You Can Win If You Want

Namna Ya Kufanya Maamuzi Sahihi7 Min Read

Namna ya kufanya maamuzi sahihi

Utangulizi

Maamuzi sahihi ni changamoto kubwa sana kwa watu wengi kwenye maisha yao ya kila siku kwenye utendaji wake

Watu wengi sana wamejikuta katika wakati mgumu linapokuja suala la uchaguzi wa maamuzi ya aina fulani

Kila mmoja ana haki ya kufanya maamuzi yake binafsi kwenye maisha bila kusukumwa na mtu mwingine

Uchaguzi wa maamuzi huambatana na aina ya maisha anayotaka kuishi mtu bila kuingiliwa na mtu mwingine.

Kuna nyakati unaweza kuwa umezongwa na machaguo mbali mbali ambayo yanahitaji maamuzi yako

Na hapo ndio changamoto huanzia kwani unaweza kujikuta unafanya maamuzi ambayo yanaweza kuharibu kabisa

Au hata kusababisha majuto makubwa sana kwa mtu mmoja au hata jamii kwa ujumla inayo zunguka

Maamuzi sahihi si suala la hiari bali lazima kwasababu ndio njia inayoweza kuleta ustawi mzuri kwa mtu na jamii

Haijalishi unataka kufanya maamuzi kwenye jambo gani,jambo la kuzingatia ni kufanya maamuzi sahihi.

maamuzi sahihi
Photo by cottonbro studio on Pexels.com

Sio Kila Maamuzi Magumu Ni Maamuzi Sahihi

Kuna wengi huchanganya kati ya maamuzi magumu na maamuzi sahihi wakizani kuwa maamuzi sahihi lazima yawe magumu

Ijapouwa wakati mwingine maamuzi sahihi yanaweza kuwa maamuzi magumu na yanayotaka ujasiri mkubwa

Lakini pia kufanya maamuzi sahihi sio lazima yawe yale magumu yanayoweza kuharibu mambo mengine!

Unapaswa kufanya maamuzi ambayo yapo katika njia sahihi bila kuegemea sababu zenye upendeleo au mazingira fulani

Maamuzi magumu yanaweza kuwa sahihi na yasiwe sahihi kabisa kutegemea na aina ya changamoto

Changamoto za maisha za kila siku ndio chanzo kinachohitaji maamuzi sahihi kwenye ufumbuzi wake.

Kuna Wakati Maamuzi Sahihi Yanaweza Kuwa Na Machaguo Zaidi Ya Moja

Nyakati zingine unaweza kujikuta maamuzi yote ya ufumbuzi wa jambo ni sahihi na yanafaa kutumika

Yaani unajikuta hujui haswa ushike kipi na uache kipi kwasababu kila moja lina faida zake ambazo unazihitaji

Hii inaweza kuwa aina nyingine ya changamoto kwa mtu au watu wanaotaka kupata maamuzi sahihi kwa wakati huo

Maisha yana machaguo ya aina nyingi sana na kila mmoja huchagua chaguo analotaka kwa mapenzi yake

Shida huja je, hayo machaguo ni sahihi kwenye maisha kwa ujumla au faida zake hudumu kwa muda kiasi gani?

Kuna maamuzi huwa mazuri sana kwa muda mfupi mno na mengine huwa na faida za muda mrefu kwenye maisha

Kuna yale maamuzi unaweza kufanya ukaona kama umeweza sana kwa wakati huo,

Lakini baada ya miaka kadhaa ukajikuta upo na majuto makubwa sana au umesababisha matatizo kwa wanao kuzunguka.

maamuzi sahihi
Photo by Leeloo The First on Pexels.com

Maamuzi Sahihi Hayaongozwi Na Hisia

Kuna wale ambao hufanya maamuzi yao kwa sababu ya hisia walizo nazo mfano furaha, huzuni NK

Na baada ya muda hugundua kuwa wamefanya maamuzi mabaya yenye majuto mengi na hasara nyingi sana

Hivyo basi suala la kufanya maamuzi linahitaji uwanja mpana sana na sio kitu cha kukurupuka wakati wowote

Ikiwa watu wangekuwa wanatuliza akili zao kabla ya maamuzi wanayo fanya Dunia ingekuwa sehemu salama zaidi

Hata viongozi wengi hususani nchini Tanzania kuna nyakati hukurupuka kufanya maamuzi ambayo huleta shida kwenye maisha ya Wananchi.

