You Can Win If You Want

Mbinu za kutimiza Malengo

kutimiza malengo

Malengo ni nini?

Malengo ni maazimio au mipango anayotarajia kutimiza mtu au kikundi cha watu katika kipindi fulani cha muda katika maisha yake (yao) kulingana na sababu maalumu

Mfano kupunguza uzito,kumaliza masomo,kufungua biashara,kuanza familia na mifano mingine mingi kulingana na hitaji la mtu au watu husika.

Aina za malengo

Kuna aina kuu mbili za malengo ambazo ni :

  • Malengo ya muda mfupi
  • Malengo ya muda mrefu

Malengo ya muda mfupi

Haya ni malengo ambayo huwa yanaanzia kati ya dakika moja mpaka kipindi cha miaka mitano, ambapo muhusika hudhamiria kutimiza jambo fulani ndani ya muda wa chini ya miaka mitano

Inaweza kuwa kutimiza ndani ya masaa kadhaa ,siku,wiki,mwezi ,mwaka au miaka kadhaa chini ya miaka mitano.

Malengo ya muda mrefu

Huwa ni yale ambayo hukusudiwa kutimizwa kuanzia miaka mitano na kuendelea ,mara nyingi malengo haya huambatana na uwekezaji wa muda mrefu.

kutimiza malengo

Makundi ya malengo

Unaweza kugawanya malengo katika makundi kama ifuatavyo

  1. Kiuchumi
  2. Kijamii
  3. Kielimu
  4. Kiafya
  5. Kikazi
  6. Kidini au kiimani

Kiuchumi

Haya huwa yanaambatana na sababu za kiuchumi mfano biashara,ujenzi,ununuzi wa kitu chochote nk

Asilimia kubwa huambatana na matumizi au uongezaji wa uchumi wa mtu au watu na yanayeweza kuwa ya muda mrefu au muda mfupi kulingana na azimio la mtu au watu fulani.

Kijamii

Kundi hili huambatana na jamii inayo mzunguka muhusika moja kwa moja kama vile kubadili tabia fulani

Kujenga mahusiano bora na watu ,kuhudhuria vikao na sherehe mbali mbali kujenga misingi imara na watu au jamii kwa ujumla.

Kifamilia

Haya huambatana na sababu za kifamilia kama vile kuoa au kuolewa, kupata watoto,kutunza na kulea familia na nyingine zinazoshabihiana na hizo

Kama ilivyo kwa malengo mengine haya pia huweza kuwa ya muda mrefu au muda mfupi.

Kiafya

Huambatana sababu za kiafya kama kupunguza uzito, kuacha matumizi ya vilevi, kuzingatia mlo kamili,kufanya mzoezi na mengineyo na pia huweza kuwa ya muda mrefu au mfupi.

Kielimu

Huendana na sababu za kielimu na kujifunza vitu fulani kama vile kusoma kitabu, kujifunza ufundi fulani, kuanza au kumaliza masomo ya kiwango fulani na kadhalika.

Kikazi

Hapa muhusika anaweza kuwa na azimio kama vile kutafuta kazi,kuongeza ubora wa kazi anayofanya,kuzidisha ubunifu,kupanda cheo nk

Kidini

Katika kundi hili huambatana na mambo ya Imani zaidi kama vile kuanza ibada,kumrudia mungu,kuishi chini ya maagizo ya dini ,kuokoka,kubadili dini na kadhalika na vile vile huweza kuwa kwa muda mrefu au muda mfupi.

Sifa za malengo mazuri

Kuna sifa kadhaa za ambazo zinapaswa kuambatana na malengo ili yaweze kutimia kama alivyokusudia mtu au watu husika kama vile:

  • Yenye muda maalumu
  • Yanayopimika
  • Yanayofikika
  • Yenye uhalisia
  • Yanayojieleza au kuelezeka
Yenye muda maalumu

Ni lazima malengo yawe na muda wa mwisho ili yatekelezeke na kufikika kiurahisi mfano ndani ya mwaka ,miezi,siku hata wiki

Endapo kukiwa na muda maalumu hufanya uharakishaji na uzingatiaji mkubwa zaidi na lengo huweza kutimia kama ilivyokusudiwa.

Yanayopimika

Yani ni lazima pia kuzingatia upimikaji wake ili kuweza kutimiza malengo au lengo kama ilivyoazimiwa na muhusika

Ikiwa yatapimika basi husaidia sana kuweza kufanya tathmini kwa baadae endapo lengo limetimia au halijatimia na kusaidia kujipanga upya kuongeza au kupunguza baadhi ya vitu.

Yanayofikika

Hili pia ni muhimu sana kwasababu inasaidia kuweka lengo kwa kuzingatia uhalisia uliopo ili kuepuka maumivu na majuto

Chukulia lengo kama kununua gari la milioni 20 ikiwa uwezo wako wa sasa huwezi kupata kiasi hiko cha pesa

Maana yake ni kuwa utajikuta unalazimisha kufanya mambo mabaya yenye majuto mbeleni au kujipa mawazo na maumivu yasiyo ya lazima kwa lengo ambalo hukutakiwa kulitekeleza kwa muda huo.

Yenye uhalisia

Lazima malengo yawe na uhalisia sio yale ya kusadikika ili yaweze kufikiwa kwa urahisi na haraka

Lengo kama kupata mwenza mwenye vigezo vyote unavyotaka linaweza kufikiwa ila lisiwe kwa muda unaotaka au isiwezekane kabisa

Kutokana na uhalisia wa maisha ,mazingira na watu. kwahio jitahidi unachotaka kutimiza kiwepo kwenye uhalisia halisi kwanza kabla ya kutekeleza.

