Kiwango cha umasikini huanzia kitandani
Kiwango cha umasikini ni kipimo kinachokuonesha hali ya umasikini uliyonayo
Ukitaka kujua kiwango cha umasikini wako anza na kitanda unacholalilia
Ukiwa hapo kitandani fanya tathmini ya kitanda chako, godoro, mto hata mashuka unayotumia!
Kisha geuza macho angalia juu ya paa la nyumba yako au yenu
Endelea kuangalia mazingira ya chumba chako kizima yakoje
Halafu inuka nenda nje ya chumba na kagua mazingira ya vyumba vingine na eneo lote kuzunguka nyumba
Malizia kwa kuangalia majirani wanaokuzunguka
Nyumba zao, maisha yao na mazingira yao yote.
Fanya maamuzi kuanzia kitandani
Ili uweze kubadili maisha yako jifunze kujipa hamasa kupitia kitanda chako
Kama unaona uvivu kuinuka na kuchukua hatua yoyote ya kubadili maisha yako basi anza na kitanda chako
Jiulize hivi kitanda changu kinasapoti niendelee kulala? au kinanihamasisha niinuke nikapambane?
Kuna muda watu huweza kulala sana na kupotezea kabisa kufanya jitihada za kujikwamua wakati huo huo vitanda vyao vinawahimiza kuamka
Unakuta watu wanaamua kukaa nyumbani kwao bila kazi ikiwa nyumba yao inawapa ishara za kupambana
Unalazimisha kukaa bila kuhangaika ikiwa majirani zako na mazingira yanayokuzunguka yanakuonesha kabisa fanya jambo!
Hakuna nyumba mbaya wala mazingira mabaya
Endapo umeridhika na kitanda chako, chumba na mazingira yako kutoka moyoni basi endelea na kile unachoona ni sahihi
Lakini kama kitanda na kila kinachokuzunguka kinakuhimiza kujituma zaidi basi tumia hio kama Hamasa yako.
Geuza kitanda kuwa hamasa
Kama unaona uvivu wa aina yoyote basi tumia kitanda chako kama hamasa mpya
Maana asilimia zaidi ya 70 kitanda huonesha kiwango cha umasikini ulionao
Hapa sisungumizii kitanda cha ndugu yako! au nyumba ya ndugu yako!
Namaanisha kile ulichonunua wewe kwa pesa halali ya jasho lako
Au kile ulichokulia katika nyumba ya kwanza ya familia yako
Simaanishi kitanda cha gharama ulichonunuliwa na mtu mwingine yoyote
Wala kitanda unachotumia mahala ambapo hapahusiani na nyumbani kwako au kwenu.
Mzingira yako ni hamasa
Aina ya chakula unachokula kwa siku, mavazi unayotumia,mfumo mzima wa maisha na kila kinachokuzunguka
Vinatosha kuwa hamasa katika kupambana kwako
Usikubali kuridhika ikiwa vitu vyote vinakuonea huruma!
Kwanini uridhike kwa mlo mmoja usio na afya kwa siku?
Usije kuridhika kwa kuvaa nguo za mtumba kila siku!
Unawezaje kutuliza akili ikiwa hata maisha ya hapo unapokaa unaogopa kuleta mgeni kwa kuona aibu?
Aina ya marafiki zako ni hamasa kubwa
Marafiki ulionao wanatosha kukufanya uinuke na kufanya jambo
Kuwa na marafiki ambao hawawezi kukusaidia hata shilingi laki 1 ya haraka inapotokea tatizo kubwa hilo ni tatizo lingine!
Yani wote wameajiriwa au wanafanya kazi za malipo ya posho!
Wale ambao hawana kazi na wanashinda vijiweni!
Marafiki ambao hawana Ushauri wowote zaidi ya kushabikia mpira na starehe
Usikubali kuwa na rafiki ambae hawezi kuwa kukupa mawazo chanya ya maendeleo
Yule ambae kila siku anaishi kama jana, hajui afanye nini au abadili nini
Kataaa ukaribu na mtu ambae hajawahi hata kuwaza mafanikio makubwa wala mbinu za kujikwamua
Tengeneza urafiki na mtu mwenye kufikiria mbali na anaejua nini anataka katika maisha yake hata kama leo hii bado hana chochote.
Ukoo wako ni hamasa zaidi
Ikiwa upo katika ukoo ambao hata matatizo kama misiba na maradhi lazima mchangishane hio inatosha kukupa hamasa
Ukoo ambao kuna historia ya mtu aliye poteza maisha kisa kukosa pesa za matibabu!
Kama unajua ukoo wako hakuna aliye fanikiwa kufika mafanikio ya juu iwe Elimu, biashara hata kitu chochote basi pambana sana
Usibweteke ikiwa ukoo wako wote mkikusanya kila mnachomiliki haifiki thamani hata ya kuwalisha mwaka mzima bila kufanya kazi kabisa
Ndugu yangu familia na ukoo wako tu Vinatosha kukufanya uinuke na kuanza upya
Acha kuishi kimazoea na usikubali kabisa kuwa wa mwisho katika utafutaji
Ni bora utafute ukosefu kuliko kuacha kutafuta kabisa.
Maisha hayataki hamasa za nje wala motisha za watu wengine
Hao “motivation speakers” (wahamasishaji) sio kitu kitakufanya kubadili maisha yako
Ikiwa wewe mwenyewe huoni kitu cha kukupa hamasa kupitia maisha yako binafsi
Usipoteze muda kuhudhuria vikao na semina za kila siku kwa lengo la kutafuta hamasa
Vitabu unavyonunua kila mara sio sababu ya wewe kutajirika au kuanza utekelezaji.
Tumia maisha yako iwe hamasa kuu
Fanya mazingira yako kuwa sababu kuu na zenye uzito wa wewe kutenda na kutochoka kupambana.
Tengeneza chuki na kitanda chako
Kila unapoamka asubuhi au unapotaka kulala usiku jenga chuki na eneo unalo tumia kulala
Jiambie nachukia sana kutumia kitanda hiki, chumba au mazingira yako yote
Sema kwa hisia na uchungu kuwa utafanya kila unachoweza kubadilisha kila kitu kwenye maisha yako.
Jenga chuki na marafiki zako
Hao marafiki ambao umeona kabisa hawakufikishi popote
Wachukie! Sio kwa ubaya bali kwa mawazo chanya tu
Sema kuwa sitaki tena marafiki watakao nifanya nishindwe kimaisha
Na weka nia moyoni kuwa utakuwa miongoni mwa marafiki wanaojitambua na kujua nini wanataka hapa Duniani.
Hujaja Duniani kuwa msindikizaji
Usikubali kusindikiza wengine wewe sio bendera
Umeumbwa kwa kusudi maalumu na unapaswa kufanya kitu kupitia maisha yako
Hao unao waona wamefanikiwa kwenye maeneo mbalimbali sio watu maalumu sana
Hawajaumbwa tofauti na wewe
Kila mmoja ana masaa 24 kama mwingine kwenye siku yake
Wote tuna damu na maji Sawa na akili Sawa tofauti ni matumizi ya akili tu
Ukiondoa tofauti za kimaumbile ambazo hazihusiani na kufanikiwa,
Hivyo wewe hukuletwa kushabikia mafanikio ya wengine,
Wala kujimbembelezesha kwa wengine au kusujudia wengine kisa wamefanikiwa
Wote tunapaswa kuheshimiana tu na kuhakikisha kuwa kila mmoja wetu anafanya kwa uwezo wake kile alicholetwa Dunia kufanya.