Jinsi Ya Kuanzisha Biashara Ya Matunda
Biashara ya matunda ni biashara inayopendwa sana Duniani kote na hata nchini Tanzania lakini pia ina faida kubwa
Licha ya matunda kuwa na faida nyingi mwilini pia bado kuna faida nyingi sana za kiuchumi kwenye matunda
Biashara hii ina dharaulika sana lakini ni miongoni mwa biashara zinazolipa sana licha ya urahisi wake katika uanzishaji
Matunda pia ni biashara inayotumia mtaji kidogo sana lakini faida yake huwa mara mbili au zaidi ya mtaji
Vile vile ni biashara rahisi kufanywa na jinsia zote na rika zote bila haja ya kuona aibu wala kujificha
Pia inaweza kufanywa kwa muundo wowote ule mfano kutembeza au kukaa mahala na unaweza kuanza kwa mtaji mkubwa au mdogo.

Kila tunda lina msimu wake wa kupatikana kuna misimu baadhi ya matunda hupotea na misimu mingine huwa mengi
Na bei hupanda au kushuka kutegemea msimu husika wa matunda sokoni wanunuzi na hata faida yake.
Mgawanyo Wa Aina Za Biashara Ya Matunda
Unaweza kufanya biashara hii katika mgawanyo wa aina mbili
- Matunda ya kukata kata
- matunda mazima
Aina hizi zinategemea wanunuaji, kuna wanaotaka matunda mazima kwa ajili ya familia au hupenda kujiandalia wenyewe
Na wapo ambao hutaka yaliyokatwa na kula wawapo katika mihangaiko ya siku au hata lengo la kupunguza kazi za kuyaandaa matunda.
Matunda huuzwa wakati wowote lakini wengi hupendelea zaidi majira ya jioni au asubuhi baada ya kifungua kinywa
Biashara Ya Matunda Ya Kukata
Huu huwa mchanganyiko wa matunda mbali mbali yaliyokatwa na kuchanganywa pamoja katika sahani , bakuli au mfuko
Mfano Maembe, Nanasi, Ndizi, Machungwa , matikiti maji nk Matunda haya humenywa na kukata katwa katika vipande vidogo vidogo
Kisha huchanganywa kwa pamoja ndani ya chombo cha kuuzia kulingana na kipimo cha bei maalumu wengi huuza shilingi elfu 1000
Matunda yaliyokatwa ni rahisi sana kwa wateja hasa wanaokuwa katika mihangaiko ya majukumu nje ya nyumba zao.

Bei ya kuuza inategemea mahala ulipo au unapofanyia biashara na hata aina za watu wanaonunua
Wengi huanza na bei kati ya elfu moja na kuendelea kwakuangalia msimu wa upatikanaji matunda na kipato cha wateja
Unahitaji kuwa na beseni au ndoo, kisu, mabakuli yenye mifuniko, mifuko, maji ya kuosha na kunawa na matunda yenyewe na hata Epron na kofia japo sio lazima
Unaweza kuuza kwa oda maalumu, kibandani na hata kutembeza mitaani inategemea na namna ulivyojiandaa
Ikiwa ni kibandani utatakiwa kukodi eneo au kutengeza kibanda kizuri cha kuuzia hivyo gharama zitategemea na ulipo
Kama ni kutembeza unaweza anza kwa mguu au baiskeli yenye toroli au baiskeli ya kawaida ila ukaweka kikapu kurahisisha ubebabiji wa vitu;

