Utangulizi
Biashara ya vitumbua ni biashara rahisi sana kufanyika katika mazingira yoyote yale na wateja wa uhakika wapo kila eneo
Vitumbua ni moja kati ya vitafunwa vinavyopendwa sana nchini Tanzania na watu wa aina zote au hata jinsia zote
Vitumbua ni kitafunwa chenye mchanganyiko wa mchele na sukari kama viungo vikuu zaidi na vinginevyo kwa mapenzi ya mpishi.
Maeneo mengi mjini au hata vijijini hutumia vitumbua kama kifungua kinywa na sio chakula kigeni kabisa kwa wakazi wote
Licha ya utamu wake na ladha ya kipekee ,bei rahisi na uharaka wa kupatikana bado imefanya vitumbua kununuliwa sana na watu wengi.
Biashara ya vitumbua inaweza kufanywa na watu wa kipato cha aina zote kwa maana ya wale wenye mtaji mkubwa au hata mdogo,
Kwa sababu viungo vikuu vya kutengeneza vitumbua hupatikana kila mahala kwa bei rafiki zaidi ambayo watu wengi humudu.
Bila kusahau mchele hulimwa sana Tanzania na maeneo mengi sana hutumika kama chakula kikuu kwa wakazi wengi
Hivyo biashara ya vitumbua kwakuwa hutumia zaidi mchele maana yake hakuna wasi wasi kabisa kwenye upatikanikaji wake.
Muda mzuri zaidi wa kuuza vitumbua ni asubuhi kwa ajili ya chai au jioni kuanzia saa kumi mpaka usiku.
Mtaji Na Mahitaji Ya Biashara Ya Vitumbua
Mtaji wa biashara ya vitumbua hutofautiana kulingana na mapenzi ya mfanya biashara bila kusahau mazingira
Kuna wale wanaofanyia biashara nyumbani au wengine huamua kukodi eneo maalumu la biashara
Pia kuna ambao huifanya biashara hii rasmi na kisasa zaidi na pia huamua kuipa thamani kubwa sana.
Kwahio kwa kuziangatia vigezo hivyo , mtaji wa biashara hii huweza kutofautiana sana kati ya mtu mmoja na mwingine,
Ila kwa uchache sana kwa ambae anaanzia chini kabisa na nyumbani kwake basi angalau shilingi elfu Hamsini za Tanzania( 50000) zinatosha kuanzia.
Kila mmoja huwa na mapenzi yake binafsi linapokuja suala la mahitaji hivyo hapa yataorodheshwa mahitaji muhimu zaidi,
- Mchele uliosagwa unga
- Unga wa ngano kidogo na sio lazima
- Sukari
- Hamira
- Hiriki
- Karai maalumu la vitumbua
- Mafuta ya kupikia
- Nazi (sio lazima)
- Mkaa au gesi
- Kijiti cha chuma cha kugeuzia vitumbua
- Ndoo au deli linaloonesha ndani na lenye mfuniko
- Sufuria au bakuli kubwa la kuwekea uji wa vitumbua
- Kijiko cha kuchotea chenye ukubwa wa wastani
- Benchi la kukalia wateja ( sio lazima sana)
- Jiko
- Vifungashio kama mifuko na magazeti .NK
Wateja Na Bei Ya Biashara Ya Vitumbua
Bei ya kuuza vitumbua huanza kati ya shilingi mia moja mpaka shilingi elfu moja kutegemea na hali ya kipato cha wateja,
Vile vile gharama za ununuzi malighafi na mazingira ya kuuzia huweza kupelekea bei kuwa kubwa zaidi au ndogo zaidi.
Wateja wa vitumbua sio wakutafuta na tochi kwa maana kuwa biashara hii hujiuza yenyewe kwa wahitaji
Uzuri ni kuwa ni biashara ambayo haihitaji kutumia nguvu kubwa sana kwenye matangazo hasa mitaani au vijiweni,
Ni biashara ambayo wateja huja wenyewe japokuwa jitihada za pembeni huweza kuleta wateja zaidi.
- Mitaani
- Stendi za daladala
- Vijiwe vya boda boda na bajaji
- Maeno ya shuleni na vyuo mbali mbali
- Ofisi aina zote
- Stendi kuu za mabasi ya mikoa mbali mbali
- Hotelini na migahawani NK
Pia wateja wengi zaidi hupatikana kwenye mitandao ya kijamii kama facebook na instagram hivyo ni muhimu kujitangaza huko pia.
