto za unyanyasaji
Kuna mabosi wakorofi na hawana utu, wanapenda kutesa, kubaka, kudhalilisha wafanyakazi wao
Wakati mwingine hata kuwanyima pesa za malipo kwa wakati na chakula,
Unapaswa kuwa mkali na hakikisha mkataba wako upo wazi na unajieleza vema sheria zote za kampuni
Hakikisha una vibali halali vitakusaidia kumshitaki kila mteja anaeenda kinyume na wafanyakazi wako
Na itapendeza mishahara iwe inapitia chini ya kampuni na wewe ndio unaewalipa wafanyakazi wako
Wateja kuwafanyisha kazi nyingine wafanyakazi nje ya kazi za ndani na kuwatumia kwa malengo tofauti
Hakikisha mkataba umeeleza mambo yote muhimu na kukataza mambo yote yasiyotakiwa na hakikisha unapajua mahala unapopeleka wafanyakazi kufanya kazi, yani lazima upajue nyumbani kwa mteja wako.
Namna ya kupata wafanyakazi
- Mitandaoni kama Facebook
- Vijijini
- Wahitimu wa shule na vyuo mbalimbali
- Mawakala wadogo wadogo wa mikoani
- Mitaani hasa wale wanaofanya kazi migahawa, ongea nao wape faida za kufanya kazi chini ya kampuni yako.
Namna ya kupata wateja
- Mitandaoni kama Instagram
- Maofisini
- Mitaani hasa maeneo ya watu wenye uwezo
- Sehemu za ibada kama kanisani nk
Jambo la msingi ni kuwa na kadi za biashara na kuzisambaza maeneo mbalimbali, uzuri biashara hii inajiuza yenyewe na utapata shida miezi ya mwanzo tu.
Ushuhuda kutoka kwangu
Nimewahi kuwa na kampuni ya wafanyakazi wa kazi za ndani iliyoitwa “Muhasu Domestic helpers agent company limited”
lakini nilisitisha kutokana na changamoto zilizokuwa nje ya uwezo wangu kwa wakati ule,
Hivyo naongea kitu ambacho nina kifahamu vyema na nina uhakika nacho kwa asilimia zote.
Namna ya kuandaa wazo wa biashara ya wafanyakazi wa ndani
Chunguza familia chache za karibu yako na utagundua uhitaji uliopo na changamoto zao,
Wewe binafsi kama tayari una familia yako utagundua umuhimu wa kuwa na mfanyakazi wa ndani,
Angalia wakina mama walio ajiriwa au kujiajiri maeneo mbalimbali utagundua wanahitaji wafanyakazi ili waweze kufanya shughuli zao kwa amani
Andaa wazo lako lakini hakikisha kuwa limejikita kuleta suluhu zaidi na kuondoa changamoto zote za wateja na wafanyakazi kwanza kabla ya kuwaza faida
Kwasababu pesa katika sekta hii zipo nyingi sana, wateja ni wengi sana na hata waajiriwa wanaweza kuwa wasomi ambao bado hawajapata kazi,kama tu utaweka maslahi mazuri kwa wote
Sekta hii haina upinzani na bado ina soko na fursa kubwa sana.
Namna Ya kuanza biashara ya wafanyakazi wa ndani kwa wenye mitaji
Kama una mtaji wa kutosha angalau milioni 2 mpaka 3, na kama umejipanga na kudhamiria kufanya biashara hii basi fanya hivi:
- Sajili kampuni, fatilia vibali kama Tax clearance, leseni, na vibali vingine,Tafuta ofisi yenye eneo la kutosha nje au ndani, weka thamani zote unazotaka
- Fatilia kuhusu utaratibu wa bima za afya kwa wafanyakazi na NSSF (hii hata kwa baadae sio lazima mapema)
- Andaa mikataba ya wafanyakazi na wateja (mabosi zao) hapa andika kila kitu ili kuweka maslahi baina yao wote wawili na kampuni
- Fafuta sare za wafanyakazi inaweza kuwa magauni, tisheti au nguo zozote kikubwa ziwe ambazo atavaa eneo la kazi
- Tafuta wafanyakazi kadhaa wa kuanza nao, wape Semina na Elimu ya kutosha, wafundishe majukumu yao na Elimu zote kuhusu kazi na nini wanapaswa kufanya kwa namna unayotaka wewe (sio lazima utoe wafanyakazi mbali kama Huna mahala pa kuwalaza na vibali, Anza na walipo karibu
- Weka mishahara mizuri kwa wafanyakazi angalau mshahara wa chini uanze laki moja
- Jitangaze na weka matangazo yako sehemu mbali mbali kama Instagram, na hakikisha matangazo yanavutia mteja na kushawishi.