Yanayoelezeka

Kwamba kuanzia mwazo mpaka mwisho yapo wazi unaona kabisa utaanzia wapi na utaishia wapi pia yanaoyoonesha mbinu za ukweli na hatua kwa hatua kufikika.

Faida za kuwa na malengo

  1. Husaidia kutoa dira na muongozo wa unachotaka kutimiza
  2. Husaidia kuonesha njia na hatua za kufuatilia unachotaka
  3. Huongeza hamasa katika ufatiliaji wa jambo
  4. Husaida kupima kiwango cha mafanikio na kufanya tathmini kwa ujumla
  5. Hukusogeza karibu na mlango wa mafanikio unayotaka
  6. Huongeza ari ya uzingatiaji wa jambo
  7. Huifanya akili kutafuta mbinu na njia mbali mbali za kufanikiwa

Jinsi ya kupanga malengo ili yafanikiwe

Zifuatazi ni hatua au njia zinazosaidia katika kupanga na kufanikisha jambo husika

  1. Jua unachotaka na jihakikishie moyoni

    Awali lazima ujue kipi hasa unataka kutimiza kabla hujaanza kufanya chochote

  2. Andika malengo yako

    Chukua kalamu na daftari na andika kila unachotaka kutimiza hatua kwa hatua na weka muda maalumu unaotaka kuyatimiza

  3. Vunja vunja malengo katika vipande vidogo vidogo

    Ili ikupe urahisi wa ufatiliaji kila siku bila kuchoka yani usilibebe lengo kwa ukubwa kama lilivyo bali lichambue katika hatua ndogo ndogo

  4. Weka mikakati na mipango

    Andaa mikakati ya wazi namna gani utafatilia lengo lako na maelezo yote kwa kina

  5. Weka nia na dhamiria

    Nia ikiwa kubwa na hamasa huwa kubwa zaidi,kwahio lazima uwe na nia ili uweze kupata njia ya kufanikiwa

  6. Anza ufatiliaji

    Kidogo kidogo na usitumie nguvu kubwa bali tumia akili zaidi,hakikisha kuwa kila siku unafanya kitu hata kidogo ndani ya lengo lako na anza mambo rahisi kwanza

  7. Pambana na changamoto usizikimbie

    Kila unapokutana na changamoto yoyote itafutie suluhu na usikubali ikushinde

  8. Pima kiwango cha mafanikio yako

    Kila unachofanya katika mikakati yako jitahidi kupima na kujua ni kwa kiasi gani umefanikiwa ili ikikusaidie kuongeza juhudi au kubadili njia unayotumia.

Mambo ya kuzingatia ili kufanikiwa na kutimiza malengo

  • Weka malengo yenye sifa kamili kama yenye uhalisia,yanayopimika,yanafikika,yawe na muda na yanayoelezeka
  • Kamilisha malengo na fanikiwa kuanzia akilini, kabla hujaanza utekelezaji jione ndani ya akili yako namna utakavyofanya na kumaliza kila kitu kwa mafanikio
  • Kuwa na imani katika malengo yako yani amini kuwa yanawezekana hata kama hujafanikisha chochote
  • Dhamiria na usikubali kukatishwa tamaa kwa sababu zingine zozote
  • Andika kila unachotaka na pitia ulichoandika kila siku kabla ya kulala au baada ya kuamka
  • Jifunze kila mara kuhusu unachotaka ili uwe na taarifa za kutosha na fatilia kila kitu kinachohusu malengo yako na yafanyie kazi kwa kiwango cha juu
  • Fanya tahtmini za mara kwa mara kujua kama unachofanya kitaleta matokeo chanya au unakosea mahala
  • Usizipe nafasi changamto zitakazojitokeza na fanya kila unachoweza kubaki kwenye lengo
  • Jitoe kwa kila kitu na fanya kila unachoweza kufanikiwa ikiwa lengo linahitaji watu,pesa ,malighafi,muda au kitu kingine chochote
  • Usirudi nyuma mambo yanapokuwa magumu bali ongeza hamasa na jitihada na ikiwa hali itakuwa ngumu zaidi jipe mapumziko mafupi na kisha songa mbele
  • Jitenge na mambo au watu watakaofanya ushindwe kutimiza malengo yako na andaa mazingira rafiki kwako na watu wenye mchango chanya.

Hitimisho

Nini tofauti kati ya malengo na mipango?

Malengo ni maazimio anayotarajia au kukusudia mtu au watu kutimiza katika kipindi cha muda maalumu
Lakini mipango ni mikakati,mbinu na njia anayokuwa nayo mtu au watu kwa nia ya kutimiza malengo

Malengo ya maisha ni nini?

Ni maazimio makuu ambayo yamebeba maana nzima ya maisha ya mtu au watu husika katika maisha yao yote watakayoishi duniani

Kwanini watu hawatimizi malengo?

Kuna sababu kama kutopanga malengo yenye sifa stahiki, kutojitoa na kutokuwa na dhamira,kuzembea utekelezaji na wakati mwingine kuchoka na kuishia njiani

Nini chakufanya unapohisi kukata tamaa

Kukataka tamaa ni hali inayomkuta kila mtu kutokana na changamoto anazo kutananazo lakini unapaswa kutafuta hamasa mpya kila mara ili kukupa nguvu

Share this article
Shareable URL
Prev Post

Jifunze kujiajiri

Next Post

Ajionavyo Mtu Nafsini Kwake Ndivyo Alivyo

Comments 1

Acha Comment Yako

Read next

Huruhusiwi ku copy. Asante.