Kujiajiri kupitia taaluma yako ni kitu cha msingi na kitu kinachowatesa watu wengi sana kwani wanamaliza masomo wakiwa na matumaini ya ajira
Duniani changamoto ya ajira limekuwa tatizo kubwa sana , japokuwa kuna baadhi ya nchi angalau kuna unafuu wa upatikanaji ajira, suluhisho ni kujiajiri kupitia taaluma yako
Tanzania ni moja kati ya nchi zenye uhaba mkubwa wa ajira serikalini na sekta binafsi,
kuna baadhi ya vigezo nje ya taaluma yako kama ukivikosa basi sahau kabisa kitu kinaitwa ajira.

- Mfano Konekshi ya watu mbalimbali mbali hasa viongozi, nimeshuhudia watu wengi ambao hawana GPA kubwa wakiajiriwa kwakua tu wana ndugu zao katika uongozi wa juu
- Rushwa hasa ya pesa, maana Rushwa ya ngono kwa maisha ya sasa ni kama haina nguvu kubwa sana hivo usijisumbue hata kuwaza kutoa ngono upate kazi na pia kama Huna pesa za kuhonga nyingi sahau ajira na wakati mwingine unaweza kutoa pesa na usipate ajira
Inaumiza sana kuteseka zaidi ya miaka 16 kusoma, umepoteza muda mwingi na pesa nyingi
Halafu unahitimu unakosa ajira, hakuna namna zaidi ya kujiajiri kupitia taaluma yako tu
Lakini pia ukosefu wa ajira umesababishwa na mambo mengine kama vile
- Kuongeza kwa idadi ya wahitimu na kusababishia ushindani mkubwa katika soko la ajira , miaka ya nyuma wahitimu wa fani mbalimbali walikuwa wachache sana hivo nafasi za ajira zilihitaji watu wengi lakini sasa idadi ni kubwa kuliko hata uhitaji wa ajira zenyewe
- Ukosefu wa viongozi yenye weledi na ubinafsi wa viongozi hivyo kupelekea hata maeneo yanayohitaji wataalamu kushindwa kufikisha kwasababu ya weledi wa kazi na matumizi ya mabaya ya pesa za umma, kuna shule nyingi zina uhaba wa walimu na walimu waliohitimu wapo wengi mtaani lakini serikali inasema haina pesa za kutosha! Ila wanazidi kujilimbikizia Mali
Hivyo ukiwa kijana ambae umemaliza chuo, mtoto wa masikini,
Huna yoyote unaemjua kwenye uongozi wa juu na Huna muelekeo wala uhakika wa ajira
usipoteze muda wako mwingi kuhangaika na utafutaji wa ajira! Jiajiri kupitia taaluma yako
Tafuta ajira huku unajiajiri
Sisemi usitafute ajira ya ndoto zako lakini najaribu kukuepusha na upotezaji muda na majuto baadae
Kutumia miaka 3 au 5 kutafuta ajira huku ukiwa huna uhakika wa maisha yako ya mbele
Naona kama sio kitu chenye afya sana, ukizingatia umri haurudi nyuma
Hivyo tenga muda wako vizuri ikiwezekana hata kabla hujatoka chuoni “jua nini unataka kufanya mtaani nje ya ajira rasmi “
Yani lazima uwe na wazo la kukuingizia pesa iwe utaajiriwa au hutoajiriwa Ila ndani ya taaluma yako
Na wazo litafute ukiwa bado chuoni na endapo umeshahitimu basi anza muda huu
Waza kitu cha kufanya nje ya ajira kupitia taaluma uliyosomea na elimu uliyoipata
Mtaani kuna pesa nyingi sana tafuta nyavu yako na uzitege!
Mimi ninaamini kuwa nchi kama Tanzania fursa bado nyingi na kila mmoja anauwezo wa kuchukua fursa yake na akaingiza pesa nyingi kikubwa ni DHAMIRA NA IMANI
Mfano umesoma sheria jiulize hapo mtaani unapokaa raia wangapi wanajua haki zao! Utagundua hakuna na kama wapo haizidi asilimia 1%!
Sasa jiulize kuna wanasheria wangapi wanahitimu kila mwaka vyuoni lakini hakuna mafanikio ya moja kwa moja kupitia Elimu zao kwa jamii?