Namna Ya kupata faida kwenye biashara ya wafanyakazi wa majumbani
Huu ni mfano tu lakini unaweza kutengeneza faida yako kulingana na taratibu zako, eneo unalofanyia na gharama za uendeshaji pia vile unataka wewe
Mwanzo kabisa usitegemee faida kubwa sana Anza na kuweka mambo Sawa na Uaminifu kwa wafanyakazi na wateja
- Mteja alipie pesa za awali za kutafutiwa mfanyakazi, hii itategemea na gharama zako unazotumia kugharamia wafanyakazi wako mfano Laki moja kwa kila mfanyakazi
- Wakate wafanyakazi pesa za vitambulisho vya kazi, fomu za kujiunga na ikiwezekana idadi ikiwa kubwa sare za kazi
- kila mfanyakazi atakae kuwa chini ya kampuni atakatwa asilimia kidogo kwa kila mshahara kila mwezi labda elfu 5 au 10
- mfanyakazi yoyote anaekwenda kinyume na sheria za kazi au atakae vunja mkataba alipe pesa za mshahara wa mwezi mmoja
- mteja anaetaka kukatisha mkataba kwa sababu zake anapaswa kulipa kiasi fulani cha usumbufu
Namna Ya kufanya biashara ya wafanyakazi kama Huna mtaji
Kama Huna pesa za vibali na usajili changamoto ni kubwa sana na inaweza kukuweka hatarini zaidi
Maana wafanyakazi wengi wa ndani kwa sasa ni mtihani mzito na hawana uhakika wa kutofanya Matukio mabaya kazini kwao
Hivyo lazima itakupa hatari ya kesi mbalimbali na kuharibu jina lako kwa Wateja wako
Ila unaweza kuanza kwa watu wa karibu yako unao wafahamu vyema ili kupunguza changamoto:
- Unganishia watu kazi hasa wale unaowajua mpaka nyumbani kwao na tabia zao kwa ujumla ili ikitokea shida kwakua Huna vibali itakuwa rahisi kupata Msaada na mahala pa kuanzia
- Unaweza kuanza biashara hii hata kama Huna hata shillingi moja, kikubwa uwe na simu, wafanyakazi unaowajua na wateja basi
- Fungua akaunti za mitandao kama Instagram na Facebook na anza matangazo yako
- Ipe biashara yako jina lolote unalotaka na ambalo utatumia kusajili baadae
- Wape mafunzo wafanya kazi utakaopata kwa kuanzia mambo yote muhimu kama usafi na heshima
- Panga bei za wateja, mishahara na kila kitu kama nilivyo elekezeka hapo juu kwa wale wenye mitaji, tofauti tu kuna vitu kama sare, bima nssf nk sio lazima kwakua Huna pesa
- Kuwa makini, fatilia wafanyakazi mara kwa mara na wateja ili kugundua kama kuna tofauti yoyote inayoendelea na uweze kuweka Sawa mapema
Taratibu pesa unazopata Anza usajili haraka wa biashara na vibali kwanza kisha endelea na biashara yako mpaka itakapokuwa kubwa. Unaweza kuanza biashara yoyote bila mtaji.
Mambo ya kuzingatia katika biashara ya wafanyakazi wa ndani.
- Fatilia wafanyakazi na wateja mara kwa mara upate mrejesho wao ili ujue kama kuna shida na uweke Sawa mapema
- Simama katika haki na usiendeshwe na tamaa ukasahau haki za wafanyakazi na wateja
- Uaminifu wako na wateja, ikiwa kuna changamoto yoyote haraka badilisha mfanyakazi na ikiwa mfanyakazi ana changamoto mbadilishie nyumba
- Haki za kupata mapumziko wafanyakazi ni muhimu na lazima angalau kwa mwezi mara moja au kila wiki kwa masaa kadhaa
- Epuka kuamini mfanyakazi yoyote hata kama kaja analia, kama hana utambulisho au hajatimiza nyaraka zake za kusajiliwa usimpe ajira kamwe yani hapa roho ya huruma na tamaa za pesa zisikuponze kabisa
- Weka mishahara mizuri yenye maslahi kuvutia wafanyakazi
- Weka maslahi mengine ya ziada kufanya wafanyakazi wavutiwe na kuona umuhimu wa kuwa chini ya kampuni yako
- Hakikisha unawapa mafunzo wafanyakazi hasa kuhusu majukumu yao ya kazi, usafi wao binafsi, namna ya kuipenda kazi na heshima.
Hitimisho
Kazi za ndani zinaweza kuleta ajira nyingi sana kwa watu wengi na kusaidia vijana kupata mitaji kwa kuweka maslahi mazuri na kuipa hadhi kazi hii,
Nchi zilizoendelea zina heshimu sana wafanyakazi wa ndani na hulipwa mishahara mizuri na stahiki zao zote kama wafanyakazi wengine
Lakini pia Biashara ya wafanyakazi wa ndani inataka uvumilivu mkubwa, hekima na busara sana katika kutatua changamoto za wafanyakazi na wateja. Kama una hasira za karibu bora usianze biashara hii.
Comments 1