Dawa ya msongo wa mawazo ni muhimu kwa kila mmoja wetu, lakini pia tunahitaji dawa inayoweza kutibu na kujisikia ahueni katika nyakati ngumu za maisha na changamoto mbali mbali za kila siku.
Kuna ile hali ya kuhisi kama kuchanganyikiwa, kukosa amani, kukosa raha, kuwa na hasira, kujihisi kama mwili wako haupo pamoja na nafsi yako nk.
Hali hii huweza kusababisha madhara makubwa Katika afya kama maradhi ya moyo, kuwehuka, lakini pia madhara kwa maisha ya muhusika wakati mwingine jamii kwa ujumla.
Kuna watu hufikia maamuzi ya kujitoa uhai katika maswala ambayo wangeweza kuyafumbua, lakini wapo wanaodhuru watu wengine na kuishia kupata kesi na kuharibu maisha yao.
Msongo wa mawazo unaweza kuwa wa muda mrefu au muda mfupi kulingana na aina ya changamoto.Pia soma namna kusahau mambo ya nyuma.
Mara nyingi msongo wa mawazo husababishwa na mambo ambayo yana nafasi kubwa ya kuepukika au kusuluhika.
Msongo wa mawazo unaweza kusababishwa na mambo mengi kama vile,
biashara kwenda kombo, changamoto za kazini, changamoto za mahusiano, ndoa na familia, changamoto za masomo kama kukosa ada na mambo mengine mengi.
Baadhi ya msongo wa mawazo huweza kutibika kwa njia mbalimbali kama
- Kuzungumza na mtu aliyekusababishia tatizo na mkafikia muafaka mzuri
- Kukubali uhalisia kuwa kuna mambo hayabadiliki na unapaswa kuyapokea
- Kuomba Msaada kwa watu wengine kama changamoto ni zakifedha
- Kupanga ratiba zako upya kwa changamoto za kazi na kutumia muda wako vizuri
- Kupanga bajeti zako na kufanya mambo ya msingi zaidi kabla ya matumizi mengine
- Kutafuta wataalamu katika mambo ambayo huwezi kufanya na yale yanayohitaji umakini
- Kupanga upya malengo yako na kuyarahisisha.
Unapokuwa katika msongo wa mawazo na kabla hujaendelea kuumia au kuumiza wengine unapaswa kujua kuwa,
Mosi “hakuna tatizo lisilo na tiba,”
Pili “una uwezo wa kukabiliana na tatizo lolote na kuleta suluhu bila madhara yoyote kwako na kwa mtu mwingine,” hivyo unapaswa_
1. Kutafuta na kutambua chanzo cha msongo wa mawazo yanayokusumbua kwa kina zaidi na
2 Ilazimishe akili yako kuwaza Sana mbinu ya kutatua tatizo bila kuleta madhara kwani ufumbuzi wa matatizo upo katika akili zetu.
Kuna mambo mengi Unayoweza kufanya unapokuwa katika hali hii ya msongo wa mawazo itakayo kusaidia kujua chanzo kwa kina na kuifanya akili ipate suluhuhisho, dawa kubwa ya haraka ni
KUTEMBEA UMBALI MREFU KWA MIGUU
Kutembea umbali mrefu inasaidia kuifanya akili yako kufanya kazi zaidi na kutafuta suluhu ya changamoto zako,
Itakufanya uwaze sana tatizo lako na kuna muda unaweza kujiona kama Huna tatizo kabisa.
Kadiri unavyotembea Ndivyo akili hufanya kazi na utaanza kuona njia mbali mbali unazoweza kutumia kutibu tatizo lako
Pia unapata ahueni kupitia nguvu inayotumika katika matembezi yako na,
Inakufanya ujisikie kama umetua mzigo mkubwa moyoni wako.
Mbinu zingine za kuondoa Msongo
Haijalishi unapitia changamoto gani kubwa kitu cha kwanza jua kuwa haupo peke yako!
Watu wengi wanapitia mambo mengi makubwa zaidi lakini kwa muonekano wa nje unaweza kuhisi wamekamilika.
- Hivyo kamwe usiwaze kujidhuru wala kudhuru mtu kabisa bila kujali uzito wa tatizo lililopo.
Fanya hivi kupunguzaa na kuondoa kabisa msongo wa mawazo
- Ondoka eneo la tukio, kama umekaa sehemu na mtu au mazingira yaliyosababisha msongo wa mawazo
- Tembea umbali mrefu kwa miguu, kila unapoona hali ya msongo nenda matembezi
- Ongea na mtu mwenye busara, tafuta mtu zungumza nae hii itakusaidia kuona umetoa uchungu moyoni
- Fanya kitu kinachokutoa jasho sana kama mazoezi ya viungo na kazi za nyumbani
- Jitenge kwa muda, tafuta mahala unapoweza kuwa mwenyewe kwa muda ili upate muda mzuri wa kutafakari
- Usimwambie kila mtu, chagua watu wa kuongea nao wenye Msaada na epuka kila mmoja kujua hali yako kwani wengi hufurahia matatizo ya wengine
- Jilazimishe kufanya kitu unachokipenda zaidi, kama vile kuogelea, kusikiliza muziki, kucheza games, kusoma majarida kama forbes
- Jichanganye eneo la watu wengi, kama sokoni, stendi,vijiweni, pembezoni mwa bahari, hapo utapata nafuu na kukukumbusha thamani ya maisha
- Pumua kwa nguvu mara kwa mara na kunywa maji mengi, hii hukufanya upate nafuu kwani unatoa nguvu iliyokubana kwa ndani
- Jiambie mara kwa mara kuwa changamoto uliyonayo ni ya muda mfupi na kila kitu kitakaa sawa
- Pumzika muda mwingi na kupata usingizi wa kutosha
- Kuwa karibu na familia au watu uwapendao zaidi
- Meditation mara kwa mara kwa kutuliza akili yako na kuingia ndani ya akili yako.
Mambo ya kuepuka unapokuwa na msongo wa mawazo
- Epuka kutumia kilevi cha aina yoyote
- Epuka kuendesha chombo cha moto
- Epuka kukaa karibu na silaha yoyote
- Epuka matumizi ya mitandao ya kijamii kwani hukufanya kuhisi hujakamilika kwa kuangalia maisha ya wengine ambayo pia sio maisha halisi
- Epuka kuzungumza na kila mtu matatizo yako
- Epuka kuomba Ushauri kwa mtu ambae hana uzoefu wa kutosha wa matatizo unayopitia
- Epuka kulinganisha maisha yako na maisha ya mtu mwingine aliyekuzidi.
Hitimisho
Huwezi kuepuka changamoto na matatizo ya kila siku kwani maisha yana kila sababu za kukufanya uumie,
Ila unaweza kujizuia namna unavyopokea mambo na taarifa mbali mbali katika mtazamo Chanya.