You Can Win If You Want

Changamoto za biashara na jinsi ya kukabiliana nazo

Changamoto za biashara ni nini

Changamoto za biashara ni hali (vikwazo na matatizo) zinazojitokeza katika biashara na kutishia au kupelekea biashara kuanguka kabisa

Biashara ina hitaji mbinu, mipango na mikakati katika kufanikiwa na kujiedesha

Hakuna mtu ambae huanzisha biashara kwa lengo la kushindwa!

Ila kuna muda hutokea changamoto na sababu mbali mbali zinazopelekea biashara kushindwa kuendelea

Katika hali hii watu wengi hupata matatizo kama msongo wa mawazo kupitiliza, hofu ya mara kwa mara, kukosa usingizi, kuwa na hasira na hata kushindwa kumudu maisha mengine nje ya biashara zao!

Tafiti zinaonesha kuwa biashara nyingi hufa /huanguka katika kipindi cha miezi 6 mpaka miaka 5 toka zinapofunguliwa

Makundi ya changamoto za biashara

Kuna aina mbili za makundi ya changamoto za biashara

  1. Changamoto za muda mfupi, hizi huwa zile changamoto za kila siku na mara nyingi hupata suluhisho la haraka lakini kama zikikosa suluhisho hupelekea changamoto kuwa kubwa na madhara makubwa zaidi katika biashara
  2. Changamoto za muda mrefu, changamoto hizi huwa zile za kudumu na mara nyingi hutaka suluhisho kubwa na la uhakika katika biashara kwasasabu changamoto hizi mara nyingi hupelekea biashara kufa kabisa

Changamoto kuu za biashara (vyanzo vikuu vya changamoto za biashara)

  1. Ukuaji wa teknolojia
  2. Mzunguko mdogo wa mauzo na  fedha
  3. Mabadiliko ya uchumi wa nchi na Dunia kwa ujumla

Changamoto zikiwa nyingi huweza  kupelekea kuanguka kwa biashara au kuyumba kwa biashara

Sababu zinazopelekea vyanzo vya changamoto za biashara

  1. Nyakati mbaya
  2. Ukosefu wateja
  3. Ukosefu wa malengo ya biashara
  4. Ukosefu wa muda
  5. Uhaba wa mtaji
  6. Ushindani mkubwa
  7. Ubora  mdogo wa bidhaa au huduma
  8. kubadilika kwa misimu
  9. kubadilika kwa sera na uongozi
  10. kufanya biashara kwa mazoea
  11. Kukua kwa Teknolojia
  12. usimamizi mbovu na wafanyakazi wasio stahili
  13. Tamaa ya mafanikio ya haraka na kukosa malengo ya biashara
  14. Ukosefu wa uzoefu wa kutosha
  15. Imani za kishirikina

Changamoto za biashara biashara

Nyakati mbaya 

Kila mmoja anaeanzisha biashara huwa na nyakati zake, kuna nyakati za mtu ambazo humfanya afanikiwe na zipo nyakati mbaya kwa kila mmoja ambazo huwa ngumu kufanikisha jambo lolote hata kama atakuwa amejipanga kwa kila kitu!

Watu wengi hawajui nyakati zao na hujikuta wakipata hasara kubwa na hata kuchukia wanachokifanya kwa kutojua tu nyakati zao sahihi za kutekeleza malengo. Pia soma Alama za nyakati na mafanikio 

Ukosefu wa wateja 

Hali ya wateja kuacha kununua katika biashara,  kupelekea bidhaa kuharibika  au kupitwa na muda baada ya kukaa muda mrefu hivyo kuleta hasara kubwa na mfanyabiashra kushindwa kuendelea na biashara yake

Ukosefu wa malengo ya biashara

Malengo ni kama dira ya biashara husika, malengo hutoa muongozo wa wapi biashara inatakiwa kufika na vipi itafanikiwa

Malengo husaidia kupima ukuaji wa biashara na kutoa mikakati ya kuendesha biashara husika

Watu wengi hufanya biashara zao bila kuwa na malengo na mikakati ya muda maalumu.

