Maana Ya Kufanya Mambo Madogo Kwa Ukubwa
Kufanya mambo makubwa sio lazima uwe na Rasilimali nyingi au uwezo mkubwa
Bali unaweza kufanya mambo makubwa kwa kutumia ulichonacho
Ikiwa imeshindikana kufanya mambo makubwa yaliyo ndani ya uwezo wako usiogope wala kuhisi kuwa haiwezekani
Angalia hiko kidogo unacho kifanya na kifanye katika hali ya ukubwa na ubora
Inaweza kuwa kazi ,biashara,Familia au jambo lolote katika maisha yako
Mfano ulitamani kuwa Muhasibu wa Benki fulani
Lakini sasa unafanya kazi katika taasisi tofauti au pengine unafanya kazi nje kabisa ya Fani yako
Sasa badala ya kuumia na kuona kama umepotea njia jitahidi kufanya kazi hio hio ambayo inakupa Riziki kwasasa
Na sio kuifanya tu bali ifanye katika kiwango ambacho ungefanya kama,
Ungekuwa katika Taasisi ile ile ya Benki uliyokuwa na tumaini la kuajiriwa kabla.
Pia chukulia ulitamani kumiliki kiwanda cha Maandazi lakini uwezo wako umeishia katika kuuza maandazi ya mtaji usiozidi Elfu tano
Badala ya kuumia sana hebu uza maandazi hayo hayo kwa ubora mkubwa na ubunifu wa hali ya juu na mapenzi makubwa
Kama ambavyo ungefanya endapo ungekuwa na kiwanda chako cha maandaazi au hata biashara nyingine yoyote.

Kama Hupati Unachopenda Penda Unachopata
Huu ni msemo rahisi na umezoeleka katika maisha yetu pia wenye maana kubwa katika harakati za kufikia mafanikio
Hasa kwa wale ambao bado wanajitafuta na wanaanzia chini kabisa kwenye malengo na ndoto zao
Ikiwa umetafuta kitu ulichokipenda lakini hujapata kabisa , basi unapaswa kuanza kupenda ulichonacho kwa wakati huo
Maisha na muda havimsubiri mtu yoyote ndio maana pia watu husema Maisha hayata kungoja ukigoma kwenda nayo!
Maana yake ni kuwa ikiwa utaona maisha hayajakupa unachotaka na ukaamua kukaa kusubiri
Elewa kua maisha na muda vitasonga mbele na wewe ndiye utakae baki nyuma.
Ulitamani kuwa Mwalimu lakini hujapata ajira Serikalini ila umepata nafasi ya kufundisha kwenye kituo fulani kidogo
Unatakiwa kufundisha katika kiwango ambacho ungefundisha kama ungeajiriwa Serikalini au katika sekta nyingine
Au ulitamani kuwa Daktari lakini unauza Duka la dawa ,badala ya kuona maisha hayana maana unapaswa kuhudumia hao wagonjwa wanaokuja hapo dukani
Katika ubora ambao ungewahudumia kama wangekukuta Hospitalini ndani ya uwezo na Rasilimali ulizonazo kwa sasa
Pengine hata unafanya biashara ndogo iwe yako au ya mtu mwingine hata kama haikidhi kiwango cha matumizi yako kwa sasa,
Unapaswa kufanya kwa mapenzi makubwa ,ubunifu na ubora wa hali ya juu kama ambavyo ungefanya endapo hio Biashara ingekuwa kubwa.
Mambo Makubwa Huja Baada Ya Kufanya Mambo Madogo Kwa Ukubwa
Bila kujali ukubwa wa malengo uliyonayo,
Amini kuwa hutoweza kufanya mambo makubwa ikiwa unashindwa kufanya mambo madogo ya sasa
Lazima ujifunze kufanya vitu vidogo katika ubunifu wa hali ya juu na hapo utaweza kuhimili kufanya mambo makubwa baadae
Usidharau kitu unachokifanya sasa hata kama hukipendi au unaona hakina maana katika maisha yako ya baadae
Amini kuwa safari ya maisha ni maandalizi ya muda mrefu na kila unachofanya sasa hakikuja kwa bahati mbaya bali kuna kusudi yake
Lazima uwe na jicho la kuelewa maana ya kila hatua unayopitia katika maisha ili kujenga Misingi ya maisha ya mbele.
