Utangulizi
Maisha makamilifu ni swali ambalo kila siku hunijia akilini mara tu niamkapo na kugundua kuwa bado nipo hai kwa mara nyingine,
“Ninawezaje kuishi maisha kwa ukamilifu japokuwa mimi sio mkamilifu?”
Ninajua kabisa kuwa mimi Mwajuma Muhasu sijakamilika kabisa kwa maana Duniani hakuna Kiumbe kamilifu mbele za Mungu,
Ila Je? Kutokuwa mkamilifu ni sababu ya kuishi maisha yangu nusu nusu?
Sijakamilika kwa maana kuwa ,Ni kweli sina mvuto mbele za macho ya wengine
Wala sina kipato kikubwa kama wengine
Na wala sina cheo kikubwa kama wengine
Au hata sina tabia nzuri kama wengine
Au vyovyote vile nilivyo ila tu najua sio kiumbe mkamilifu mbele za wengine au kama wengine mbele za Mungu.
Ila licha ya madhaifu yote hayo bado naweza kuishi maisha makamilifu.
Kama ungepewa siku 30 pekee zakuishi Duniani je ungemaliza uhai wako kwa kufanya mambo gani muhimu zaidi?
Basi sasa ikiwa umepata jibu, anza kufanya mambo hayo kuanzia sasa hivi kwani ukweli ni kuwa hujui umebakisha muda gani kuishi Duniani,
Hupaswi kuweka maisha yako rehani wala kubetia uhai, usikubali kujutia ukiwa kaburini bali anza sasa na badili historia yako ya kesho.
Ukamilifu Sio Utakatifu
Kuna tofauti kubwa sana kati ya kuwa mtakatifu na kuwa mkamilifu vilevile kuishi maisha makamilifu!
Utakatifu ni mambo ya imani za Dini zaidi ambazo siwezi kuingia kwa undani,
Halafu ukamilifu maana yake ukamili wa maumbile na kiroho zaidi ambavyo kwa nijuavyo mpaka sasa ni kuwa hakuna mkamilifu na wote tuna mapungufu,
ILA
Maisha makamilifu maana yake ni kuishi kwa namna ambayo hutoacha majuto wala pengo lolote katika kila chaguo na maisha utakayoishi bila kujali kiwango chake
Kwa maana kuwa haijalishi utaishi miaka mingapi, kwa kipato gani wala utaishi wapi bado unapaswa kuishi kwa namna ambayo kama ukifa leo basi ufe ukiwa unatabasamu.
Ufe ukiwa huna deni na maisha uliyoishi wala maisha yasiwe na deni na wewe katika kila sekunde uliyotumia Duniani.
Kumbuka
Hakuna aliyekamilika ila kuishi maisha yasiyo kamili ni chaguo lako.
Usihusishe Kukosea Na Kuishi Kamili
Kukosea ni kawaida sana kwa kiumbe yoyote yule ndio maana bado tunasisitizwa kuwa hakuna kiumbe kamilifu na wote tuna mapungufu,
Ila hapa pia haihusiani kabisa suala la kukosea na kuishi maisha makamilifu kwa maana unaweza kukosea wakati wowote ule wakati unaishi maisha makamilifu.

Ninaogopa Sana Majuto
Moja kati ya udhaifu wangu ambao nimeruhusu kila anae changamana namimi ajue mapema kabisa basi ni majuto
Majuto ni kitu ambacho nilikipiga marufuku kwa miaka mingi sana na mpaka sasa ninaishi ndani ya falsafa ya ukamilifu pekee.
Adui yangu namba moja ni majuto na kamwe siwezi ruhusu anitawale wala kutawala maisha yangu kabisa.
Mara kwa mara nimekuwa nawaza nawezaje kuepuka kujutia mbeleni? Nifanye nini ili nisiache neno ningejua! au napaswa kuishi vipi ili nikifa niwe huru kwenye kifo changu?
Majuto Ni Mjukuu
Unajua kwanini wahenga wa zamani walitunga msemo huu?
Hata mimi sina jibu la wazi sana kitu gani haswa walimaanisha wazee wetu ila ninaweza tafsiri kwa falsafa zangu kama hivi….
Mjukuu ni mtoto ambae huzaliwa baadae sana kwa maana baada ya babu na baba au mama na bibi..
Hivyo mjukuu huzaliwa baada ya miaka kadhaa fulani mingi kiasi kupita na huja tayari ameshachelewa maisha waliyoishi wengine
Hivyo majuto pia ni macheleo ya mambo ambayo yalipaswa kufanyika kabla vilevile majuto huja baada ya kupitwa na mengi.