Ukosefu wa muda

Mara nyingi hutokea kwa waajiriwa au watu ambao wanamambo mengi nje ya biashara zao hivyo kushindwa kusimamia kwa wakati biashara zao

Uhaba wa mtaji

Sababu nyingine ambazo hufanya watu kufunga biashara zao ni mitaji

Wengi huanza wakiwa na mitaji kidogo au bila mtaji na kushindwa kuendeleza biashara kwa baadae kutokana na kukua kibiashara

Hivyo hujikuta wakikata tamaa au hata kukimbiwa na wateja kutokana na uhaba wa bidhaa au huduma

Ushindani mkubwa

Kila siku hutokea watu mbalimbali ambao huanzisha biashara au huduma Sawa na ile unayofanya

Hii hufanya soko kupata mibadala mingi na wateja kuchagua mahala palipo bora zaidi kwa upande wao

Hivyo watu wengi hushindwa kuendana na kasi ya mabadiliko na kushindwa kupata ufumbuzi wa haraka namna ya kubaki na wateja wao wa mwanzo au hata wapya

Ubora mdogo wa bidhaa au huduma

Kuwa na bidhaa bora na huduma nzuri ni chagua la kwanza la mteja yoyote anapofanya manunuzi

Watu wengi hufanya biashara zao katika ubora wa chini sana, hivo kupelekea wateja kutoona umuhimu wala sababu za kufanya manunuzi kwao

Mwisho biashara hukosa wateja na muhusika huamua kufunga kabisa

Kubadilika kwa misimu ya biashara

Sio kila msimu huwa na mauzo!

Mfano msimu wa kilimo cha zao fulani, msimu wa maradhi fulani (kama corona na barakoa), msimu wa mapenzi ya kitu fulani kutokana na ushawishi wa kijamii

Sasa kuna watu hufungua biashara kutokana na kusoma aina ya msimu mmoja na kuamini kuwa mambo yataendelea,

Hivo baada ya msimu kupita na mambo kuisha hufanya soko lote liishe na biashara hufungwa!

Lakini pia kuna misimu mibaya ya soko na wateja, hali ngumu na changamoto za maisha hufanya wateja kubadili aina ya manunuzi ya huduma au bidhaa zao

Kubadilika kwa sera za nchi na uongozi

Kila kiongozi Huja na sera zake hasa kwa nchi kama Tanzania

Hii kuchanganya sana wafanyabiashara kwa kushindwa kuendesha biashara zao kutokana na mabadiliko mbali mbali ya sera za nchi na viongozi wapya kila mara

Kama kupanda kwa kodi na gharama za maisha hivo kupelekea biashara nyingi kuyumba

Wengi wanao athiriwa huwa wawekezaji kutoka nchi na mataifa mengine hivo huamua kufunga biashara zao

Kufanya biashara kwa mazoea

Wafanya biashara wengi hufanya biashara zao bila ubunifu wa ziada, hukosa Elimu ya kuendesha biashara zao, huduma kwa wateja mbovu nk

Hii hufanya wateja kuchoka na kuamua kutafuta sehemu nyingine za ununuzi

Hivyo hupelekea biashara kukosa wateja na kufungwa

Kukua kwa Teknolojia

Mitandao mingi imeanzishwa kwa kufanya urahisishaji wa huduma na bidhaa kumfikia mteja popote alipo

Hii hufanya wateja wengi kuwa na machaguo ya haraka kwa njia za  mitandao mfano TEMU, AMAZON nk

Usimamizi mbovu na wafanyakazi wasiostahili

Kukosekana kwa usimamizi mzuri wa biashara katika hatua zote hufanya biashara kufa mapema

wengi huanzisha biashara wakiwa na kazi nyingine hivo kuajiri watu wasio na mapenzi ya dhati ya kukuza biashara

Tamaa ya mafanikio ya haraka

Watu wengi hutaka kuona mafanikio ya biashara ndani ya muda mfupi hivo kujikuta wakichoka mapema katika kipindi ambacho biashara inajitafuta na haina mzunguko mkubwa

Biashara inataka malengo ya muda mrefu na inahitaji muda na uvumilivu mkubwa iweze kujikuza

Ukosefu wa uzoefu wa kutosha

Uzoefu ni muhimu sana katika kufanikisha biashara nzima, kuanzia katika usimamizi, ununuzi, mikakati na utunzaji wa fedha

Wengi huanzisha biashara ambazo hawana uzoefu nazo hivo hukutana na changamoto nyingi ambazo hushindwa kuzitatua na mwisho hukata tamaa kabisa

Imani za kishirikina

Hakuna uchawi katika biashara, wengi wameingia katika mtego wa kuamini waganga na manabii feki

Wanajikuta wakipoteza nguvu na pesa nyingi kuamini biashara zao zinataka dawa za mvuto na kuondoa wachawi!