Haya na wewe leo hii umemaliza sheria Ila unangoja kuwa wakili wa serikali! Kuna mahakama ngapi hapa Tanzania?
Zipo sekta binafsi ngapi hapa Tanzania? Na kuna wahitimu wangapi wanaziangalia hizo sekta na mahakama!
Huna pesa mfukoni Ila una elimu ya sheria! Huna pesa Ila una wateja ambao Ndio hao hao raia wa mtaani wamejaa wengi sana
Sasa badala ya kusubiri ajira kwanini usitumie Elimu yako kupata pesa? Biashara sio mtaji
Chagua kipengele kimoja tu chenye uhitaji mkubwa labda ndoa, fundisha kina mama na kina baba sheria za ndoa,
Au sheria za mirathi (watu wana kufa kila siku), sijui sheria za kazi nk
Jiulize kuna single mother wangapi wanatesa na watoto kwa kutojua tu sheria na haki zao kwa wazazi wenzao?
Kuna wa mama wangapi wanateseka na ndoa kwa kutojua tu sheria za ndoa na haki zao?
Kuna wafanyakazi wangapi iwe viwandani au sekta ndogo ndogo wanateseka kwa kutojua haki zao?
Tatua changamoto za jamii moja kwa moja kwa kupitia taaluma yako
Hebu mimi na wewe tujiulize kuna migogoro mingapi ya ardhi kila kukicha! Watu hawajui hatua za kufuata kununua na kulinda ardhi zao!
Lakini wasomi na wataalamu wa ardhi wapo mtaani wanangoja ajira za serikalini
Chagua eneo moja tu ulilosomea na unaloliweza sana kisha jifunze mbinu za kuuza (sales) kupitia vitabu kama sales like crazy uteke wateja
Pia kuna channel kama YouTube kuna video nyingi zina fundisha mbinu za kuuza na kupata wateja
Kwa kuanza anza mtaani kwako, tumia simu yako, na usifirikie faida kwanza
Ila jenga uaminifu na fanya watu waone faida ya unachowasaidia
Umesoma sijui human rights au human resources? Itumie mtaani kwako! Saidia watu wako kwanza wakati unasubiri hizo ajira hewa!
Umesoma Accountant, au labda economics, sijui marketing kwanini sasa huitumii mtanii kwenu?
Kuna wafanya biashara wangapi wanafanya biashara kimazoea hapo mtaani kwenu na hawajui wafanye nini kwenye mambo ya fedha!
Hawajui wafanye nini kukuza biashara zao wala hawana uelewa na mambo yote ya biashara
Nachojua wapo wengi tu na wana pesa ndogo ndogo za kuweza kukulipa kama tu utajua namna ya Kuwasiadia na wakafanikiwa
Umesoma agriculture, kijijini kwenu kuna mashamba kibao yanahitaji wataalamu wa kuelekeza watu wapate faida katika kilimo na ufugaji!
Basi nenda kijiji kingine kama unaona aibu kuonekana msomi halafu upo mashambani
Fikiria wazo ndani ya taaluma yako
Umesoma social development, ehe una project gani ya kuleta maendeleo katika jamii yako? Au unangoja kuwa afisa mtendaji!
Sawa una haki ya kuwa afisa mtendaji lakini jiulize kuna wahitimu wangapi wa social works na kuna idadi ya kata ngapi zinahitaji afisa watendaji!?
Kila mwaka kuna wahitimu wengi wa social development lakini,
Tanzania bado masikini vile vile hakuna hata project kubwa ya kuondoa au kupunguza umasikini
Umesoma Ualimu iwe wa sekondari au msingi na upo mtaani hapo, angalia idadi ya watoto wanao soma kisha jiulize wana uhitaji gani kupitia taaluma yako?
Hakuna mzazi asiyetaka mwanae afaulu anza na mtoto mmoja ambae ana nia ya kusoma
Mfundishe somo unaloliweza sana kwa muda wako wa ziada hata nusu saa tu hapo hapo nje ya unapokaa na usiombe pesa!
Ukifundisha vizuri ndani ya mwezi atawaambia wenzake na idadi itaongezeka,
Taarifa zitafika kwa wazazi hapo sasa Ndio weka mikakati ya malipo kwa kuangalia uwezo wao
Heshimu muda na gharama ulizotumia kupata taaluma yako usikubali kujitolea!
