Utangulizi
Biashara ya mahindi ya kuchoma sio biashara ngeni kabisa nchini Tanzania lakini pia ni miongoni mwa biashara ndogo yenye faida kubwa sana
Watu wengi wanaofanya biashara hii wana uwezo wa kuendesha maisha yao ya kila siku bila kusahau kufanya mambo yenye maendeleo
Wengi hudharau sana biashara ya mahindi ya kuchoma na kuhisi kuwa haina faida sana wala uwezo wa kufanikisha malengo
Wamesahau kabisa kuwa mahindi ya kuchoma ni moja kati ya kiburudisho kipendwacho na watu wengi sana mjini hata vijijini
Japokuwa huuzwa kwa bei ndogo sana lakini mzunguko wa wahitaji na wateja huwa mkubwa zaidi hivyo kufanya faida kupatikana kwa haraka
Mtaji wake wa kuanzia ni mdogo sana na upo ndani ya uwezo wa mtu yoyote mwenye nia ya dhati
Hii hutokana na ukweli kuwa baadhi ya vifaa kama jiko unaweza kuanza na lile la matumizi ya nyumbani la kila siku
Bila kusahau huhitaji vifaa vingi kuanza kuchoma mahindi zaidi ya jiko , wavu na mahindi yenyewe!
Vile vile uhakika wa kuuza ni mkubwa hata kama utaamua kuuzia mtaani kwako au hata nje ya nyumba unayoishi
Pia kutokana na kupendwa na watu bila kusahau bei rafiki kwa wateja imefanya biashara hii kupata mvuto zaidi
Vile vile biashara hii haihitaji ujuzi wala utaalamu wowote wa ziada zaidi ya kuchoma mahindi pekee.

Sehemu nyingi huuza kipande kidogo cha muhindi wa kuchoma shilingi mia moja na muhindi mzima kuanzia mia 5
Bei huweza kupanda au kushuka kutegemea mazingira,msimu na hata sababu zingine za muuzaji kama ushindani.
Kwa kawaida biashara ya kuchoma mahindi inahitaji vifaa vichache sana vya kuanzia biashara kama ifuatavyo:
- Jiko la kuchomea
- Wavu wa chuma
- Chumvi
- Ndimu
- Pilipili ya unga
- Mkaa
- Mahindi
- Vifungashio kama magazeti
Ukweli ni kuwa biashara hii haina mambo mengi kutokana na uhalisia wake hasa kwa wateja wanao nunua
Sio aina ya baishara inayotaka mteja kukaa hapo hapo kula mahindi aliyonunua na zaidi wateja hupendelea kusimama
Ni chakula rahisi kuliwa katika mazingira yoyote yale hivyo usiwaze kuweka vitu vingi kwa lengo la kuvuta wateja
Ila kama unaweza kupata benchi husaidia zaidi wateja kuvutiwa kukaa hasa wakati wanangoja huduma
Hivyo unaweza kuanza biashara hii hata kwa mtaji wa Elfu 3 tu za kununulia mahindi hasa kipindi cha msimu huwa mengi sana
Kama tayari una jiko na wavu wa kuchomea mahindi , ukishapata uhakika wa wateja utakuza mtaji taratibu kupitia faida unayopata.
Na kama una mtaji mzuri zaidi unaweza kufanya biashara kwa namna ya utofauti zaidi kwa uzingatiaji wa mazingira mazuri.
Sehemu Zenye Wateja Wengi Wa Biashara Ya Mahindi Ya Kuchoma
Biashara hii ina wateja wengi sehemu yoyote ile bila kuogopa kabisa unaweza kuanzisha hata mtaani kwako
Lakini ili kuongeza mzunguko mkubwa zaidi wa biashara yako zingatia maeneo kama:
- Stendi za dala dala
- Stendi za mabasi ya mikoani
- Vijiwe vya boda boda na bajaji
- Vijiwe vya mazungumzo ya vijana
- Mashuleni
- Nje ya vyuo mbali mbali
- kwenye Masoko
- Fukwe za bahari
- Na shemu nyingine zote zenye mkusanyiko wa watu wengi.
Biashara hii zaidi hupendwa msimu wa baridi na mvua hakika wateja wengi hufurahia kutafuna mahindi ya moto wakati baridi.

Mambo Ya Kuzingatia Kwenye Biashara Ya Mahindi Ya Kuchoma
- Ununuzi wa mahindi laini yenye ladha
- Hali ya joto (Moto) yaani mahindi yawe ya moto na epuka kuandaa mahindi mengi na kuyachoma kabla ya uwepo wa wateja
- Kutokuunguza mahindi kabisa yaani epuka kuuza mahindi meusi
- Kutokuwa na hali ya uchafu wa aina yoyote kuanzia mazingira na mwili hasa zingatia usiwe unavuja jasho kabisa
- Kauli nzuri hasa jitahidi kuwa muongeaji sana hufanya mteja atafune muhindi haraka na kuongeza mwingine
- Muda wa kuanza biashara hasa jioni na usiku, pia unaweza kuanza mchana inategemea na wateja wako
- Pilipili ya unga isiyo washa sana na ndimu kwa wateja wanopenda.
Hitimisho
Biashara hii ya mahindi ya kuchoma ni biashara isiyotumia nguvu kubwa sana japo ina changamoto chache kama:
Baadhi ya wateja hutaka kujichagulia mahindi wao wenyewe wanayotaka na hii hupelekea kukwazika kwa muuzaji kiasi
Hivyo jitahidi kuwa na subra sana pia nunua mahindi yenye mvuto kwa wateja hasa yale makubwa makubwa.