You Can Win If You Want

Jinsi Ya Kupanga Bajeti Ya Biashara6 Min Read

jinsi ya kupanga bajeti ya biashara

Utangulizi

Bajeti ya biashara kama ilivyo kwenye bajeti binafsi ya matumizi kwa mtu ,ni muhimu sana ili kupata ustawi bora wa biashara

Biashara yoyote ile ili iweze kukua na kufikia mafanikio makubwa, suala la bajeti nzuri haliepukiki kabisa

Bila kujali biashara inahusu kutoa huduma au kuuza bidhaa, iwe jumla au reja reja bado bajeti ni muhimu sana kuwepo

Kwani bajeti ndio huipa biashara ustawi na ukuaji mzuri zaidi kuanzia eneo la mapato mpaka matumizi ya biashara.

Lengo kubwa la mfanyabiashara yoyote huwa kuongeza mzunguko wa pesa na faida kwenye biashara yake

Hivyo kuweza kufikia lengo hilo ni lazima kuzingatia bajeti nzuri ya biashara husika kwenye maeneo yote ya Fedha

Kumbuka sio lazima kuwa na Elimu ya darasani ili kupanga bajeti ya biashara yako hata kama ni biashara kubwa au ndogo

Pia soma kwa kubonyeza link hii namna ya kupanga bajeti ya matumizi binafsi.

Biashara Nyingi Hufa Kwa Kukosa Bajeti Nzuri

Moja kati ya sababu kubwa zaidi ya biashara kufa au kuanguka ni suala la ukosefu wa bajeti nzuri na mzunguko wa fedha

Wafanyabiashara wengi hufanya biashara zao kwa mazoea na kutozingatia thamani ya utunzaji wa bajeti

Asilimia kubwa huchanganya biashara na maisha binafsi na hii hupelekea wengi kukosa muelekeo mzuri

Bajeti ya biashara hupaswa kuheshimika na kutofautishwa na bajeti ya maisha na matumizi binafsi

Haifai kabisa kwa namna yoyote ile kuweka mazoea kwenye biashara na maisha nje ya biashara

Kuna watu huona biashara zao kama sehemu za mizaha au mahala pa kuponea shida zao hasa zile za haraka

Kwa maana kuwa haoni shida kabisa kupunguza pesa za biashara na kufanyia mambo yasiyo na msingi wowote nje ya biashara

Ndio maana wengi huwaona WAHINDI na WACHAGA kama wabahili sana lakini ndio watu wenye mafanikio zaidi ya biashara Tanzania,

Kutokana na kutokuwa na mzaha kabisa kweye biashara zao na bajeti zao au hata malengo ya maisha kwa ujumla.

kupanga bajeti ya biashara
Photo by Nataliya Vaitkevich on Pexels.com

Faida Za Kupanga Bajeti Ya Biashara

Kupanga bajeti ya biashara ni muhimu sana hasa ukizingatia faida zake kama zifuatazo:

  • Huipa biashara ustawi mzuri , biashara inahitaji pesa ili kuweza kujiendesha vema zaidi kupitia bajeti yake
  • Husaidia kukuza biashara kwa mafanikio, bajeti nzuri ya biashara ni kiini kikubwa zaidi hasa katika ukuaji wa biashara husika haijalishi ni biashara ndogo au kubwa
  • Hondoa au kuepusha hatari ya kufirisika kwani husaidia kujua namna ya kupanga matumizi ,kutenganisha matumizi na kusimamia matumizi kwa usahihi
  • Husaidia kufikia malengo ya biashara kwa urahisi na uhakika zaidi
  • Husaidia kupata wawekezaji wengi na wazuri zaidi hasa biashara inapokuwa kubwa
  • Ni silaha katika kufanya maamuzi na kuweka mipango ya baadae kwenye biashara
  • Hurahisisha zaidi katika ufuatiliaji wa ukuaji wa biashara kwa urahisi na uhakika
  • Husaidia zaidi katika utunzaji wa pesa za biashara na kujua kwa undani namna ya kutunza na kuhifadhi faida na matumizi au hata mapato wa ujumla .NK

Mali Bila Daftari Huisha Bila Habari

Wahenga hawakukosea kabisa waliposema msemo huu, ukweli ni kuwa ni lazima na muhimu kuwa na bajeti

Tena kwa njia ya kutunza kumbukumbu bila kujali zitatunzwaje iwe kwa maandishi ,kichwani na hata vifaa vya kisasa

Ili kuwa na mafanikio hasa katika biashara suala la bajeti na kumbukumbu za mauzo au mapato halikwepeki kabisa

Mzunguko mzima wa pesa za biashara ni lazima kuhifadhiwa ili kuweka sawa marejeo ya kumbukumbu nzuri

Hivyo basi ni vema sana kuwa makini zaidi hasa kwenye masuala yote yanayohusu pesa za biashara iwe kubwa au ndogo.