Ikiwa utadharau ulichonacho hata kama ni kidogo basi kuna uwezekano wa kutopenda kikubwa cha baadae
Moyo wa kushukuru na kuridhika ni nguzo muhimu sana katika kutafuta mafanikio na amani ya maisha ya kila siku
Hivyo bila kujali uwezo au Elimu uliyonayo au muonekona wako na hata ukubwa wa malengo uliyonayo
Ikiwa tu hujafika au kupata unachotaka basi anza kuongeza mapenzi katika ulichonacho na kifanye katika ubora mkubwa na uaminifu
Kisha jitihada zako zitakufungulia njia katika kufikia mafanikio unayotaka hapo baadae na utaona faida ya hatua uliyoanza nayo
Simaanishi uridhike na kuacha malengo yako La hasha! Nina maana jenga mapenzi na unachofanya huku ukipambana kupata kilicho bora zaidi .

Nyenzo Za Mafanikio
Katika mafanikio unapaswa kuzijua nyenzo hizi na zitakusaidia sana kuweza kufurahia safari yako ya maisha na mpambano ya kila siku
- Ubunifu
- Uaminifu na uadilifu
- Heshima
- Nia na mapenzi ya dhati
- Uvumulivu
Ubunifu
Hii ni nyenzo muhimu zaidi katika maisha na mafanikio ya kila mmoja , nyenzo hii inatumika katika maeneo yote
Inaweza kuwa katika mahusiano, Biashara ,kazi na hata maisha ya muingiliano wa kila siku na kila mtu
Ukitaka kufanikiwa bila kujali unachokifanya basi lazima uwe mbunifu iwe kwa jambo lako au hata jambo la mtu mwingine
Yani tafuta namna ya kuwa tofauti sana na watu wengine iwe wafanyakazi wenzako hata wafanya biashara wenzako na hata washindani wako kwa ujumla
Iwe unafanya kitu unachokipenda au usichokipenda jua tu kuwa ubunifu utakusaidia kutimiza malengo yako ya sasa na hata baadae.
Uaminifu na uadilifu
Uaminifu ni silaha kubwa katika maisha yako yote hata kama unahisi huonekani jua tu kuwa unapaswa kutenda mema bila kujali kitu unachokifanya
Epuka hali ya kuhisiwa vibaya na kuwekwa katika kundi la watenda maovu hata kama unafanya jambo kwa siri
Ukiwa muaminifu na muadilifu bila kujali kitu unachofanya itakufungulia fursa nyingi sana kwa watu wanao kuzunguka
Itakujenga na kukupa nafasi ya kupewa kipaombele katika mambo mengi ambayo kimsingi yanaweza kuwa chachu ya kufikia malengo unayotaka.
Heshima
Ni nyenzo muhimu katika mafanikio na maisha kwa ujumla hata kama unafanya kazi mbaya au umri wako ni mkubwa kuliko viongozi wako
Unapaswa kuheshimu kazi na watu bila kujali ubaya wake wala nafasi zao iwe umewazidi vyeo hata Elimu au uzoefu
Jua kuwa mafanikio yako yapo mikononi mwa wengine na wanaweza kuwa na mchango wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja
Hivyo kitu cha msingi ni kujenga Heshima kwa kazi yako au wanaokuzunguka hata kama huwapendi
Heshimu kazi yako na fata ratiba zote kama inavyopasa , bila kusahau kumuheshimu bosi wako na wote wanao kuzunguka
Jenga heshima kwenye biashara yako hata kama bado ndogo na huoni faida yoyote bila kusahau wateja wako na wasikilize maoni yao
Lakini pia unapaswa kuheshimu kila mmoja na jamii kwa ujumla bila kujali umri ,cheo wala muonekano na mafanikio ya mtu kwa sasa
Heshimu pesa unazopata na zitunze kwa malengo hata kama unapata pesa ndogo sana jitahidi kuheshimu kila senti.