Hii hupelekea biashara kukosa jitihada yakinifu na fedha za uendeshaji mwishoni hufa kabisa

Changamoto za biashara na jinsi ya kuzikabili

Kutatua /kukabiliana na changamoto za biashara

Nyakati mbaya

Jua nyakati zako za mafanikio kabla hujaanza biashara yako kwa kuangalia upo katika wakati  gani wewe binafsi  kwanza

Angalia nyakati ulizinazo kama zinaandamana na vikwazo na mapito magumu mengi zaidi mfano unauguza, umetoka kufiwa na mtu wa karibu sana, una madeni mengi sana, Huna furaha moyoni nk

Ukiwa katika nyakati za matatizo mengi huwa sio wakati muafaka wa kuanzisha biashara yako kwani utashindwa kabisa namna ya kuimudu na inaweza kuanguka mapema

Fungua biashara yako katika nyakati zilizotulia kuanzia moyoni mapaka mazingira yako ya nje ya mwili

Ukosefu wa wateja

Kukabiliana na hali ya ukosefu wa wateja unapaswa kuchunguza na kubadili mambo Haya :

Zingatia eneo zuri la biashara kwa kuangalia mambo yafuatayo 
  • Eneo linalofikika kiurahisi, halina vikwazo vingi na lenye kuonekana haraka
  • Eneo lenye mzunguko mkubwa wa watu wenye uhitaji na bidhaa au huduma unayotoa
  • Sehemu ambayo ina maegesho ya magari kwa kuangalia aina ya bidhaa na huduma yako kama ina  wateja wanaokuja na usafiri wao binafsi
  • Eneo salama kwa wateja nyakati zote wanazo hitaji bidhaa kutoka kwako
Bei rafiki kulingana na aina ya bidhaa au huduma yako, mazingira halisi ilipo biashara na aina za wateja wako

Mfano kuna bidhaa unaweza kuuza bei ya 1000 tandika na ukapata wateja Ila ukiuza masaki ikaonekana haina ubora!

Kuna bidhaa unaweza kuuza elfu 10 Dar es Salaam na ikauzika Ila ikakosa soko kigoma!

Hivo Lazima upange bei ambayo inaendana na uhalisia wa uchumi wa wateja wako

“Matangazo” 

Unaweza kuwa na bidhaa au huduma nzuri Ila ikakosa matangazo mazuri! Jitahidi kuweka bajeti katika matangazo yako ili kufikia watu wengi zaidi, jitangaze sehemu zote za mitandao na usichoke

“Huduma bora kwa wateja” 

Mteja ni mfalme, lazima umpe heshima mteja na muhudumie katika kiwango ambacho hata kwa mara nyingine atakumbuka kurudi kwako! Zingatia yafuatayo :

  • Wafanyakazi waadilifu na wacheshi
  • Ofa mbali mbali kwa wateja kama kupelekewa bure bidhaa zao kwa wale wa karibu (free delivery)
  • Punguza la bei
  • Kauli nzuri
  • Usafi wa mazingira na bidhaa nk
“Bidhaa au huduma nzuri” 

Jitahidi uuze bidhaa na huduma bora zaidi na zinazojiuza bila kutumia nguvu, mteja akipata huduma kwako basi awe na sababu ya kurudi na kuacha kununua mahala kwingine

Hapa zingatia sana bidhaa na huduma ambazo zinatatua na kutibu changamoto za mteja moja kwa moja

Ukosefu wa malengo ya biashara

Lazima uwe na malengo ya biashara yako, yaandike vizuri na uyasimamie

Biashara lazima iwe na malengo ya muda mrefu au muda mfupi kulingana na hitaji lako

Malengo yatakusaida kukupa dira na kuendesha biashara yako

Ukosefu wa muda 

Kama umebanwa sana kiasi cha kushindwa kusimamia na kuendesha biashara yako tafuta msimamizi mzuri akusaidie

Msimamizi anaweza kuwa ndugu, mke /muwe, watoto au hata ajiri mtu wa uhakika

Japokuwa changamoto za kufanya kazi na ndugu huwa kubwa na pia kuajiri mtu huweza kusababisha kuua biashara

Unapaswa kufatilia biashara kila unapopata nafasi mara kwa mara

Au usifungue biashara mpaka utakapo weka Sawa mambo yako mengine kwanza

Uhaba  wa mtaji 

Ikiwa biashara ina uhaba wa mtaji,

anza na bidhaa muhimu kwanza

Tafuta msambazaji mmoja ongea nae na chukua bidhaa zinazouzika sana kwa Mali Kauli (hakikisha unakuwa muanifu)

Tafuta wawekezaji

Kama Biashara yako ina soko la uhakika na umeyumba katika mtaji basi ongea na watu wenye uwezo kwa kukupa sapoti na angalia namna ya kushirikiana nao

Ongea na ndugu, jamaa na marafiki

Usiogope kuonekana omba omba, zungumza na watu wakukopeshe au wakusaidie usikubali biashara kufa wakati una watu wanaokuzunguka

Kopa

Kwenye taasisi mbali mbali kwa riba, japo sishauri sana kukopa kwenye taasisi ikiwa biashara bado mpya na changa,