Biashara ya Vitumbua Kwa Wenye Mitaji Mikubwa
Bishara hii huweza kupewa thamani kubwa zaidi kulingana na ukubwa wa mtaji au mazingira ya muuzaji
Maeneo ya uswahilini hayawezi kuwa sawa na maeneo ya watu wenye kipato cha juu au hata cha kati.
Hivyo muuzaji wa vitumbua wa uswahilini hawezi kuwa sawa kwa ukubwa wa mtaji na muuzaji wa maeneo ya watu wenye pesa .
Kwahio ukiwa na mtaji mzuri unaweza kufanya biashara hii kwa ukubwa na thamani ya juu zaidi au kama biashara kuu,
Kwakuwa na chapa (brand) ya vitumbua na kuuza kisasa zaidi huku ukizingatia ubora na utamu wa vitumbua,
Unaweza pia kuweka chai, maziwa ,kahawa au hata juice kama kinywaji kwa ajili ya wateja wenye uhitaji,
Hio husaidia kuongeza thamani zaidi kwenye biashara hii na hata kuleta mvuto kwa wateja na kujitofautisha.
Hivyo basi kwa wenye mtaji mzuri,kuna njia mbili za kufanya biashara hii
- kuwa na eneo maalumu kwa ajili ya biashara ya vitumbua pekee ,eneo lililo karabatiwa vizuri na mvuto kwa wateja wenye kipato kizuri au
- Kuwa na vijana wengi wasambazaji ,vijana wenye uwezo wa kusambaza na kuuza vitumbua mitaa mbali mbali kisha kuleta mapato.
Njia Mbali mbali Za Kufanya Biashara Ya Vitumbua
- Kutembeza mitaani (kuwa na vijana kadhaa kwa ajili ya kusambaza)
- Kuuzia nje ya nyumba
- Kuuza kwa oda maalumu hasa maofisini au mitandaoni
- Kutafuta eneo moja maalumu kama vijiweni au hata kibandani.
Mambo Ya Kuzingatia Kwenye Biashara Ya Vitumbua
- Usafi wa hali ya juu sana
- Kupika vitumbua laini na vyenye ladha
- Kutoweka unga tofauti na unga wa mchele na kuweka kidogo sana kama italazimika mfano unga wa ngano (epuka vitumbua kuwa kama ugali kwa ndani)
- Kutopunja sukari wala kuweka sukari nyingi sana
- Kuweka mafuta yakutosha wakati wa kuchoma vitumbua
- Eneo lenye mkusanyiko wa watu wengi
- Uivaji wa vitumbua kwa ndani
- Utunzaji wa hali ya joto la vitumbua yaani usiuze vitumbua vya baridi
- Rangi ya kuvutia ya vitumbua na visiwe na rangi nyeupe wala nyeusi iwe ya brauni NK
Changamoto Za Biashara Ya Vitumbua
Hakuna biashara isiyo na changamoto kwenye uendeshaji wake hivyo haipaswi kuogopa kabisa
Inapokuja kwenye biashara hii ya vitumbua, changamoto kubwa zaidi ni:
- Kupanda kwa bei ya mafuta
- Kupanda kwa bei ya sukari
- Kupanda kwa bei ya mkaa
- Kupungua kwa msimu wa mchele
Hivyo changamoto hizi huweza kusababisha hali ya kuyumba kwa biashara au hata kufa kabisa kwa biashara,
Ila kwa mfanya biashara mwenye nia na mapenzi ya dhati kwenye biashara yake hutafuta njia sahihi ili kulinda biashara,
Njia ambayo itasaidia kubaki kwenye biashara yake na kutoharibu ubora wa vitumbua kwa wateja kama iliyo kawaida,
Kwa maana ya kuangalia mbadala ya kupata malighafi au hata kukubali faida kidogo kwa lengo la kulinda biashara.
Hitimisho
Biashara ya vitumbua huweza kufanywa na mtu yoyote kwa maana ya jinsia ya kike au hata ya kiume bila hofu
Biashara hii inaweza kuendesha maisha ya kila siku na hata kusaidia ufikiaji wa malengo makubwa ya mtu
Haijalishi kiwango cha Elimu ya mtu, kama kijana msomi asiye na kazi kabisa bado anaweza kuanza biashara hii na kusaidia maisha yake.
Wengi hudharau sana vitumbua na kuona kama biashara chafu au hata ipo kwa ajili ya kina mama wasio na Elimu,
Sio sahihi kabisa kwasababu kuna pesa nyingi sana kwenye vitumbua na kwa mjasiriamali mwenye jicho la fursa.