Nia na mapenzi ya dhati
Kama utakipenda kitu kutoka moyoni hata kama huna mpango nacho kwa baadae itakusaidia sana kukupa fursa unazotaka
Penda unachofanya hata kama unaona hakina maana kwa sasa ila kama kinakupa faida fulani unapaswa kuwa na mapenzi nacho
Ukikipenda kitu na kuweka nia nzuri katika utendaji wake itakusaidia sana kukifanya katika ubora na ubunifu
Ukifanya katika ubora na ubunifu pia itakusaidia kujenga mvuto na kuvutia wengine kisha utaonekana na utapendwa na hapo utafungua mlango wa fusa mpya
Uvumilivu
Kitu chochote kinataka muda wa kutosha ili kiweze kuzaa matuda unayotaka mfano ukilima huwezi kuvuna siku moja lazima uwe na subra wakati huo huo,
Utapaswa kuilinda na kuihudumia mbegu kwa mapenzi na usahihi mkubwa ili iweze kukupa mazao unayotarajia
Kwahio hata katika mambo mengine lazima ujifunze kuwa na subra na uvumilivu wa hali juu ili uweze kufanikiwa na kutimiza malengo yako .
Mafaniko Yamejificha Katika Mambo Madogo Madogo
Usiumize kichwa sana kutaka kufanya mambo makubwa ambayo huna uwezo nayo wala usipoteze muda kungoja upate ndio ufanye
Bali unaweza kuanza na ulichonacho hata kama ni kidogo sana na ukafanya katika ubora mkubwa kama ambavyo ungefanya endapo ungekuwa na kila kitu
Sio lazima iwe vifaa vingi au pesa kubwa, mfano unataka kumiliki kiwanda cha sabuni lakini kwa sasa unatengeneza sabuni nyumbani
Hio pekee inatosha kukupa mafanikio kama utetengeneza sabuni zenye ubora kwa kutumia hivo hivo vifaa na ujuzi wako
Sio uchakachue sabuni kwa ajili ya kuongeza faida huku una haribu jina la biashara yako hapo baada ya muda utatafuta mchawi na hutompata
Tengeneza sabuni za ubora mkubwa kama ambavyo ungetamani biashara ya kiwanda chako cha baadae iwe
Na linda chapa ya bidhaa zako kuanzia chini kabisa hata kama utapata faida ndogo
Au chukuli mfano wewe ni Fundi nguo ila huna wateja wengi wala vifaa vya kisasa lakini una ujuzi mkubwa wa kushona nguo
Badala ya kusubiri uwe na vifaa ndio ufanye kwa ubora unaweza tumia ujuzi wako kwa kushona vizuri ndani ya uwezo wako
Kumbuka wateja wana tabia ya kuambizana na kuona ubora au ubovu wa huduma yako kwa mara ya kwanza kabisa.
Usidharau mambo madogo madogo
Usidharau jambo hata kama ni dogo , kama utaweza kujenga misingi imara katika jambo dogo basi hata jambo kubwa utaweza kulihimili.
Walio fanikiwa katika maeneo mbalimbali hawakufanya mambo makubwa ghafla wala hakuna muujiza ambao walitenda
Ila waliona udhaifu na mapungufu yaliyopo katika maeneo ya wengine kisha wakabuni mbinu za kuja na utofauti bila kusahau ubunifu kidogo
Kisha wakazipa thamani kazi na biashara zao na mwisho wakaona mafanikio kwa kutumia mambo hayo hayo yanayodharaulika kila siku
Hakuna muujiza katika maisha wala mtu maalumu kuliko wengine ni vile tumetofautiana katika uwezo wa kuona fursa , matumizi ya akili na kusudi la kuumbwa.
Muda Haurudi Nyuma

Ikiwa utagoma kwenda na muda elewa tu kuwa hata wenyewe hauto kusubiri kila siku kuna pambazuka na usiku unaingia!
Epuka kuendelea kusubiria utimilifu yani kungoja upate kila kitu ndio ufanye jambo kwasababu utajikuta unapoteza muda na pengine usiweze kabisa
Jitahidi kuangalia ulichonacho na kifanye hivo hivo na baada ya muda utajishukuru wewe mwenyewe kwa kuanza mapema
Muda haujawahi kusimama na wala muda hauna kitu cha kupoteza kamwe
Ila sisi Wanaadamu ndio tunapaswa kukimbizana na muda maana hatuna umri mrefu wa kuutumikia muda.
Maisha yetu yana ukingo baada ya muda fulani lakini pia uwezo wa kufikiri na kutenda vina muda wake wa kuisha matumizi
Kuna wakati ulikuwa mtoto, ukawa kijana na utakuwa mzee hivyo basi inawezekana hata usifikie uzee na ukaondoka Duniani Mapema
Swali ni je utafurahia kuwa mzururaji Duniani na msindikiza wengine kisa uhaba wa Rasilimali ikiwa ulikuwa na uwezo wa kufanya kitu kisha kuacha alama?
