Utangulizi
Biashara ya burger bado biashara ngeni sana kwa wakazi wengi wa nchi ya Tanzania na hata soko lake bado lipo wazi na hakuna ushindani,
Burger sio chakula maarufu sana kwa wakazi wengi nchini Tanzania ukilinganisha na aina nyingine ya vyakula
Naweza kusema kuwa biashara ya burger haijaweza kuenea sana kwa sababu ya ugeni wake kwa watanzania wengi,
Lakini gharama za uendeshaji ni ndogo sana au hata za kawaida sana tofauti kabisa na ukubwa wa jina la burger!
Watu wengi wakisikia neno burger basi huwaza kuwa ni aina ya chakula cha kifahari sana hata cha gharama kubwa mno
Hii imepelekea uoga kwenye akili za walio wengi kuanzia wateja na hata wafanya biashara wenyewe.
Burger Sio Chakula Cha Ufahari
Kama iliyo vyakula vingine kama mihogo ,maandazi nk basi hata burger ndio ilivyo pia na sio jambo zito
Wauzaji wengi wa burger wanaofanya biashara hii wameikuza sana kiasi cha kuuza kwa gharama kubwa mno,
Hali ambayo inafanya wateja kuogopa na kuona kama chakula cha anasa au kinawafaa watoto wa geti kali pekee.

Mahitaji Ya Biashara Ya Burger
Mara nyingi mahitaji hutegemea na namna mfanya biashara amepanga kufanya biashara yake ila hapa tutuweka mahitaji ya msingi zaidi,
- Mshine ya kusaga nyama ( sio lazima ,unaweza nunua nyama iliyo sagwa)
- Jiko
- Wavu wa kuchomea nyama
- Chips chombeza (sio lazima)
- Nyama ya kuku na ya ng”ombe na viungo vya nyama
- Nyanya
- Mayonise
- Tomato sause
- Mkate wa burger au hata skonzi ya duara
- vitunguu
- Majani ya salad ( sio lazima sana)
- Mshine ya kupashia moto burger au hata oven ya kawaida
- Sahani
- Vifungashio
- Eneo
- Viti , meza NK

Kitu cha msingi zaidi kwenye burger ni nyama , inapaswa kuwa na ladha nzuri sana na yenye ubora mkubwa
Nyama ndio ina beba maana nzima ya burger zako pia ndio huleta utofauti kati ya wafanya biashara washindani.
Hivyo ni lazima kujifunza kuandaa nyama ya burger kwanza kama unataka mafanikio kwenye biashara hii
Nyama lazima iwe na viungo ,laini na isiyo vunda wala kuharibika. Bila kusahau muundo wa duara maalumu.
Unaweza ingia Google au Youtube kuna madarasa ya bure kabisa namna ya kutengeneza nyama na burger.

Bei Ya Kuuza Burger
Mara nyingi bei hutegemea mazingira, kipato cha wateja na hata uwekezaji wa mfanya biashara husika,
Ila angalau bei yafaa kuwa kati shilingi elfu moja mpaka elfu tano za Tanzania au zaidi kwa wateja wenye pesa.
Pia bei hupaswa kuzingatia ukubwa wa burger na vikorombwezo viliyomo ili mteja apate chaguo la kutosha.
Biashara Ya Burger Kwa Wasio Na Mitaji Mikubwa
Kama huna mtaji mkubwa bado unaweza kufanya biashara hii hata nyumbani unapoishi kama kuna mzunguko wa watu
Au unaweza kutengeneza na kuuza kwa oda maalumu au hata kujitangaza mitandaoni na kupata wateja wengi.
Maeneo mengi ya uswahilini ni rahisi sana kuuza burger kwa urahisi kwa wasio na mtaji mkubwa kwasababu ,
Haihitaji mambo mengi sana kuunda burger za uswahilini zaidi ya nyama kidogo ,mkate na vitunguu au mayonise kiasi.
Wakazi wengi wa uswahilini hawana mambo mengi na wala hawajui ladha kamili ya burger tofauti na mjini
Maana asilimia kubwa ya wakazi wa mjini au sehemu za watu wenye pesa wana uzoefu wa maisha ya nchi za nje.
Hivyo kama uko nyumbani na huna mtaji mkubwa ,unaweza kuanzia hapo hapo kwanza na kukuza mtaji wako.
Angalau shilingi elfu 50000 inatosha kuanzia kwa anaeanza kufanyia biashara nyumbani kwa kutumia vifaa ya nyumbani
Kuhusu mashine ya kusaga nyama sio lazima kwasababu nyama zilizosagwa pia huuzwa buchani.