Kwasababu unaweza kushindwa kurejesha na kuwa katika hali mbaya zaidi

Ushindani mkubwa 

Changamoto hii unapasawa kuwa na ubunifu mkubwa angalia nini hasa wamekuzidi washindani wako na weka zaidi yao

Mfano bei ya chini, na wewe hakikisha unatafuta bidhaa za bei ya chini zaidi ili upunguze bei kwa wateja

Zawadi na ofa mbali mbali, weka ofa za mara kwa mara kwa wateja wako ili wafurahie mfano huduma za kupelekea bidhaa bure kwa walio karibu nk

Usikubali washindani wako wa kuzidi maarifa, kila siku tafuta mitego mipya ya kunasa wateja wako

Huduma na bidhaa bora 

hakikisha bidhaa na huduma zinajiuza hata kwa macho ya nje na zinaubora wa kudumu

Tatua changamoto za wateja kabla hujawaza kupata pesa na faida

Toa huduma ambazo zinaendana na kasi ya ubora wa biashara zingine mara kwa mara

Kubadilika kwa msimu

Hakikisha kuwa unaujua kiundani msimu uliopo kama unafanya biashara ya muda mfupi au muda mrefu

Mfano miripuko ya magonjwa, jua kuwa kuna muda magonjwa yatapita!

Kwahio fanya biashara ya kudumu na kama unataka ya msimu kuwa makini na fatilia taarifa kwa kina ili usiingie katika hasara

Kubadilika kwa sera za nchi

Kama ni muwekezaj wa nje, tafuta nchi yenye sera zinazodumu na kueleweka

Na kama ni mfanyabishara wa ndani ya nchi fatilia mara kwa mara mabadiliko ili ujiandae kabla ya madhara!

Kufanya biashara kwa mazoea 

Hapa zingatia kuweka malengo mapya ya biashara yako

Jielemishe mara kwa mara na nenda na wakati

Jua kuwa tupo katika Dunia ya kasi ya teknolojia hivo mambo yanaenda kasi sana

Na wewe unapaswa mara kwa mara kujua wateja wanataka nini kwa wakati huo na haraka ufanye vile inapaswa

Kukua kwa Teknolojia 

Lazima ujifunze kwenda na wakati! Usilazimishe kubaki nyuma ya maendeleo ya techolojia

Utakosa wateja wengi sana kwa kufanya biashara kizamani, hivo lazima ujue namna ya kuuza mitandaoni pia!

Tumia teknolojia kama njia ya kukua kibiashara usiwe nyuma sana

Tamaa ya mafanikio ya haraka 

Lazima uwe mvumilivu na Ipe muda biashara kukua kwa kuweka malengo ya biashara ya muda mrefu ili uweze kuona matunda yake

Usiwe na haraka wala kutaka kukua haraka haraka kwani lazima utachoka na kuishia njiani

Lakini pia fanya biashara unayoipenda kupitia kipaji, taaluma au ujuzi wako ili ikusaidie kuifanya kwa mapenzi na bila kuchoka haraka hata mambo yanapokuwa magumu

Ukosefu wa uzoefu 

Kama Huna uzoefu wa biashara unayofanya jitahidi kutenga muda mwingi wa kujifunza mambo mbali mbali kuhusu biashara yako na omba Ushauri kwa wazoefu

Kila siku jipe muda wa kufatilia mambo ya msingi ya biashara yako ili uwe na Elimu ya kutosha ya kutatua changamoto

Lakini pia kama una uwezo ajiri mtu mwenye uzoefu mzuri aweze kukusaidia kuendesha biashara yako

Unaweza kuweka msimamizi unaemuamini sana na mwenye uzoefu mzuri na  akakusiadia kuangalia na kukuza biashara

Lakini pia jitahidi kujifunza kupita yeye ili uweze kuijua biashara vema

Imani za kishirikina

Usikubali kuingia katika mtego huu, kataa kabisa kuamini katika uchawi kwenye biashara yako

Epuka kutumia dawa za giza, kama unaamini katika Mungu basi kwa imani yako mwenyewe omba Mungu wako

Pia endesha biashara kwa kutumia kanuni bora za biashara

Hitimisho

Biashara inataka mipango na mikakati, usikate tamaa maana changamoto nyingi huwa za kawaida tu kwa biashara yoyote ile Duniani

Unapaswa kujifunza na kuzikabili changamoto bila kuchoka kila mara maana kadiri biashara inavyokuwa Ndivyo utakutana na changamoto mpya na kubwa kila zaidi .

Share this article
Shareable URL
Prev Post

Mbinu za kupata furaha na amani katika maisha

Next Post

Mambo ya kuzingatia kukuza biashara yako

Comments 2

Acha Comment Yako

Read next

Huruhusiwi ku copy. Asante.