Nikiri tu kuwa Mwajuma Muhasu ninaogopa sana majuto kwa gharama yoyote ile ndio maana kila nipatapo nafasi yakufanya kitu basi hukifanya kwa ujuzi wangu wote.
Kabla sijalala kila siku hutumia dakika kadhaa kujihakikishia kuwa siku yangu nimeiishi kwa namna ambayo nimeridhika na sina shaka kabisa,
Ikiwa nitagundua makosa basi mara tu nikipata bahati ya kuamka tena basi nitahakikisha nasahihisha makosa yangu yote kabla sijaanza majukumu ya siku mpya.

Neno Ningejua Huja Baada Ya Safari
Mama yangu kipenzi enzi za uhai wake (Allah Ampe Kauli Thabiti) Aliniambia neno hili mara kadhaa kila nilipoenda kinyume na maagizo yake,
Licha ya upole wake uliopitiliza , Mama yangu bint Ramadhani Kitama ,Hakuacha kuniasa mara kwa mara nikoseapo.
Nikiri tu kwamba licha ya kuishi maisha mengi nikiwa mwenyewe,nikijiongoza na kujipangia maisha baada ya kukosa waangalizi wa karibu,
Maneno ya hekima ya marehemu mama yangu yamekuwa kama mwanga na tochi iangazapo kwenye kila giza ninalopita
Ndio maana mpaka sasa licha ya mengi mabaya na magumu niliyopitia bado ni binti imara sana ambae kila ninapokumbuka nyuma yangu..
Ninabaki kutabasamu kwa furaha na mara kadhaa hutokwa na machozi ya huzuni kwenye zile kumbukumbu zisizofutika.
“Ningejua ningefanya kile sasa nimechelewa!” Hakika Mama yangu aliweza sana kuondoa mwanae kujutia chochote hata kwenye mazingira magumu.
Ukitaka Kula Kondoo,Kula Aliyenona Itakusaidia Kuishi Maisha Makamilifu
Siongelei kondoo wa bwana mbele ya mchungaji wa kanisa fulani,
Wala siongolei kondoo wa bwana shamba yule pale machungoni!
Ninaongelea kondoo kwa maana ya maisha na kila unachofanya kila siku kwenye maisha unayoishi!
Machaguo unayochagua yanapaswa kuwa yaliyonona kiasi kwamba hayatakuachia shombo badala ya shibe.
Moja kati ya siri ambayo ninakupa leo hii wewe hapo kijana mwenzangu unaesoma makala hii niliyokuandalia ili kukutia moyo,
Usikubali kondoo dhaifu kwa maana atakupakaza shombo badala ya shibe takatifu.
Kondoo aliyenona kwenye maisha maana yake amua kufanya vitu vyenye mantiki sanifu, vinavyoacha alama kubwa na kubadili maisha kwa ujumla,
Fanya vitu hata kama ni vichache au vidogo lakini katika uyakinifu na ukubwa ambao kila atazamae aseme yes kweli kitu kimefanyika.
Haijalishi uwezo au uchumi wako wasasa, bado unaweza kufanya kwa namna ya undani na uzito mkubwa kuliko unavyodhani
Fanya kwa uyanikifu ili ikitokea umeshindwa kwenye jambo lako basi usimame na kusema ulifanya kila ulichopaswa kufanya ila tu haukuwa wakati wako wa ushindi,
Badala ya kujiwa akilini na neno laiti ningejua! kwani neno hili litakusumbua maisha yako yote.
Na kama ukishinda basi uwe umeshinda ushindi wenye kishindo kizito sawa na jitihada zako.
Thamani Ya Pesa Ni Ileile Hata Pesa Ikitupwa Chooni
Najua bado unajiuliza mambo mengi sana na pengine unaona kabisa Mwajuma Muhasu amedata sana leo,
Usijali twende sawa na taratibu sana kisha utanielewa mbele ya makala hii nzito na nzuri niliyokuandalia leo.
Unajaua kwanini unahisi kama nakuchanganya?
Kwasababu unajidharau hivyo ulivyo leo hii…unadharau kipato na maisha yako, unadharau biashara yako ndogo hata unadharau mazingira yako yote yanayokuzunguka!