Hatua Za Kupanga Bajeti Ya Biashara

  1. Weka malengo ya biashara yako

    Ili kuwa na bajeti nzuri ni lazima kuwa na malengo ya biashara kwanza yanayotoa dira ya biashara husika

  2. Elewa kwa kina mzunguko wa pesa za biashara

    Hapa ni lazima kujua pesa zote zinazotoka na kuingia, kuanzia mapato, matumizi na faida kwa ujumla

  3. Tenganisha mapato na matumizi

    Ili kuwa na kumbukumbu nzuri ni lazima pesa za mapato zijulikane na zile za matumizi pia zijulikane kwa uwazi

  4. Weka hesabu zote za mapato na matumizi za mwaka na mwezi

    Ili kupata mrejesho mzuri ni vema kujua mapato ya mwezi na mwaka kwa undani ili kupata uhakika wa bajeti nzuri

  5. Orodhesha mahitaji yote ya biashara kwa biadhaa moja moja

    Kila bidhaa hupaswa kujitegemea ili kujua bidhaa ipi ina mzunguko mzuri na ipi haina kwa lengo la kujua kipi zaidi kinapaswa kuzingatiwa

  6. Jumlisha mapato ya bidhaa zote zilizopo kwa mwaka na mwezi

    Hii husaidia kupata wastani mzuri wa mapato kwa biashara nzima kwa mwaka na mwezi

  7. Jumlisha matumizi yote ya mwaka na mwezi

    Hapa hupaswi kuacha hata yale matumizi madogo sana kwani ndio njia nzuri zaidi kujua wapi pesa zinatumika zaidi

  8. Toa jumla ya matumizi kwenye mapato kwa mwaka na mwezi

    Sasa chukua mapato yako kisha toa jumla ya matumizi yote kwa mwezi na mwaka na angalia kiasi kinachobaki ndio faida yako

  9. Rudia mchakato

    Mpaka kufikia hapo utapa picha halisi ya bajeti yako ,kama pesa za matumizi ni nyingi kuliko mapato rahisisha mahitaji ya biashara na tafuta namna ya kupunguza matumizi.

    Siri Za Kuwa Na Bajeti Nzuri Ya Biashara (Kupunguza na kubana matumizi)

    1. Kuomba punguzo la bei kwa wauzaji wa jumla na kukubaliana kabla ya kununua
    2. Kutafuta machimbo ya bei rahisi zaidi kwenye manunuzi ya vitu vyote vya biashara
    3. Kununua vitu kwa bei ya jumla hata kama ni vile vya matumizi ya kawaida ambavyo sio bidhaa za kuuza
    4. Kuajiri wafanyakazi wa gharama nafuu hususani wale ambao bado hawana uzoefu mkubwa kwenye soko la ajira kwani huwa na mishahara nafuu
    5. Kuto ajiri idadi kubwa sana ya wafanyakazi hasa wale wenye elimu kubwa zaidi na kama hakuna ulazima wa wafanyakazi bora kufanya kazi mwenyewe kwenye biashara hasa ikiwa changa
    6. Kutangaza matangazo ya bei nafuu au bure kabisa kuliko yale yanayohitaji pesa nyingi, kuna njia nyingi sana za kutangaza biashara kwa gharama nafuu zaidi
    7. Kutochanganya matumizi binafsi na yale ya biashara hata kama ni biashara ndogo sana
    8. Kuondoa kabisa matumizi yasiyo ya lazima kwenye biashara hasa yale yasiyo ingiza faida
    9. Kununua vifaa na vitu vinavyodumu muda mrefu zaidi
    10. Kurudisha asilimia kadhaa ya faida kwenye mzunguko wa biashara mara kwa mara ili kukuza biashara haraka
    11. Kutochukua mikopo isiyo na lazima kukuza biashara au kuchukua mikopo ya riba nafuu kama italazimika

    Mambo Ya Kuzingatia Ili Kufanikiwa Kwenye Kupanga Bajeti Ya Biashara

    • Kuhusisha malengo ya biashara ya muda mrefu na muda mfupi, pia soma hapa kujua namna ya kupanga malengo ya biashara
    • Kuwa na msimamo na moyo mgumu sana hasa kwenye matumizi
    • Nidhamu ya hali ya juu kwenye matumizi ya fedha zinaoingia na kutoka kwenye biashara
    • Kurikodi na kuandika kila mapato na matumizi kila wakati hata kama ni pesa ndogo ndogo au kubwa (mali bila daftari, huisha bila habari)
    • Kutofautisha kati ya mahitaji ya lazima na mahitaji yasiyo ya lazima mara kwa mara
    • Kusubiri faida ndio itumike kufanya matumizi binafsi na kutotumia mapato nje ya matumizi ya biashara
    • Kufuatilia mienendo ya wafanyakazi mara kwa mara kwa siri ili kujiridhisha na matumizi sahihi ya rasilimali za biashara
    • Kuajiri wafanyakazi waadilifu na wenye nidhamu ya matumizi.
    bajeti ya biashara
    Photo by Tima Miroshnichenko on Pexels.com

    Hitimisho

    Bajeti ya biashara ni rahisi sana na wala haihitaji elimu yoyote kuweza kufanikisha hilo kwa kiwango kizuri

    Kuna watu hawajasoma kabisa lakini linapokuja suala la bajeti za biashara zao huwazidi hata wale waliosoma sana

    Pia wapo ambo hawajui kabisa kusoma wala kuandika lakini wapo makini sana kufuatilia mfumo mzima wa bajeti za biashara zao

    Kwahio ni muhimu sana kuwa na bajeti nzuri ya biashara ili kusaidia kukuza faida na mzunguko mzuri wa biashara.

    Share this article
    Shareable URL
    Prev Post

    Namna Sahihi Ya Kupanga Bajeti Ya Matumizi14 Min Read

    Next Post

    Namna Ya Kuweka Mipaka Binafsi Ya Maisha6 Min Read

    Leave a Reply

    Your email address will not be published. Required fields are marked *

    Read next

    Huruhusiwi ku copy. Asante.