Fikiria miaka zaidi ya 16 umepoteza vitu vingi, ulivumilia mambo mengi na hata wazazi walijinyima kwa ajili yako
Halafu leo hii unaenda kujitolea miaka zaidi ya mitatu kwenye taasisi ya mtu halafu muda wa kuajiri ukifika wanaleta watu wao!
Kuna faida za kujitolea sikatai lakini fikiria umejitolea miaka 3, hulipwi au unalipiwa pesa kidogo sana
Ambayo haitoshi hata nauli halafu muda unafika wa kuajiriwa analetwa mtu mwingine!
Hebu hata wewe waza tu je ungetumia hio miaka 3 kujiajiri kwa wazo lako ndani ya taaluma yako ungekuwa na wateja wangapi?
Hata kama unaamini katika kujitolea basi angalau panga muda wako vizuri fanya vyote
Yani jitolee kwenye hio taasisi na jitolee kwenye biashara yako
Huwa nina shangaa sana mtu anapoteza muda wake mwingi kujitolea kwenye biashara au taasisi za watu wengine
Bila hata malipo ila hachoki na hakati tamaa lakini anaona ugumu kujitolea kukuza wazo lake!
Mtu anafanya sales kwenye kampuni za watu na anaingiza wateja wengi ila anaona shida kutafuta wateja wake hata kwa mara moja moja!
Tumia mitandao kujiajiri kupitia taaluma yako
Kama unaona aibu kuonekana msomi mshamba hapo mtaani au kijijini kwenu basi mitandao naamini ni sehemu sahihi zaidi
Huo muda unaotumia kuperuzi na kufatilia maisha ya wengine hebu badilika na tumia kupost taaluma yako.
Jiweke kisomi, na ongelea huduma zako kwa njia ya kuelimisha kupitia Facebook, Instagram , jamiiforums nk
Elekeza watu kile unachokijua iwe sheria, uhasibu, uchumi, siasa, Ualimu nk
Mtaji ni muda wako kidogo, simu na vocha tu, naamini ukiwa na nia na dhamira
Ndani ya miezi michache utapata watu wa kuwahudumia, kikubwa usiweke tamaa mbele anza na kujitolea!
Heshimu taaluma yako na usifanye biashara (kazi) nje ya taaluma yako
Mfano umesoma sheria halafu unauza maandazi, umesoma Ualimu unaamua kuuza mitumba
Umesoma agriculture unaenda kubeba zege, umesoma maendeleo ya jamii tunakukuta unauza duka la nguo za watoto, mesoma economics unaenda kudanga!
Umesoma sijui project planning halafu unakuja kuuza mgahawa!
Sasa aliyesoma hotel management afanye nini? Au yule mama asiye na elimu kabisa mtaani afanye nini?
Haya mambo Ndio yameshusha thamani ya elimu ya Tanzania na mpaka sasa msomi anadharaulika mitaani
Haiwezekani msomi awaze Sawa na yule ambae hakusoma
Fanya hizo kazi lakini kwa muda ambao unajitafuta huku unajitolea kupitia taaluma yako halisi
Na kama umeamua kufanya hizo biashara,
Inawezekana ulitamani kuwa hivyo toka awali sasa kwanini ulipoteza muda na pesa kusoma kitu ambacho hukipendi na ulijua hutokitumia!
Jiajiri kupitia taaluma kuipa hadhi jamii na kurudisha thamani ya elimu yako
Naomba nisieleweke vibaya, sipingi wala kudharau maoni na maamuzi ya mtu,
Sikatai kuwa kujitolea kuna faida, sibishi wala kukinzana na yoyote anaejitafuta kwa kufanya chochote
Ila najaribu kuonesha njia kwa wale waliokwama namna ya kufanya maamuzi baada ya Kuhitimu Elimu zao
Hivyo simama katika unacho kiamini maana maisha ni zawadi ya muda mfupi na kila mmoja anapaswa kufurahia kwa namna yake
Kujiajiri bila pesa sio rahisi lakini inawezekana hivyo amua sasa kufanya mabadiliko katika maisha na jamii yako kupitia taaluma yako
Comments 1