Unajiona kiumbe aliyepotea katikati ya Dunia hii kubwa isiyo na chembe ya huruma kwa viumbe dhaifu na masikini,
Unaona kabisa kuwa huwezi kupiga hatua yoyote wala kufanya chochote kama ambavyo waliokutangulia wamefanya,
Unahisi kabisa kuwa kuna kila harufu ya upendeleo kati ya Mungu na wanaadamu wake, ambapo wachache walipewa mihuri ya mafanikio na wengine mihuri ya umasikini.
Pengine unahisi hata mimi Mwajuma ni miongoni mwa wale waliobahatika kuwa kundi la wenye mihuri ya mafanikio!
Hivyo unahisi naandika hadithi za kusadikika kwenye makala zangu na pengine unadhani sijui ugumu wa mapito ya maisha.
Lakini siku moja utafanikiwa kumjua Mwajuma Muhasu na hakika utashangaa sana au hata kulia sana ,kisha utasema kuna watu wenye mioyo ya dhahabu kuliko mifuko yao.
Kwakusema hayo naomba nikutoe hofu kuwa ,huyu anaeandika hapa anajua maisha na ugumu wa maisha nje mpaka ndani,
Unapaswa kuamini na kujifunza hiki kidogo ninachotamani kukufikishia na kisha kibadili maisha yako yote.
Chukulia Mfano Huu Mdogo Wa Pesa
Haijalishi pesa itakuwa kwenye choo cha aina gani ! wala haijalishi itaganda kinyesi kiasi gani! na pia haijalishi itatoa harufu kiwango gani bado itaitwa pesa,
Itagombaniwa kwakuwa ni pesa na inaweza kusababisha choo kivunjwe ili kuchukua hio pesa!
Unajua kwanini kuna matangazo kila kona ya watu wanunuao pesa chakavu na mbovu? au umewahi kujiuliza kwanini pesa hata iwe mbovu kiasi gani kamwe haitupwi jalalani?
Ukipata jibu basi tambua kuwa maisha yako ni zaidi ya thamani ya pesa.

Thamani Ya Maisha Yako Ni Zaidi Ya Thamani Ya Pesa
Sikia nikuambie kitu hapa, haijalishi unajionaje kwasasa hapo ulipo elewa kuwa thamani yako ni kubwa sana
Maisha unayoishi bila kujali yalivyo ,tambua kuwa yana thamani kuliko kitu chochote kile ukijuacho Duniani
Wengi hushusha au kupandisha thamani ya mtu kwakuangalia alichonacho {material} wanasahau kuwa vitu si chochote mbele ya uhai wa mtu.
Usicheke!
Najua unacheka sana kwamaana kila ukiangalia pembe za maisha yako unaona kabisa hazina thamani yoyote ile kwasababu huna kitu,
unajiona sawa na shilingi iliyodumbukia chooni na kamwe haina thamani inayoweza kufanya choo kivujwe ili itolewe!
Hapo unajisemea kuwa kama pesa haipotezi thamani ikiwa kwenye tundu la choo ! je kuna mtu anaweza kudumbukia chooni kufuata noti chache?
Au mpaka aone pesa zenye wingi kiasi chakuleta mabadiliko kwake kulingana na hali yake ya uchumi?
Na hapo unapata jibu kuwa wewe ni kama shilingi ambazo kamwe haziwezi kufuatwa au kusababisha choo kuvunjwa ii zitolewe nje!
Pesa Nyingi Zimeundwa Na Shilingi Moja
Upo sahihi kuwa thamani yako ni ndogo sana kama unavyoamini ila kumbuka hata pesa kubwa sana ndani yake ina shilingi nyingi ndogo ndogo,
Hivyo ikipungua hata shilingi moja kwenye zile pesa nyingi basi pia hata thamani ya pesa na jina la pesa hushuka chini pia!
Kusanya Shilingi Zako Ili Ziwe Na Thamani Kubwa
Mambo madogo madogo ambayo unafanya leo hii kwa kila sekunde moja inayopita ndio siku moja yatafanya yajulikane kama mambo makubwa!
Usijali sana kuhusu maisha unayoishi zingatia kuyaishi kwa ukamilifu wake ili hata siku ukiwa ndani ya choo basi uwe kama lile begi kubwa la hela ambalo litafanya choo kivunjwe ili litolewe nje,
Au litafanya watu wadumbukie bila kujali harufu ya kinyesi.
Nakuagiza kuanzia sasa nenda kaishi na tawala Dunia yako kwani unathamani sawa na yoyote mwingine mwenye uhai sawa wewe.