Mtaji Wa Biashara Ya Matunda Ya Kukata kata
Mtaji unategemea namna unataka kuanza lakini hata elfu 30000 inatosha kama huna mabakauli au vifaa
Maana sio lazima kuanza kwa idadi kubwa ya matunda wakati bado huna uhakika wa soko.
Asilimia kubwa matunda huuzwa sokoni kwa bei ndogo sana kwa bei ya jumla mfano soko kama Buguruni au vetenari na mabibo,
Muda mzuri wa kupata matunda mazuri sokoni na kwa bei rafiki ni asubuhi sana alfajiri ,
Bei huanzia shilingi 10 mpaka mia 200 au zaidi kidogo kulingana na aina ya tunda na msimu kwa masoko hayo ya mkoa wa Dar es salaam.
Kuna uwezekano mikoa mingine bei ikawa rahisi zaidi kutokana na ukweli kuwa matunda mengi hutoka nje ya Dar es salaam
Kwahio ukiwa na shilingi Elfu kumi au elfu 15 una uhakika wa kupata matunda mengi ya kuanzia bila shaka.
Biashara Ya Matunda Mazima
Haya maana yake ni uuzaji wa matunda ambayo hayajakatwa katwa kabisa yaani unauza matunda kama ulivyo nunua sokoni
Kama mteja atahitaji unaweza kumkatia hapo hapo na unapaswa kuwa na vifaa vyote kama kisu , maji , na hata sahani au mifuko
Utaratibu ni ule ule unaweza kuuza kwa kutembeza, kukaa mahala na hata kwa oda maalumu.
Mtaji pia utategemea na wewe mwenyewe mapenzi yako na namna unataka kuanza au kuendesha
Lakini kwa kiwango cha chini elfu 10 inaweza kutosha kwa ununuzi wa matunda, Mwanzoni hupaswi kununua vitu vingi mpaka uwe na uhakika wa soko
Pia unaweza kuanza na aina moja ya matunda mfano machungwa pekee, kisha ukafuata utaratibu kama wa hapo juu
Kuhusu kodi ya eneo au usafiri wa baiskeli kwa wasiotaka kutembeza kwa miguu utapaswa kufanya uchunguzi binafsi.
Mambo Ya Kuzingatia Katika Biashara Ya Matunda
- Usafi wa hali ya juu kuanzia vyombo, muonekano, mahala pa biashara mpaka matunda yenyewe
- Mkusanyiko wa watu wengi
- Bei rafiki
- Kauli nzuri
- Uvumilivu
- Juhudi za kutafuta wateja
- Matunda mazuri yenye mvuto na yasiyo haribika
Namna Ya Kupata Wateja Wa Biashara Ya Matunda
Vaa vizuri , kuwa msafi muda wote na muonekano wa kuvutia kisha pita maeneo kama;
Au kama utaamua kukaa sehemu moja pia zingatia baadhi ya maeneo haya maana huwa na uhitaji zaidi
- Hospitali hasa kwa nje kutegea mida ya kuona wangojwa
- Ofisi mbali mbali kubwa au ndogo
- Jirani na magereza hasa siku za kuona wafungwa
- Shuleni
- Stendi za magari
- Vijiwe vya pikipiki na bajaji
- Mitandaoni
- Sokoni
- Majumbani hasa nyumba za watu wenye kipato kiasi
- Mitaani nk
Changamoto Za Biashara Ya Matunda Na Suluhisho
- Matunda kuoza
Jitahidi kuanza na matunda yasiyo haribika haraka hasa kama huna wateja mfano machungwa , tango au matikiti pia tunza kenye jokofu kama unalo
- Ushindani mkubwa
Jaribu kuwa mbunifu na angalia udhaifu wa washindani wako au hata chagua eneo lenye wauzaji wachache
- Matunda kuisha msimu
Hii hupelekea bei kupanda zaidi kwahio jitahidi kutafuta wateja wenye uwezo zaidi au uza matunda kulingana na msimu.
Hitimisho
Kumbuka hizo gharama sio ramsi na hazijajumuisha baadhi ya vifaa kama kodi , kibanda , wala usafiri wowote
Hapo ni picha nzima na wazo la jumla namna ya kuanza Biashara ya matunda kwahio lazima uchunguzi wa kina lazima ufanyike kwanza
Vitu kama faida, mtaji, gharama za uendeshaji zinaweza kutofautiana kati ya sehemu moja na nyingine.