Biashara Ya Burger Kwa Wenye Mitaji Mikubwa
Kwa mwenye uwezo mzuri na mtaji mkubwa anaweza kufanya biashara ya burger kwa namna nzuri zaidi,
Kwa maana ya kufanya biashara yenye chapa (brand) maalumu na rasmi inayo jitegemea.
Hapa pia itapendeza kuzingatia wateja wenye kipato cha kati au kikubwa hivyo kuweka ubora kuendana nao
Lakini pia kuzingatia eneo zuri lenye utulivu mkubwa sana na lenye kuvutia hata kama ni eneo dogo,
Vile vile usajili wa biashara, vibali muhimu , wafanyakazi wa kuhudumia na hata matangazo yakutosha zaidi.
Kwahio hii ni picha halisi namna mtu mwenye mtaji anaweza tekeleza wazo hili pasi na shaka kabisa
Hatua Za Kufuata Kwa Wenye Mitaji Mikubwa
- kuchagua jina zuri la biashara
Liwe jina jesepi na rahisi kukumbukwa na ikiwezekana liendane na neno burger
- Usajili wa biashara
Ni muhimu kusajili biashara ili kuwa huru na kufanya biashara hii kwa upana na uhakika
- Kutafuta eneo
Sio lazima liwe eneo kubwa sana , hata kibanda cha wastani kinatosha sana muhimu kuwe na muonekano mzuri
- Kuweka samani
Kama viti na meza au urembo mwingine wenye kuleta mvuto
- Kuajiri wafanyakazi
Kama kuna ulazima wa kuwa na wafanyakazi pia bila kusahau sare za kazi
- Kujitangaza
Biashara ni matangazo hivyo lazima kuwe na mkakati wa kutafuta masoko kwa njia zote
- Kuboresha huduma mara kwa mara
Hususani kusikiliza matakwa ya wateja kisha kufanyia kazi mara kwa mara.

Mambo Ya Kuzingatia Kwenye Biashara Ya Burger
Ili kupata mafanikio makubwa zaidi kwenye biashara hii nchini Tanzania japokuwa hakuna ushindai mkubwa sana,
Mambo yafuatayo ni muhimu sana kuzingatiwa:
- Nyama yenye ladha nzuri
- usafi
- Eneo lenye mzunguko wa watu wengi kama maeneo karibu na vyuo, ofisi mbalimbali au stendi za magari
- Bei ya wastani kulingana na kipato cha wateja
- Kipimo kizuri cha burger
- Kutokupunja nyama
- Uwepo wa vikorombwezo muhimu vyote.NK
Hitimisho Na Changamoto Za Biashara Ya Burger
Biashara ya burger bado ina soko kubwa na fursa nchini Tanzania hivyo ni rahisi sana kupata wateja wengi,
Kwa mfanya biashara mwenye nia na malengo makubwa anaweza kuipa biashara hii thamani kwa ubunifu na kufanikiwa
Hakuna jambo rahisi lisilo na changamoto kabisa ila inawezekana kwa mwenye nia ya dhati na malengo makubwa,
Changamoto kubwa zaidi ni ugeni wa chakula hiki kwa wakazi wengi wa Tanzania pia imani kuhusu bei,
Wengi wameaminishwa kuwa ni chakula cha gharama kubwa sana au hata anasa sana kukila hivyo huogopa!
Kitu ambacho sio kweli kabisa maana burger ni chakula cha haraka na kiburudisho cha kawaida kama vyakula vingine.