Namna Unavyoweza kuacha tabia mbaya
Kuacha tabia mbaya imekuwa jambo gumu na changamoto kubwa kwa watu wengi
Kila mmoja wetu ana tabia yake mbaya ambayo imekuwa kama mazoea, anatamani kuacha ila anashindwa kabisa
Tabia mbaya inaweza kuwa inayojulikana au ile ya siri, inaweza kuwa inachukiwa na ndugu, familia, marafiki au hata jamii nzima
Lakini pia huenda wewe mwenyewe unaichukia hio tabia Ila changamoto ipo katika kuiacha moja kwa moja
Kuna muda unaweza kuacha kwa kipindi fulani ila baada ya siku, wiki au mwezi unajikuta unarudia tabia ile ile
Mfano tabia ya ulevi, tabia ya uasherati, kugombana na watu, tabia ya wizi, punyeto, hasira na kisirani pamoja na tabia nyingine nyingi
Tabia hizo zinaweza kuwa na athari mbali mbali kama kiafya, kiuchumi, kikazi, kifamilia na athari nyingine
Ambazo huweza kuchochea mambo mengi mabaya na yenye majuto makubwa katika maisha yako moja kwa moja au jamii kwa ujumla
Zifuatazo ni baadhi ya mbinu unazoweza kutumia kuacha tabia unayoichukia sana na kuwa mtu mpya
- Jua chanzo cha tabia yako mbaya
- Orodhesha hasara (madhara) ya tabia mbaya usiyotaka na faida za tabia nzuri unayotaka
- Tafuta mbadala wa tabia yako mbaya
- Badili mazingira ya tabia yako mbaya usiyoipenda weka uzito na ugumu wa kufanya tabia mbaya na weka mazingira mepesi ya kuvutia ya tabia nzuri mpya
- Dhamiria na kuwa na imani
- Badilika kidogo kidogo
- Usimwambie mtu wala kutangaza mabadiliko yako
- Jipe muda na usirudi nyuma
Jua chanzo cha tabia yako mbaya
Kabla hujaanza kutafuta namna ya kubadilika, anza kutafuta chanzo cha tabia uliyonayo, siku zote kujua chanzo cha tatizo ni nusu ya tiba ya tatizo lenyewe
Mfano tabia ya ulevi kila unapojaribu kuacha unagundua kuwa kuna rafiki zako hukushawishi kwa namna mbali mbali
Na kujikuta unarudia, au pengine unaishi karibu na maeneo ya bar na hizo sehemu wanazouza vilevi
Au mfano mwingine tabia ya kutumia pesa vibaya na kukosa akiba chanzo utagundua labda unatembea na pesa nyingi mfukoni
Hivyo kushawishika kununua kila unachokutana nacho njiani
Hata kwa tabia nyingine yoyote tafuta chanzo chake na usijiongopee kabisa kuwa muwazi na moyo wako ufunguke kabisa
Kisha andika vyanzo vyote kwenye karatasi na jihakikishie hujaacha kitu
Orodhesha(madhara) ya tabia mbaya usiyotaka na faida za tabia nzuri
Fanya kwa uwazi kabisa wala usijidanganye, andika ni mara ngapi umepata hasara kutokana na tabia yako mbaya unayoichukia
Hata kama bado hujapata madhara ya moja kwa moja
Angalia mifano ya watu waliopata hayo madhara na andika yote mfano tabia ya uzinzi na uasherati mwisho wake ni maradhi ya kudumu kama HIV
Tabia ya udangaji mwisho wake ni kupigwa, kuuliwa, kudhalilishwa kingono na maradhi mengi yasiyotibika
Pia tabia ya kutumia pesa vibaya mwisho wake ni umasikini
Kisha andika faida za tabia unayotaka kuwa nayo mfano tabia ya kutunza pesa ni kupata mafanikio
Kuacha udangaji ni kuepuka maradhi, tabia ya kuacha punyeto ni kuwa na viungo vya uzazi imara na faida nyingine zile zinazokushawishi kuacha tabia mbaya
Tafuta mbadala wa tabia yako mbaya
Ukishajua chanzo, faida na madhara sasa jiulize unahisi ikiwa utaacha hio tabia,
Je utafanya kitu gani kingine ambacho hakitakufanya urudie tabia ya awali bila kujiumiza wala kukufanya utamani tabia ya mwanzo?