Kwanini Tunapaswa Kuishi Maisha Makamilifu?
inawezekana kila mmoja anaetamani kuishi maisha makamilifu anasababu zake ambazo haziwezi kulingana au kufanana na mwingine ila,
Kwa upande wangu ninasababu kuu mbili ambazo hunipa ujasiri wa kuepeuka majuto kupitia maisha yangu ambazo ni:
- Kifo ni fumbo
- uhai ni zawadi ya muda mfupi
Kifo Ni Fumbo
Hivi unajua kuwa kifo ni kitu pekee kikubwa zaidi ambacho kinaonesha ufundi wa Mungu aliyeumba viumbe hai pamoja na kifo chake?
Vipo vingi vikubwa zaidi vioneshavyo ufundi wa Mungu ila kwenye kipengele cha kifo aliweka siri ambayo licha yakuumba Binaadamu wenye mfano wake ila hakurusu wagundue kifo.
Kifo kingejulikana kwa namna mbalimbali basi huenda hali ya Imani juu ya Mungu mpaka sasa ingebaki asilimia 0%
Hapo hata wanasayansi nguli wameshindwa kabisa kufumbua fumbo juu ya kifo na mpaka sasa hakuna ajuae siku yake ya kufa,
Licha ya wote kuwa na uhakika wa kufa siku moja ,ila imebaki kuwa siku isiyo na jina kwa kila mtu aliyepo hai.
Suala la kufa haliepukiki kabisa kwa kiumbe hai yoyote yule haijalishi umri,kipato,jinsia wala cheo chake,
Mbaya zaidi kifo huja muda na wakati wowote ule bila kujali chanzo kitakachopelekea kifo cha muhusika fulani.
Kwamaana hii kama kifo ni ahadi ya mja na Mungu ambayo lazima siku moja itimizwe basi maisha makamilifu hupaswa kuchukua mkondo wake kwa kila sekunde.
Uhai Ni Zawadi Ya Muda Mfupi
Haijlishi utaishi maisha marefu kiasi gani bado utamu wa uhai hufupisha urefu wote nakufanya siku yako ya mwisho utamani kulilia muda zaidi.
Hakuna awezaye kukupa zawadi ya uhai zaidi ya yule awazaye kuichua pia.Na si mwingine ila Mungu pekee,
Uhai ni zawadi yenye thamani kubwa sana kuliko zawadi nyingine zote Duniani kwa kiumbe chochote na mbaya zaidi uhai haununuliki!
Chezea vyote ila kamwe huwezi kucheza na uhai , kwamaana uhai ukienda basi kamwe haurudi!
Kuna watu wenye pesa nyingi sana ila hawana uhai halafu kuna masikini wengi sana wasio na chochote chakujivunia zaidi ya uhai pekee,
Muoneshe Mungu wako kuwa hakukosea kukuleta Duniani wala hajakosea kukuacha hai mpaka leo na kuchukua wengine kila sekunde!
Njia kubwa zaidi yakuonesha kuwa unathamini sana zawadi ambayo Mungu amekubariki nayo basi ni kuishi kwa ukamilifu kwa kila sekunde unayopumua sasa.
Kwa upande wangu mara kwa mara huwa najisemea:
“Kwakuwa nipo hai , hata kama sina kingine zaidi chakujivunia basi uhai wangu pekee hunifanya niishi maisha makamilifu kwa maana kuna siku sitokuwa nao.“

Fanya Hivi Ili Uweze Kuishi Maisha Makamilifu
- Tambua kusudi la maisha yako
Anza kwakujiuliza kwanini unadhani uliletwa Duniani au kwanini unahisi upo hai mpaka sasa?
- Andika upya malengo yako
Anza upya hujachelewa na badili ramani ya maisha yako kwa namna ambavyo unatamani kuishi upya ili kubadili historia yako
- Tumia ulichonacho
Anza na kilichopo mbele yako kabla hujataka ambacho huna na kitumie hicho kidogo kwa ukubwa zaidi
- Tafuta maana kwenye maisha unayoishi
Yape maisha yako maana ambayo yatakutafsiri wewe na namna unavyoishi kila siku na kila unachofanya kwa kila sekunde inayopita
- Fanya tathmini ya maisha unayoishi
Tenga muda wako mara kwa mara na jiulize swali moja tu kuwa ikitokea ukafa muda huu ,je utaridhika na kifo chako au utahisi kupungukiwa kwenye maisha uliyoishi?