Wengine hufanya maamuzi kwa sababu ya kufurahisha watu walionao kisha huingia kwenye mtego wa majuto

Bila kusahau wale ambao hufanya maamuzi kwa sababu ya sifa wanazopewa na wapambe walionao

Na wale ambao hufanya maamuzi ili kukomoa wengine kwa sababu binafsi au chuki walizonazo

Halafu wale ambao hufanya maamuzi baada ya kutumia aina fulani ya kilevi kama pombe au bangi!

Wote hawa na wengine wengi hujikuta kwenye majuto sana baadae au hata maumivu kwao binafsi na jamii nzima.

Sababu Za Watu Kufanya Maamuzi Mabaya

  • Kutumia hisia zaidi ya fikra mfano wakati wa furaha hasira au hata huzuni
  • Kutaka kufurahisha wengine
  • Tamaa za muda mfupi
  • Wapambe au machawa
  • Kuomba ushauri kwa watu wasio sahihi mfano mitandaoni
  • Ubinafsi na kutaka kujipendelea
  • Starehe za muda mfupi
  • Mafanikio ya njia za mkato
  • Haraka na pupa
  • Ukosefu wa uzoefu
  • Ushawishi wa makundi na mazingira
  • Ushawishi wa rika na umri
  • Uoga na hofu ya kushindwa
  • Ubishi , ujuaji na kutokubali kushindwa NK.

Faida Za Maamuzi Sahihi

  1. Huleta matokeo bora ya kudumu na muda mrefu
  2. Huleta haki
  3. Huleta furaha ya kudumu
  4. Huleta amani na utulivu wa akili
  5. Huleta amani kwa mtu,familia na jamii
  6. Hujenga uwezo wa kujiamini
  7. Husaidia kujenga ustawi bora wa maisha
  8. Huongeza heshima NK

Changamoto Za Maamuzi Sahihi

  • Kutengwa
  • Kupoteza mahusiano na watu wa karibu
  • Kuchukiwa
  • Kukosa baadhi ya vitu
  • Msongo wa mawazo
  • Kutamani kukata tamaa
  • Maumivu wakati wa mchakato
  • Kuhisi hali ya kukosea na kujiona haupo sawa
maamuzi sahihi
Photo by Vincent M.A. Janssen on Pexels.com

Hatua Za Kufanya Maamuzi Sahihi

  1. Elewa tatizo au changamoto yako kwa undani

    Ili kufanya maamuzi sahihi lazima pia ujue tatizo lako kwa kina na uwanja mpana zaidi kwasababu husaidia kutoa ufumbuzi bora

  2. Ainisha machaguo ya ufumbuzi na maamuzi uliyo nayo

    Baada ya kujua tatizo lako sasa ainisha aina zote za maamuzi ambazo unazo na unazohisi zinaweza kuleta suluhu

  3. Ainisha faida na hasara za kila chaguo ulilonalo kwa kuzingatia malengo yako

    Kila mtu huwa na malengo kwenye maisha hivyo unapotaka kufanya maamuzi sahihi kumbuka malengo yako mara kwa mara na yahusishe kwenye maamuzi yako kwa kuangalia faida na hasara za maamuzi unayotaka

  4. Tafakari kwa kina

    Baada ya kuwa na uchaguzi wa chaguo moja, sasa jipe muda wa kuwaza chaguo lako kwa kina zaidi na jiulize kwanini umeamua iwe ivo

  5. Pima uzito na uwiano

    Angalia uzito wa uchaguzi wa chaguo lako na mengine uliyo yaacha kisha angalia na uwiano wake na jiridhishe kuwa hujakosea