Chukulia mfano tabia ya uasherati na punyeto ni kutafuta mwenza mmoja mwenye vigezo unavyopenda wewe atakae kufanya usihangaike tena
Au tabia ya ulevi unaweza tafuta mbadala wa kunywa aina nyingine ya kinywaji ambacho hakina kilevi kabisa kama soda au juice
Hivo hivo kwa tabia nyingine zote tafuta mbadala kwanza ili ikusaidie kuacha tabia mbaya ya awali,
Bila kujiumiza wala kuwa na msongo mkubwa wa mawazo na matamanio ya kurudia tabia ile ile
Badili mazingira ya tabia yako mbaya usiyoipenda, weka uzito na ugumu wa kufanya tabia mbaya na weka mazingira mepesi yakuvutia ya tabia nzuri mpya
Hapa sasa kwakuwa ushajua chanzo cha tabia yako mbaya na umeshatafuta mbadala kabisa sasa unatakiwa kubadili mazingira yako
Kama chanzo ilikuwa marafiki badili ratiba za kuonana na marafiki zako au
Badilisha aina ya marafiki na tafuta ambao hawafanyi tabia mbaya ulizokuwa unafanya awali
Endapo chanzo kilikuwa kuishi karibu na maeneo wanayouza vilevi basi hama mtaa kabisa
Na kama huwezi kuhama tafuta Kitu cha kukuweka busy muda wa kufunguliwa bar unapofika
Kama chanzo kilikuwa ukosefu wa pesa za kumudu gharama za maisha na kukupelekea kuwa mdangaji au mwizi,
Utatakiwa kutafuta kazi hata kama ina malipo kidogo tu ili ikufanye ujue thamani ya kutafuta pesa zako za halali na thamani ya kujitegemea
Kwa kadiri utavyoona chanzo cha tatizo lako wewe mwenyewe
Amua kuwa dereva na daktari unaepaswa kujitibu kwa dawa zako mwenyewe katika kubadilika
Dhamiria kuacha tabia mbaya na kuwa na imani ya tabia nzuri
Katika hatua hii sasa weka nia ya dhati na amini inawezekana kuwa vile unavyotamani
Jenga picha ya kuwa tayari umeshakuwa na tabia unayotaka, ingia ndani ya akili yako na jione kama vile wewe sio mlevi tena, sio mdangaji tena, sio mwizi tena, sio mgomvi tena nk
Fikira namna utakavyokuwa na furaha pamoja na jamii inayokuzunguka baada ya kuwa na tabia mpya
Badilika kidogo kidogo
Siku zote ukitaka kuona jambo ni rahisi basi lifanye kwa hatua ndogo ndogo,
Usiwe na haraka wala usitake mabadiliko ya ghafla bali jipe muda maana ni ngumu sana kubadili kitu ulichokizoea zamani, lakini ukiamua unaweza
Kwahio fanya hatua ndogo ndogo kila siku mfano,
Punguza kuonana na marafiki, punguza mawasiliano na mashoga zako wanaokufanya ukadange nk
kunywa juice mara kwa mara japokuwa mwanzoni utaona kazi sana lakini kadiri siku zinavyozidi kwenda utaanza kuzoea na kufurahia juice badala ya pombe
Fanya hivo kwa tabia nyingine yoyote weka mabadiliko ya mbadala wako kidogo kidogo na usitumie nguvu kubwa sana kuondoa chanzo cha awali kwani itakufanya uone kama adhabu
Usimwambie mtu wala kutangaza mabadiliko yako
Acha watu wenyewe waone mabadiliko, kamwe usiseme kuwa sasa nataka kubadilika Ila onesha kwa vitendo pekee
Kama ukiitwa mahala kunywa pombe badala ya kusema nataka kuacha pombe sema mimi situmii pombe
Ukiitwa mahala kudanga badala ya kusema nimeacha kudanga sema mimi sio mdangaji
Kadiri watu watakavyokupa uhusika wa tabia yako usiyotaka kamwe usimeme nataka kuacha ila sema sijawahi kuwa hivo
Hii itakufanya moyoni ujione mtu mwingine na itakuwa kama ahadi ndani ya moyo wako
Na itawafanya wanaokuzunguka (jamii) kuanza kukutasfiri kwa namna unayotaka na kuacha kukuhusisha katika tabia mbaya za awali, Acha vitendo viongee
Jipe muda na usirudi nyuma
Hakuna mabadiliko ya ghafla, unapaswa kuwa mvumilivu na Kutokukata tamaa
Jipe muda kuzoea mabadiliko mapya na kama ukiona unashindwa kubadilika ni kawaida sana kurudia jambo usilolitaka mara kwa mara Ila,
Kadiri unavyojisahihisha na kujipa mazoea mapya ndivyo utajikuta unabadilika kidogo kidogo mpaka kuacha kabisa
Kila unapotaka kurudia tabia mbaya fikiria hasara zake kwa ukubwa na jiambie kama sitoacha hii tabia basi nitaishia kupata hasara zile zile
Jiambie na jione namna unapata hizo hasara kila mara unapohisi kurudia tabia ya awali na mwisho wa siku utajikuta umebadilika kabisa
Hitimisho
kuna watu wengi sana ambao walikuwa na tabia mbaya mno ambazo ziliwapa athari kubwa katika maisha yao
Ila waliamua kubadilika kabisa na sasa wanafanya mambo mzuri na makubwa Katika Jamii
Asitokee mtu akakuambia kuwa haiwezekani na usikubali kuamini kuwa huwezi, amini kila jambo lipo ndani yako na unaweza kuwa vile unataka.
Comments 1