- Fanya kidogo kidogo ila kwa ubora mkubwa
Hakikisha kila unachofanya basi kifanye kwa namna ambayo hutojutia tena wala hakitokuachia maswali yoyote
- Usiogope kukosea ila jifunze kurekebisha makosa haraka
Kosa sio kosa mpaka pale litakaporudiwa hivyo kuwa makini kwenye kusahihisha makosa yako
- Usiseme utafanya kesho, kama una muda leo
Kamwe usiweke viporo kwenye maisha ikiwa unaweza kumalizia leo basi maliza kama vile kesho hutokuwepo tena
- Epuka visingizio vya aina yoyote
Unapotaka kufanya kitu basi fanya na kamwe usianze kutafuta kisingizio bali tengeneza njia mpaka iwezekane
- Beba msalaba wako na kamwe usilaumu yoyote kwa chochote
Hata pale mambo yaendapo kombo basi jiweke kama mshutumiwa namba moja kabla hujalaumu wengine.
Mambo Mengine Yanayoweza Kukusaidia Kuishi Maisha Makamilifu
- Hata kama siku ni chungu kiasi gani, hakikisha unafuraha mara baada ya kulia
- Epuka majuto kwa namna yoyote ile na mara ugunduapo umekosea basi rekebisha kosa haraka
- Usikubali kupangiwa maisha bali fanya maamuzi muhimu ya maisha yako wewe mwenyewe binafsi
- Usiogope kujaribu kila kinachokujia akilini mwako wala usione aibu kwasababu zozote zile kumbuka maisha ni yako
- Usikubali kuingia kwenye mtego wa chuki na mtu yoyote yule wala usiwe sehemu ya maisha yao kama hawakutaki
- Kilichopo mikononi mwako kwa sasa ndio chakwako kwasasa hivyo kitumie kama vile tayari unamiliki kila kitu Duniani
- Usiishi kwa kungoja kesho wala kuwaza mambo ya jana bali angalia siku yako ya leo,muda huu ambao unao kwasasa na ishi kikamilifu.
Hesabu Baraka Zako
Hebu angalia ni vitu vingapi ambavyo unavyo kwasasa lakini wengine hawana kabisa na wanatamani kuwa navyo?
Maisha unayoishi sasa hivi kuna mtu mahala ni ndoto yake anayopambania kuiishi usiku na mchana
Hata kama wewe ni masikini sana kuna mwingine anatamani uzima ulionao tu na yupo mahala hoi taabani miaka na mika hana afueni
Inawezekana wewe ni single mother ambae unapambana kulea mtoto mwenyewe ila kumbuka kuna wanandoa wengi sana ambao hawana kabisa watoto!
Kazi mbaya uliyonayo sasa hivi, kuna watu wanakesha kuitafuta usiku na mchana bila mafanikio!
Wazazi unao waona kero leo hii kuna ambao hatuna Baba wala Mama, Bibi wala Babu!
Mwenza unaemsaliti leo hii kumbuka kuna wenzako wengi wanatamani kupata kama huyo
Hivyo basi:
- Usilazimshe vitu ambavyo bado huna uwezo navyo bali tumia ulivyonavyo kikamilifu kwanza
- Ukipata nafasi ya kutumia kitu basi kitumie kama vile unatumia kwa mara ya mwisho
- Kaa mbali na vitu ambavyo havikuhusu kabisa zingatia yale muhimu kwenye maana ya maisha yako tu
- Ishi ukiamini kuwa kama hujapata basi muda wake bado na hio isikufaye ukose raha ya maisha kamwe
- Kumbuka Dunia ina vitu vingi sana hivyo unapaswa kuchagua vyako vichache tu kisha vifanye kwa umakini mkubwa
- Hata kama una malengo makubwa kiasi gani, ishi wakati unatafuta maisha yako kwa maana usiwaze kutafuta maisha tu halafu ukasahau kuyaishi.