  6. Tafuta taarifa mbali mbali kuhusu chaguo lako

    Unapaswa pia kuwa na taarifa za kutosha ili uweze kujihakikishia kuwa upo sahihi zaidi

  7. Vaa ujasiri na fanya kwa vitendo

    Baada ya kuwa na taarifa sahihi kuhusu uchaguzi wa jambo ulilonalo sasa vaa moyo wa ujasiri na fanya kwa vitendo

Mambo Yanayo Saidia Kufanya Maamuzi Sahihi

  • Malengo sahihi ,ukiwa na malengo kwenye maisha hasa yale ya muda mrefu husaidia sana wakati wa kufanya maamuzi kwenye changamoto za maisha
  • Kujua unachotaka kwa uwazi na upana mkubwa pia ni silaha ya kufanya maamuzi bora
  • Marafiki wazuri, ikiwa umezungukwa na marafiki wenye malengo na wanaojua nini wanataka kwenye maisha yao hasa zile ndoto zinazofanana na wewe husaidia wakati wa kufanya maamuzi
  • Utulivu wa akili,kama akili yako hupata muda mwingi wa kutulia na kuwaza kabla ya kufanya maamuzi pia huwa na msaada sana wakati wa kufanya maamuzi mema
  • Muda sahihi, kuna wakati maamuzi huendana na muda uliopo yani unaweza kufanya maamuzi fulani kumbe umepitwa na muda au umri wako
  • Mipaka ya maisha, endapo umejenga mipaka kwenye mambo kadhaa yanayogusa maisha yako huwa ni namna bora sana wakati wa kufanya maamuzi
  • Tabia njema , ukiwa na tabia nzuri kwenye maisha ni silaha kubwa sana wakati wa kufanya maamuzi sahihi wakati wa matatizo na changamoto
  • Uzoefu wa utatuzi wa changamoto za nyuma au hata kupitia watu wengine.

Kufanya Maamuzi Kwenye Uchaguzi Wa Machaguo Zaidi Ya Moja

Kuna kipindi unaweza kukwama kufanya maamuzi kwa sababu ya uwepo wa uchaguzi wa aina zaidi ya moja

Wakati huohuo unaweza kujikuta maamuzi yote yapo sawa na unayahitaji kwa muda mmoja kwa pamoja

Pengine unatakiwa kuchagua kimoja ila vyote vina uzito mkubwa zaidi na hapo ndio tatizo lingine hutokea!

Maana hujikuta unapitia wakati mgumu ziadi kuliko hata namna ulivyotarajia au kuliko changamoto yenyewe

Hivyo katika hali kama hii unapaswa kuzingatia zaidi faida za kudumu na zile za muda mrefu za maisha na umri au muda

Bila kusahau uzito zaidi wa chaguo lako na ugumu wa kupata tena kitu hiko kwa wakati mwingine,

Unaweza kutumia kanuni ya sababu faida na hasara ili kupata muongozo sahihi zaidi unapokuwa na hali hii.

Hitimisho Na Mambo Ya Kuzingatia Unapofanya Maamuzi

Ni muhimu sana kufanya maamuzi haijalishi ni mazuri au sio mazuri kulingana na mapenzi ya mtu lakini pia zingatia

  • Umri ulionao
  • Haki
  • Kipato chako
  • Wategemezi wako kama watoto au familia
  • Malengo ya muda mrefu na ndoto ulizonazo
  • Amani na kiwango cha furaha unayotaka
  • Mustakabali wa jamii nzima
  • Sheria za Dini na Nchi
  • Uhusiano na wengine.

KUMBUKA MAISHA UNAYOISHI SASA NI MATOKEO YA MAAMUZI ULIYOFANYA NYUMA.

Share this article
Shareable URL
Prev Post

Mbinu Rahisi Za Kufanikiwa Bila Kuchoka Sana7 Min Read

Next Post

Namna Rahisi Ya Kupata Mtaji Wa Biashara Kwa Wenye Kipato Kidogo5 Min Read

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Read next

Huruhusiwi ku copy. Asante.