Kimbizana na muda bila presha kubwa ila tu jitahidi ufanye kitu hata kama ni kidogo katika ubora mzuri na amini kuwa inawezekana.
Namna Ya Kufanya Mambo madogo Katika Ukubwa
- Andaa wazo lako unalolimudu
Wazo lolote unalotaka kutekeleza liandae na kuwa na uhakika kuwa unaliweza na kulimudu
- Panga malengo makubwa
Ndani yako jione wapi unataka kufika kupitia wazo lako na usiogope ukubwa wa malengo hata kama huna kitu kwa sasa
- Weka mikakati yako
Lazima uwe na mipango na mikakati ilinyooka hata kama hutoifanya au kuitekeleza kwa sasa
- Fanya uchunguzi kwa wengine
Walio kutangulia na angalia kama kuna udhaifu gani ambao unaona kabisa ukiziba hayo madhaifu basi jambo lako litakuwa kubwa zaidi
- Angalia ulichonacho
Angalia Rasilimali zako na zichunguze namna gani na kwa njia zipi zinaweza kukufaa katika kutekelezaji wa wazo lako kwa ubora kwanza bila kujali ukubwa wa malengo
- Anza na ulicho nacho kwa ubora
Usifanye uchakachuaji kabisa hata kama una haraka ya mafanikio, Rahisisha malengo lakini kwa njia ya kubaki na ubora jenga msingi na chapa imara kuanzia chini na mwanzo kabisa
- Endelea kujifunza vitu vipya
Hata kama unahisi unajua kila kitu kumbuka kuwa Elimu haina mwisho na jitahidi kila mara kutafuta maarifa mapya yanayohusu kitu unacho kifanya
- Usiache kuwaza malengo yako makubwa
Kumbuka lengo ni kufikia malengo makubwa baadae hivyo kila mara jikumbushe kuwa unapaswa kufikia lengo lako kwa gharama yoyote

Mambo Ya Kuzingatia Unapofanya Mambo Madogo Katika Ukubwa
- Ubunifu na jitofautishe kwa wengine kwa kuangalia madhaifu yao madogo madogo kisha kujiongeza na kuyafanyia kazi
- Heshima na nidhamu ya hali ya juu kwa kile unachokifanya na watu wote wanao kuzunguka
- Uvumulivu na subra tambua kuwa mambo yanataka muda kwahio lazima uwe na malengo ya muda mrefu ili uweze kutimiza ndoto
- Ubora mkubwa, usifanye kama unalazimishwa ila fanya kwa mapenzi na jenga imani katika jambo lako hata kama kwa sasa halina matumaini yoyote
- Mikakati na kutoyumbishwa maana utakutana na changamoto nyingi sana jambo la kuzingatia ni kuwa usikubali kurudi nyuma
- Uaminifu mkubwa yani usifanye uovu hata kama hakuna anae kuona kumbuka kuwa ukiwa na Dhamira nzuri moyoni itaonekana hata kwa macho ya nje.
Hata Mbuyu Ulianza Kama Mchicha
Huo mti mkubwa wa mbuyu unao uona ulianza mbegu ndogo na ukachepua kama mchicha kwa miaka kadhaa kisha ukawa mkubwa na imara kama unavyoonekana
Haikuwa ghafla tu kukuwa na kuwa imara bali ilitaka muda kwa mizizi kujishikiza chini na mpaka kujenga misingi imara na kufikia ukubwa kama unavyooneka
Kwahio jipe muda na kubali kujitengenezea misIngi imara kuanzia chini kabisa bila kujali udogo ulionao kwa sasa wala ukubwa wa malengo yako
Ikiwa unafanya kitu hata kama ni kidogo ni bora kuliko kutofanya kabisa.
Faida Za Kufanya Mambo Madogo Kwa Ukubwa
- Inakujengea misingi imara Kuanzia mwanzo
- Inakupa hamasa ya kufanya mambo makubwa kuanzia chini
- Inakukuza katika chapa bora (brand) mapema na uhakika wa kufanikiwa mbeleni
- Inakuongezea ubora na ubunifu mapema na hapo ndio yalipo mafanikio
- Inakujengea misingi ya uvumilivu na uendelevu katika jambo lako
- Inakupa misingi ya thamani kwenye kitu unachokifanya
- Inasadia kukujenga katika uimara wa soko na misingi ya mafanikio makubwa mapema.
pkh8cf