Jifunze Kupitia Mfano Wa Mchezaji Mpira Diogo Jota Na Mkewe
Alikuwa mchezaji mpira kutokea portuguese ambaye alichezea timu ya Liverpool FC, Huyu kaka alizaliwa mwaka 1996 na kufariki 2025 akiwa na miaka 28 pekee
Mengi yanasisimua sana kuhusu kijana huyu hasa mafanikio yake kiujumla akiwa kijana mdogo sana ila kilichonisisimua zaidi na kunipa somo kubwa sana ni:
Maisha yake ya mahusiano
Diogo alikuwa na mahusiano na mwanamke wake kwa miaka kama mitano nyuma bila kufunga ndoa ,lakini pia walifanikiwa kupata watoto 3
Mahusiano yao yalikuwa ya furaha sana baina yao wawili wala ndoa halikuwa jambo kubwa sana ambalo lilizuia wao kuoneshana upendo wa wazi
Licha ya hayo waliishi kama familia iliyokamilika na kuzaa watoto wao bila kikwazo chochote kile
Ila ajabu ni kuwa alifariki siku 11 tu baada ya ndoa yao! kwa maana alifurahia maisha ya ndoa kwa siku 10 pekee
Mke kabaki mjane kwenye ndoa ya siku 11 tu , furaha imekatishwa kama upepo wa kisuli suli na majonzi kutawala kwa muda ambao hautojulikana kwake!
Ndoto za kula mema ya ndoa zimezimika ghafla huku akiachiwa msala wa kulea watoto watatu mwenyewe! fikiria haya ni maumivu kiasi gani kwa binti huyu mdogo.
Halafu kuna binti leo hii yupo kwenye mahusiano mazuri na kijana wa watu ila kutwa ananuna kisa ndoa! utadhani aliambiwa ndoa ni tiketi ya kuingia mbinguni.
Mifano ni mingi sana
Kuna mifano ya watu wengi sana ambao walipoteza uhai mara tu baada ya ndoa zao au hata siku hiohio ya ndoa zao,
Wapo ambao walipoteza uhai mara tu baada ya kupangiwa kituo cha kazi tena baada ya mosoto wa miaka mingi bila kazi,
Vilevile kuna ambao mafanikio yao ndio yaliwaua ,mfano waliokufa kwa ajali za gari tena magari waliyonunua kwa gharama kubwa sana yakiwa kama magari ya ndoto za maisha yao.
Furahia kila sekunde ya maisha yako na iishi kikimilifu sana ili hata ukifa leo basi ubaki na kumbukumbu nzuri zakwendanazo.

Mafanikio Hayazuii Kifo Hivyo Furahi Hata Kama Hujafanikiwa
Haijalishi unataka mafanikio gani iwe ndoa , pesa ,cheo au chochote kile unachotamani kuwa nacho kwenye maisha yako
Kitu unachopaswa kuweka akilini ni kuwa hata uyapate hayo mafanikio kwa asilimia ngapi bado sio sababu yakuishi milele.
Usiwe mnyonge kisa mafanikio wala usijione si chochote hapa Duniani kwasababu tu hujapata kitu fulani,
Bali unapaswa kuishi ukiwa na tumaini kuwa kila jambo lina muda wake na jukumu lako ni kuweka jitihada pekee.
Siku ambayo utapata mafanikio yako basi pia kumbuka unaweza kuyapoteza wakati wowote na hio isiwe sababu ya kupoteza tabasamu lako.
Ikiwa Upo Hai Basi Unalo Tumaini
Mafanikio hayaandiki barua muda wakuja au muda wakuondoka hivyo tumia muda wako vyema sana huku ukiamini kuwa inawezekana
Uhai unatosha kukupa tumaini kila sekunde unayopumua na endelea kuweka jitihada bila kuchoka huku ukifurahia maisha yako,
Tumaini ni silaha ya kutochoka kwenye mapambano na vita ngumu za maisha .
Hitimisho
Leo sina maneno mengi sana ila ninakuagiza tu nenda kaishi maisha yako makamilifu kwa ukamilifu unaotaka ,
Siku zote kumbuka kuwa uoga hauzuii kifo bali unazuia kuishi.
Ukipata nafsi ya kupenda mtoto wa mtu basi mpende mpaka ahisi kuwa amechelewa sana kukufahamu!
Ukiajiriwa kwenye kazi ya mtu basi ifanye mpaka bosi kila akikuona ahisi kupagawa na kuwaza usije kuacha kazi yake!
Ukiamua kujiajiri basi hakikisha kuwa hufanyi mzaha kwenye biashara yako mpaka wahisi kama vile ulitumia pesa ya mkopo kwenye kufungua biashara!
Ukipata nafasi ya kucheka basi cheka sana kama vile hutocheka tena!
Ukipewa mualiko kwenda mahala basi hakikisha unavunja kabati kwa kupendeza ili siku nyingine uitwe tena.
Kiufupi usiyape maisha nafasi ya pili bali tumia nafasi yako ya sasa kama vile hutopata nafasi hio tena.