Makande ni chakula mchanganyiko wa mahindi yaliyokobolewa na maharage, kuna wengine huongezea jungu mawe na vitu vingine kulingana na uhitaji wake.
Wengine hupika na nyama za kukaanga, samaki za kukaanga, kuku za kukaanga nk.
Kama unaanza huna pesa wala wateja basi tumia mchanganyiko wa maharage na mahindi, nazi, na viungo kama kitunguu, nyanya, karoti na hoho.
Halafu utaongeza mambo mengine kulingana na uhitaji wa wateja wako kwa baadae ukishapata soko la uhakika.
Biashara hii ni nzuri inatumia mtaji kidogo sana lakini faida kubwa (makande yana asili ya kujaa na kuvimba yakiiva) ,
Pia ni aina ya chakula ambacho hakipikwi na wafanya biashara wengi.
Makande yana soko kubwa kutokana na ukweli kuwa sehemu nyingi vyakula hupikwa vya aina moja,
Yani wateja hawana chakula cha kubadilisha zaidi ya wali, ugali na ndizi,
Wateja wengi wanapenda makande lakini ni biashara ambayo wafanyabiashara wengi huidharau,
Hivyo kama ukiwa mbunifu ukapika makande mazuri uhakika wa kupata wateja ni zaidi ya 100%.
Mimi nimewahi kuuza makande wakati nikiwa chuoni, nilianza kwa mtaji wa shilingi elfu 5 tu,
Nilikuwa napika nyumbani na kwenda kusambaza vijiwe vya bajaji na boda boda.
Hivyo nina ongea kitu ambacho nina uzoefu nacho kwa asilimia zaidi ya 100%,
Kama umekwama Huna biashara ya kufanya, labda ni mama wa nyumbani, au Mwanafunzi wa chuo nakushari anza biashara hii.
Mtaji wa biashara ya makande
Mimi nilianza kwa mtaji wa elfu 5, nilinunua mahindi robo tatu, maharage nusu,sukari, nazi,nyanya, mafuta, kitunguu, hoho na karoti.
Mabakuli ya mifuniko nilianza na zangu na baadhi niliazima kwa wanafunzi tuliokuwa tunaishi nyumba moja, sufuria na jiko nilikuwanavyo.
Nilikuwa naroweka mahindi na maharage usiku mzima, kisha napika mapema,
Wateja nilitafuta na kuwatangazia siku mbili kabla sijaanza biashara hivyo nilikuwa na uhakika wa wateja kadhaa na namba zao.
Kwenye robo tatu ya maharage na nusu ya mahindi nilitoa wastani wa bakuli 8 kwa bei ya 1000@ jumla 8000 nikitoa mtaji nabakiwa na faida ya 3000 mpaka 3500.
Mwanzoni sikutumia faida kwa mahitaji yangu binafsi, nilihakikisha nanunua vitu vyote ambavyo sina kama kuongeza mabakuli na sufuria kubwa na jiko.
Baada ya miezi mitatu tayari nilikuwa na wateja wengi sehemu mbalimbali kama ofisi za karibu, boda boda, wanafunzi wa chuo nk. Na nilianza kupata faida ya 30000 kwa siku kwa mtaji wa 15000 kila siku.
Anza na ulichonacho
Jiangalie hapo unapoishi una kitu gani ambacho unaweza kutumia kama mtaji, iwe vyombo, iwe mahitaji ya upishi wa makande kama maharage, mahindi, una sukari, una chumvi, una mafuta nk,
Kisha angalia akiba yako nunua mapungufu ambayo Huna, ikiwa Huna akiba kopa kwa mtu yoyote na hakikisha unamrudishia.
Ikiwa Huna kila kitu basi mtaji wako hauwezi kuzidi 15000 maana nina uhakika sufuria na jiko hakuna ambae hana nyumbani,
Kwahio labda utalazimika kununua mabakuli ambayo huuzwa wastani wa 1000 mpaka 1500 kutegemea na mazingira.
Utajifunza kubana bajeti zaidi baadae kadiri unavyozoea na kuna wakati vitu hubaki hivyo unaweza tumia wakati mwingine kama mkaa, mafuta nk.
Jinsi ya kupata wateja wa biashara ya makande
Kabla hujaanza rasmi angalia maeneo ya karibu unapoishi watu gani ambao hulazimika kununua vyakula mtaani kila siku?
- Wapangaji wakiume ambao hawajaoa
- Vijiwe vya boda boda na bajaji
- Ofisi ndogo ndogo za mitaani
- Mafundi gereji
- Stendi za daladala
- Wanafunzi wa vyuo nk
Hivyo anza na wale walio karibu yako na uliowazoea ili usione ugumu sana, toka zungumza nao bila aibu kuwa unauza makande kama wanahitaji uwe unawapelekea na chukua namba za kila mteja (lazimisha wakupe namba za simu).
Hakikisha angalau unapata namba 10 mpka 15 , maana sio wote watanunua! Bei weka wastani wa 1000 kwa bakuli moja au ongeza kulingana na aina ya wateja ulionao Ila usiwe na tamaa utakosa wateja.
Lakini pia tengeneza ukurasa mitandaoni kama Facebook na Instagram na jitangaze kuwa unauza makande kwa kuweka picha nzuri za makande.
Kila siku hakikisha unapata wateja wapya angalau 5 na chukua namba zao ili iwe rahisi kuwatafuta muda wa kusambaza.
Pika muda mzuri kama vile saa 6 na nusu na pakua kwenye mabakuli masafi na weka ndani ya mfuko mzuri kisha anza kusambaza kwa wateja wako.
Mambo ya kuzingatia katika biashara ya makande
- Lugha nzuri kwa wateja wako, siku zote jishushe, nyenyekea,heshimu na kuwa mpole kwa wateja
- Usafi wako binafsi, usafi wa chakula na vyombo
- Chakula kizuri, hakikisha kuwa unapika makande laini sana, yasikose nazi au karanga ikolee yani pika kama unajipikia wewe au kama unapikia familia yako
- Uvumilivu, hakuna biashara isiyo na changamoto hivo lazima ujue jinsi ya kukabiliana nazo
- Ubunifu, hakikisha unajua namna ya kuteka wateja kwa mbinu nyingi usikubali kuzidiwa kete na wafanyabiashara wengine
- Epuka tamaa na hakikisha kuwa unawekeza katika biashara yako kwanza faida unayopata kwa kuangalia mapungufu uliyonayo
- Uaminifu kwa wateja na kuwa mkweli ukisema utapeleka sa 7 iwe hivo na ukiona makande yana hitilafu yoyote waombe msamaha wateja wako.
Kila jambo linawezekana ukiwa na nia na Imani pamoja na Dhamira ya dhati.
Comments 1